Umuhimu Wa Zakaah - 4: Zakaah Ya Bidhaa Na Mali Ya Biashara
Abu 'Ammaar
Zakaah Ya Bidhaa Na Mali Ya Biashara
Madhumuni ya kuzungumzia Zakaah ya bidhaa na mali za biashara ni kutokana na msukumo mkubwa uliojitokeza miongoni mwa Waislamu kuingia katika idara hii na hivyo kuwa wajibu kwetu kuweza kuwasaidia katika kufahamu majukumu yao katika darubini ya kisheria na wajibu wao katika kuifahamu nguzo hii na kuitekeleza ipasavyo hasa katika bidhaa za biashara.
Moja katika masharti ya kukamilishwa kabla ya kutolewa Zakaah ni kwamba mali iliyopo lazima ipitwe na Hawl (mwaka wa Kiislamu). Pia mali iwe ni yenye kumilikiwa wakati wa kutolewa umilikaji uliotimia. Na Zakaah itahesabiwa mwisho wa mwaka kwa kila kilichopo wakati wa kufunga mahesabu.
Biashara kwa ujumla imegawika katika aina kuu tatu zifuatazo:
1 Kuuza na kununua (jumla au rejareja).
2 Viwanda (vya kutengeneza vitu).
3 Kutoa Huduma (Services).
Bidhaa za biashara ni mali yoyote isiyokuwa dhahabu, fedha na wanyama waliotajwa ambao taratibu za kutolewa Zakaah tayari zinaeleweka. Bidhaa za biashara hutolewa Zakaah kwa kuangalia thamani yake na si bidhaa zenyewe.
Bidhaa na mali ya biashara vitapaswa kutolewa Zakaah endapo vitakamilisha masharti ya kimsingi (angalia Masharti yanayomuwajibikia mwenye kutoa Zakaah).
Aina zote tatu tulizozianisha zitawajibika kutolewa Zakaah kulingana na bidhaa, mali na biashara yenyewe.
YA KUZINGATIA
1 Bidhaa zitimize moja ya viwango vya Nisaab vya fedha au dhahabu.
2 Katika bidhaa/mali huangaliwa lengo lililokusudiwa wakati wa kununuliwa. Ikiwa lengo ni biashara basi hukmu yake ni hukumu ya biashara na itawajibika kutolewa Zakaah. Na ikiwa lengo si biashara haipaswi kutolewa. Ama lengo likibadilika katikati ya Hawl itaangaliwa lengo lililopo ili kujua hukmu yake kama itapaswa kutolewa au vyenginevyo.
3 Bidhaa hutiwa thamani kwa bei ya jumla iliyopo (whole sale) bila ya kujali bei yake kama ikiuzwa rejareja (retail rate) wakati itakapopaswa kutolewa.
4 Bei itakayokuwepo (market price) wakati wa kutimia kutolewa Zakaah (mwisho wa Hawl) ndiyo itakayozingatiwa bila ya kujali bei iliyonunuliwa (buying price) au kama bei imeshuka au kupanda (fluctuation).
5 Thamani ya bidhaa iliyopo (available stock value) ndiyo itakayoangaliwa ambayo itakuwa imeshaingizwa gharama nyenginezo kama V.A.T, kodi nyenginezo, faida na kadhalika.
6 Nia ya biashara haitakiwi kubadilika katika kipindi chote cha Hawl kwani ikibadilika na hukumu itaweza kubadilika.
7 Bidhaa za biashara zisiwe miongoni mwa mali ambazo tayari zimeelezwa viwango vyake (dhahabu, fedha, ngamia, ng’ombe, kondoo/mbuzi, na kadhalika). Ikiwa bidhaa hizi zimekusudiwa biashara na kutaka kutolewa Zakaah, itategemea na kipimo kitakachotumika.
Ikiwa Zakaah itatolewa kwa uzito/uzani basi hukumu ni ya Zakaah ya kitu chenyewe kama zinavyoelezwa. Na ikiwa ni kwa thamani basi hutolewa kwa mujibu wa Zakaah ya bidhaa na mali ya biashara kwani kigezo ni thamani yake na si kitu chenyewe.
Mfano 1
Ninamiliki duka la kuuza dhahabu. Nikiwajibika kutoa Zakaah nitaitoa ima kwa kuangalia dhahabu iliyopo uzito wake na kisha kutoa ninachopaswa au kuangalia thamani yake. Nikitoa kwa njia ya kwanza kwa uzito wake nitatoa Zakaah ya dhahabu kama ni madini na nikitoa kwa njia ya thamani nitatoa Zakaah ya bidhaa na mali ya biashara.
Mfano 2
Nimenunua gari tatu kwa ajili ya biashara na zimenigharimu £2000. Nikazisafirisha kwa £1500 na kulipia ushuru £2000. Juma ya gharama ni £5500.
Nikaziuza kwa pesa za ki-Tanzania Milioni 20 zote.
Nitakachopaswa kutoa Zakaah ni kuangalia mwisho wa mwaka je, nina kiasi gani katika hizi Milioni 20?
TANBIHI
Vitendea kazi katika biashara havijumuishwi katika hesabu ya Zakaah kwani si sehemu ya mali kama magari, vifaa vya ofisi na kadhalika.
Tutaweka jedwali ndogo ya kuainisha vitakavyopaswa kutolewa/kutotolewa Zakaah katika bidhaa na mali ya biashara.
|
MALI/BIDHAA/LIABILITIES |
ZINATOLEWA |
HAZITOLEWI |
|
Bidhaa zilizopo dukani na ghalani |
Ni bidhaa yenye kuongezeka na ipo kama ni mali |
|
|
Pesa zilizo benki na mkononi |
Ni mali |
|
|
Mzigo tumeshanunua bado upo njiani |
|
Kwa sababu bado haujamilikiwa kikamilifu (complete possession) |
|
Bima |
Ikiwa mtalipwa chochote katika pesa za bima |
Ni sehemu ya matumizi kwa pesa zinazotolewa kulipia Bima |
|
Malipo ya serikali Vat/income tax |
Hujumuishwa katika hesabu ya kutoa Zakaah |
|
|
Gharama za kuutoa mzigo |
|
Ni sehemu ya matumizi |
|
mishahara |
|
Ni sehemu ya matumizi |
|
Usafirishaji |
|
Ni sehemu ya matumizi |
|
Madeni (mnayodai) |
Ikiwa yanatarajiwa kulipwa |
|
|
Madeni (mnayodaiwa) |
|
Hamna uwezo wa kuyatolea (wataopaswa kuyatolea ni wanaowadai) |
|
Faida (Profit) |
Ni sehemu ya mali |
|
KUPUNGUA/KUPANDA KIWANGO CHA MALI/BIDHAA CHINI YA NISAAB NDANI YA HAWL.
Tulipozungumzia masharti yanayomuwajibikia mwenye kutoa Zakaah tuliainisha vipi mali ikipungua chini ya Nisaab hukmu yake inavyoanza upya kwa kuanza na Hawl nyengine. Na katika mali/bidhaa za biashara hukmu hii imeangaliwa kwa rai tofauti kutokana na ugumu wa kuweza kujua wakati ambapo Hawl itaanza. Hii ni kwa sababu katika biashara inawezekana kupungua kwa Nisaab na kupanda licha ya jitihada za mwenye kutoa Zakaah kupangilia muda wake wa kuanza Hawl.
Kuna rai tofauti kuhusu kiwango cha bidhaa za biashara kinacholipiwa Zakaah.
Rai ya Imaam Ash-Shaafi’iy na Imaam Maalik wanaona kwamba kinachozingatiwa katika kulazimu kutoa Zakaah mwishoni mwa mwaka ni thamani (ya bidhaa). Ikiwa thamani ya bidhaa za biashara iko chini ya kiwango (kinachopasa kutolewa Zakaah) mwanzoni mwa mwaka (wa Kiislam), kisha mwishoni mwa mwaka ikafikia kiwango, basi ni lazima kutolewa Zakaah. Na hii ni kinyume na Zakaah ya kitu, kwani Zakaah hiyo kwa upande wao inapasa kwa kuwepo kiwango katika kipindi chote cha mwaka. Wanasema kuwa hii ni kwa vile kinachozingatiwa katika bidhaa ni ile thamani yake ambayo ni vigumu kuidhibiti wakati wote kwa sababu ya mabadiliko ya bei zinazopanda na kushuka. Na kwa ajili hiyo, itatosha kutathmini kiwango wakati wa kupasa kutolewa Zakaah (mwishoni mwa mwaka). Ash-Shaafi’iy anasema kwamba ikiwa mwaka utakamilika na thamani ya bidhaa ikawa chini ya kiwango, basi mwaka huo hauhesabiwi, bali utaanza mwaka mwingine upya.
Rai ya Abu Haniyfah, nayo ni kauli ya pili ya Ash-Shaafi’iy, anasema: Kinachozingatiwa ni ncha mbili za mwaka (mwanzoni na mwishoni). Hii ni kwa vile utathmini wa bidhaa unakuwa ni mgumu katika kipindi cha mwaka mzima. Hivyo basi, mwanzo wa mwaka huhesabiwa kwa kuwa ndio hatua ya kuanza kufanyika kazi na kupata faida, na mwisho wa mwaka kwa kuwa (ndio wakati wa) kupasa Zakaah. Na kama bidhaa itakosekana kwa kuteketea yote katikati ya mwaka, basi hukumu ya mwaka itatenguka.
Kwa upande wa Imaam Ahmad bin Hanbal nayo ni kauli ya tatu ya Ash-Shaafi’iy, anasema: Kinachozingatiwa ni mwaka mzima kama ilivyo kwa fedha na dhahabu. Na kama thamani itapungua katikati ya mwaka, basi Zakaah haitolazimu. Na kama thamani ya bidhaa iko chini ya kiwango tokea pale anapoimiliki, basi mwaka hauhesabiwi kwa bidhaa hiyo mpaka thamani yake ifikie kiwango. Na ziada itahesabiwa sawasawa kwa kuzidi bei ya bidhaa, au kuongezeka ubora wake, au kwa kuuzwa kwa thamani (inayofikia kiwango), au kwa kumiliki bidhaa nyingine au mali zilizopelekea kukamilika kiwango (cha Zakaah).
Na rai hii ya Imaam Ahmad bin Hanbal ndio yenye nguvu zaidi kwa kuzingatia vigezo vya kimsingi katika masharti ya kutoa Zakaah.
Mfano
Nnafanya biashara na nilianza na mtaji wa 25,000 na katika mwaka nilifanya biashara ya kuuza na kununua na kuongezeka hadi kufikia 75.000.00 na nilipata hasara na kubakiwa na 30.000.00 ila kufikia mwisho wa Hawl mali ikaongezeka tena hadi kufikia 100.000.00.
Mali iliyopo mwisho wa mwaka ni............ 100,000
Fedha iliyopo kwa tunaowadai................. 10,000
Fedha iliyopo Benki ............................ 20,000
Mali inayowajibika Zakaah 130,000.00
Kiwango cha Zakaah kitakachopaswa kutolewa ni 130,000 X 0.025 = 3,250.00
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
