Haki Za Mwanamke Na Mtoto Katika Uislamu - Mtazamo Wa Masahihisho Na Utendaji
Talib Juma Ali
0.0 UTANGULIZI
Tunapoangalia matatizo yanayowakabili waislam leo katika maisha yao, kuanzia katika sheria zao, na utendaji wao tunaweza kujiuliza masuala mengi na mazito. Jee ni zenye kwenda sambamba na haki za binadamu? Jee ni zipi haki za wanawake kwa mujibu wa dini yetu ya kiislam ? Jee ni zipi hizo haki za watoto katika uislam? Jee ni sahihi kwamba uislam umeyazungumza masuala haya? Jawabu kwa hakika litakuwa kwamba vitu vyote hivi vimetajwa ndani ya uislam tangu karne kumi na nne zilizopita. Waislam watakuwa na fakhari ya kukujibu na kukusomea aya zenye kuthibitisha habari hizo ndani ya Quran na hadithi za Mtume SAW. Suala ambalo ningependa tujiulize jee hilo jawabu la kwamba uislam umeyazungumza hayo karne nyingi ni kitu chenye kutosha na kukata kiu ya muulizaji au yule anayehisi ananyimwa haki hizo? Kwa nini basi waislam leo pia wamo katika kwenda kinyume na hizo haki za binadamu wanawake, watoto na kadhalika? Inatosheleza kuwa zimetajwa na tukawa tunazikariri kama vile kasuku au kuziandikia tu katika nyaraka?
Kwa mtazamo huu katika waraka huu mfupi tunakusudia kulizungumzia suala hili la haki za wanawake na watoto katika uislam, mfumo wetu hautakua ule wa siku zote kwa kutaja vipengele vya haki na kuvieleza kimoja kimoja, kwani nahisi ni kitu ambacho kimechosha sana masikio ya wasikilizaji na macho ya wasomaji na hakika wamekwishatambua hayo, bali tunakusudia kulitazama tatizo katika zawiya nyengine kwendea katika utekelezaji namuomba Allah atusaidie kwa hili.
0.1 NINI TATIZO LA UMMA WA KIISLAM LEO?
Tatizo kubwa la umma huu sio katika kumiliki nyenzo muhimu za utendaji. Lakini kwa mujibu wa fikira zetu tatizo kubwa la waislam leo linatokana na akili zao . Akili zilizogubikwa na utando wa kufikiria milango ya kuelekea katika kheri kwa ajili ya maslahi ya umma na jamii kwa ujumla, waislam wamekosa njia bora, malengo, mikakati na wakati wa kukaa na kuizingatia ili waweze kupata kueneza khuluka na tabia njema katika jamii.
Ufahamu mbaya wakati mwengine wa dini umewafanya wengi ya wasomi wa kiislam ima kuacha sehemu zao muhimu za kimasomo na kuingia katika shughuli ya utoaji mawaidha pekee, na kudhani kufanya hivyo tayari watakuwa wameshaitumikia dini ipasavyo, wengine wakadhania kwamba, kuacha kusoma masomo ya kidunia na kujiingiza moja kwa moja katika masomo ya dini ndio kupigania dini zaidi na ndio zuhudi,[1] wakaona kufanya hivyo ni wajibu wao walioletewa duniani, kushugulikia dunia na kutafiti sheria za kimaumbile na za kimaisha katika kuleta mafanikio ya dunia ni kazi za wasio waislam. Ufahamu huu mbaya ndio uliosababisha kuleta mabadiliko mabaya katika dunia, kwani ikawa wale wasio na akhlaq za kidini wana fursa kubwa kuwaelekeza watu kwenye uasi dhidi ya Allah kwa kutumia hizo sheria za kimaumbile ambazo asili yake ni kumtumikia Allah, mafanikio ya dunia yasiyo ya kudumu yakapatikana na ya akhera yote yakakosekana. Haikupaswa kwa waislam kusahau kwamba nyanja zote za maisha zinahitajika kufanyiwa tafiti na kushughulikiwa kwa ajili ya kusimamisha dini na kwa ajili ya maendeleo ya dunia, ni vitu ambavyo haviwezi kutenganishwa kwani majaribio ya kwenda kinyume na akhlaqi njema kumepelekea mizani ya maisha kwenda kombo na kusababisha maafa makubwa ya kijamii kiafya kiaskari na kadhalika.
0.2 ELIMU ZA KISASA
Elimu zote zile za kisasa (kama zinavyoitwa) kama vile elimu jamii, elimu nafsi, elimu ya utamadumi, uchumi vyote hivi ni vyenye kuhitajika kutambulikana na wasomi wa kiislam katika kutatua matatizo ya zama zao, kufahamu elimu za mazingira ya mwanadamu na maarifa sahihi ya dini ni pekee vitakavyowawezesha waislam kukomboa umma wao. Ama ikiwa wasomi wa kiislam bado wamo katika matatizo ya kielimu na kufahamu mambo hapo hawataweza kumkomboa mwengine. Umilele wa risala hii ya uislam utabakia pale tuu ambapo tutatumia Quran na sunna katika kuleta mafanikio ya mwanadamu kivitendo. Hivyo lazima kuwa na chachu ya kuvifanya vifanye kazi kama vile inavyotakiwa.
0.3 MWANADAMU NA MABADILIKO
Kwa kuwa mwanadamu ndio lengo la mabadiliko kutokana na kazi ya ukhalifa aliyopewa na Allah na ndio lengo la ustaarabu, kwa maana hiyo Quran na Sunnah vinamlenga moja kwa moja pale zinapoeleza maana ya mabadiliko kama ile aya mashuhuri “Hakika Allah habadilishi yaliyomo ndani ya kaumu (miji) mpaka watu wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao”. Vilevile Allah akamfunza mwanadamu majina ya vitu vyote tangu asili ya kuumbwa kwake kama tunavyosoma aya mbali mbali ndani ya Quran, akafunzwa njia za kutambua uongofu na kutofautisha baina yake na shari, na akapewa uhuru wa kuchagua baina ya njia mbili hizo, na akaraghibishiwa njia bora zaidi kati ya mbili hizo, akafunzwa kuwa uislam ni kujisalimisha kikamilifu kwa unyenyekevu na kwa utiifu mbele ya Allah kwa kila alifanyalo, liwe ni moja kwa moja linafungamana na ibada, liwe la ndani ya nafsi au nje, ikiwa ni kulala kwa ajili ya kupumzika na kutafuta njia ya ibada itakuwa ni ibada, teknolojia na matumizi yake, elimu ya uchumi,tiba na nyengine vyote hivi vikitumika kwa ajili ya Allah i vitaingia katika jumla ya ibada na hapa ndipo ile dhana ya kupewa amana ya imani ya mwanadamu itakuwa imefikia lengo, kinyume chake ni ile hali tuliihadharisha ya kupotea mizani ya kheri katika dunia.
Lengo la maelezo haya ni kuweza kutufikisha mahala kuona ni wapi sisi waislam tupo katika kutaka kujenga misingi mizuri na madhubuti ya mustaqbala wa mwanadamu kwa ujumla na hasa kwa muislam kwa , tukiwa na dhana sahihi kwamba wanadamu wote ni wenye kuhitajia ubora wa dini hii na mafunzo yake matukufu yenye maslahi kwao hata kama wangelijipangia maslahi yao wao wenyewe, haya hayawezi kutokea pasina kutokea mabadiliko makubwa katika nafsi ya mwanadamu.
Mabadiliko ni kugeuka kutoka hali na kwenda hali nyengine ima iwe bora au mbaya. Ili kujenga jamii mpya suala la mabadiliko ni la lazima, kwa maana jamii kwa ujumla inatakiwa iwe na muelekeo wa kupendelea mabadiliko hayo kwa kuona umuhimu wake, akili mpya katika kuleta mabadiliko ni lazima na hapa tunakusudia kuonyesha kwamba wakati mwengine katika jamii wanaweza wakaweko wasiona umuhimu wa mabadiliko, na wengine wakaona hivyo, hali hii inatokana na tofauti ya thaqafa baina ya wawili hao, mmoja akahisi hali iliyopo ni lazima ibadilike kwa kuwa shida zimeongezeka, mazingira yamebadilika n.k. Mwengine akahisi kufanya mabadiliko hakuhitajiki, mambo yalivyo kwa mujibu wa mtazamo wake ni kawaida na watu wamo katika raha, katika hali zote hizi mbili tunapaswa pia kuangalia suala la ukweli na ikhlasi. Upande wetu tukiwa ni waislam tunaoishi katika zama hizi za maalumati na mwendo wa kasi katika kila kitu, ni wajibu kulitazama suala la mabadiliko na kujiuliza jee tunayahitajia? Baada ya jawabu ambalo bila ya shaka ndio, kazi kuu itakuwa ni kuangalia misingi ya mabadiliko hayo kwa mujibu wa misingi na mafunzo ya dini yetu, mabadiliko hayo ni lazima yawe yanatoka ndani ya nyoyo zetu na kwa azma na irada na matakwa yetu wenyewe, yasiwe ni yenye kusababishwa na vishawishi vya muda mfupi au matukio mafupi, na hata ikiwa vishawishi au matukio ni visaidizi vya mabadiliko basi iwe ni kwa ajili ya kujenga hiyo azma na irada na matakwa, kwa maana nyengine iwe ni njia kwendea mabadiliko makuu ya kudumu .
0.4 KWA NINI TUNAHITAJIA MABADILIKO.
Jawabu:
· Tunataka mabadiliko kwa ajili ya kuongezea ujuzi.
· Tunataka mabadiliko kurejesha imani ndani ya nafsi zetu kuwa sisi ni umma bora, umma wa kuamrisha mema na kukataza mabaya na ni umma wa imani.
· Tunataka mabadiliko ili kuweza kutoa maamuzi sahihi katika utekelezaji wa maamrisho ya dini yetu.
Mambo yatakayoweza kutuzuia na mabadiliko na lazima kujepusha nayo:
· Kuvunjika moyo kwamba mabadiliko sio kitu kinachowezekana kwa sababu waislam wanahitilafiana sana katika masuala yao.
· Uvivu unaowapelekea waislamu kushindwa kuendelea katika nyanja mbali mbali ziwe katika masuala ya kidini au hata ya dunia.
· Matatizo ya kifamilia yanayowafanya wakose fursa ya kukuza viwango vya fikira na ubunifu katika kupambana na matatizo.
· Kubakia daima katika makosa hayo kwa hayo pasina kujirekebisha.
· Kufikiria kuwa maisha ya dunia hayana faida kwa muislam.
· Kutojipima na wenzio waliosonga mbele katika nyanja mbali mbali na hivyo kukosa chachu ya maendeleo.
· Mazingira mabaya yaliyomzunguka (kukosa watu wenye akili zilizo tayari kubadilika -taasubi-).
Ili tuanze kubadilika hatuna budi na kutambua kwamba mabadiliko hayawezi kupatikana katika jamii yoyote au kwa mtu yeyote mpaka kwanza zitangulie fikira, kitu ambacho ni dharura katika kusimamisha ustaarabu kwa kila umma, na ndio tukakutia kwamba katika uislam Mtume SAW anasema -kila anaezaliwa anazaliwa katika fitra na wazee wake ndio wanaomfanya awe myahudi au mnasara-; kwa maana wao ndio wanaompa fikira, hivyo tunakutia kuwa wazee ni wenye nafasi katika kumjenga au kumbomoa mtoto, hii inatokea kabla mtoto huyo hajapata visaidizi vya nje au kama tulivyotaja mwanzo vina nafasi yake katika kukuza mawazo ya mtoto na inawezekana kumfanya awe ni sehemu mbaya ya jamii , akawa ni muislam asie na matunda bora na muislam asietakiwa na uislam, ama kinyume chake atakuwa muislam wa kupigiwa mfano , kwa tabia zake njema, atoe matunda ya kheri na ndivyo anavyotakiwa awe. Mabadiliko kuelekea kwenye uzuri ni suala la kila mmoja wetu na hasa kwa wale wenye taasisi ambazo zimekuwa na risala kubwa na hapa na kusudia sisi waislam kwa ujumla, ambao risala yetu, ni daawa kwa kila mtu. Lazima waisome risala yao vyema na kuitengeza vyema na kuituma vyema kwenye umma na kuwa na matumaini kwamba ikiwa risala itatumiwa vizuri na kupokewa vyema na umma tukaujengea irada na matakwa bila ya shaka utabadilika, kwa kuzingatia kwamba hakuna mtu anaeitakia shari nafsi; ama yule afanyae shari ni kwa sababu tu ametezwa nguvu na mwisho kukubali hoja dhaifu za iblis na kushindwa kuzingatia vyema na hii ndio maana ya kufuata matamanio, ama pale mtu ikimbainikia wazi kwamba alikuwa ni mfuasi wa shetani atasema “Laiti tungalikuwa tunasikia na kuwa na akili tusingalikuwa katika watu wa motoni” .Almulki –10.
Ama masuala ambayo daima tutakuwa tunajiuliza:
Jee ni kweli tunataka kubadilika kuelekea kwenye mazuri na kutekeleza amri za dini vyema?
Jee tunaweza kuwa bora zaidi kuliko hivi tulivyo katika kutekekeza haki za kijamii ikiwa ni watoto au wanawake?
Jee tunazo barnamiji na malengo ya kutaka kufikisha haki za watoto na wanawake kiuadilifu na sio kwa mila na desturi ambazo inawezekana zikawa wakati mwngine ni nje ya uislam?
0.5 KUBADILIKA NA KUTEKELEZA WAJIBU
Katika kuwafanya watu wabadilike na kutekeleza wajibu wao kama walivyotakiwa, tujue wazi kuwa kazi yetu ya kimsingi ni kuwajengea mazingira mazuri ili wabdilike na inawezekana wakati mwengine wakatokea watakaokataa kubadilika kwa sabsabu mbali mbali zikiwemo tulizozitaja mwanzo au kwa kutofahamu maana na umuhimu wa mabadiliko au kwa sababu kuu ya kiungu “Hakika wewe humuongoi umpendae lakini Allah anamuongoa amtakae” .
Umma tunautaka utambue kuwa lengo la mabadiliko katika dunia ni mwanadamu mwenyewe, pindipo atabadilika kwendea katika kheri basi mazingira yatamtumikia na hatakuwa mtumwa wa mazingira, mwanadamu lazima kwenda mbali katika kuzisoma sunna za maisha katika kuleta mabadiliko, mfano ikiwa unataka kumlea mtoto vyema leo hii nini cha kufanya ni wende moja kwa moja na Quran na Sunna. Au pia utumie visaidizi vyengine. Ikiwa unataka tiba ya maradhi mbali mbali basi utumie habasauda pekee na asali kama wanavyodhani wengi. Au hata kukuza utafiti katika hiyo habasauda na asali? Jee ni vibaya kugundua sunna nyengine za kimaumbile katika tiba? Hakika wale ambao watatumia vyema sheria za kimaumbile na kujua siri zake na wakafungamanisha na mafunzo ya dini yao vyema ndio watakaokuwa na uwezo wa kufikisha risala hii katika usahihi, kama alivyosema Imam Ghazali alipoonyesha umuhimu wa elimu zilizokuwepo wakati wake akasema, atakaekuwa hajui kemia au hisabati hataijua dini isipokuwa juu juu tu. Ama pale dini itakapokuwa imetenganishwa na elimu muhimu za kisasa tujue kwamba ulazimishaji na ikraha wa kufuata masuala ndio utakaokuwa juu na sio kufahamu na kukinai, ama hasara itakayotokana na haya ni waislam kuvutwa na maadui ambao watakuja na mbadala ambao utakuwa unaonyesha maslahi mazuri dhahiri yake na sumu batini yake.
0.6 WIMBI LATUKUMBA
Sababu ya kutowajibika vyema imepelekea wanawake wengi wa kiislam na miongoni mwao wasomi kububurwa wimbi la kutaka kumkomboa na kumsimamia mwanamke haki zake, katika kufanya hivyo wakachukua ufumbuzi usiotokana na asili ya dini yao bali ni mtazamo wa kimagharibi moja kwa moja au uite wa kidunia ukitaka ambao hauzingatii zaidi suala la akhlaqi za kidini bali ni wenye kutizama upande wa maslahi ya kidunia pekee, tunaweza kusema kwamba umepata nguvu kama zilivyo fikira zote zenye vipodozi bandia. Lakini tusiache kukiri kwamba wakati fulani sisi wenyewe waislam tumekuwa ni vichochezi wa hayo kwani tumekuwa ni wasimuliaji zaidi wa haki za mwanamke lakini pasina utekelezaji. Kwa sababu haja ya mwanadam ya kutambulikana ni muhimu hivyo wanawake wetu wamebeba fikira na kuzitumikia kwa hesabu yoyote ile hata kwa kupoteza dini yake na kumuweka pabaya zaidi mwanamke na kumfanya awe ala ya wanaume zaidi,[2] na kutumiliwa kwa maslahi ya kimwili ya wanaume kufedheheshwa katika matangazo ya biashara kuondoshewa malezi ya nyumbani kuonekana sio kazi, kuweza kukataa kuolewa lakini akaziniwa na kila mmoja masuala ya uhuru wa utoaji mimba n.k. Ama haki za kimsingi za mwanamke ambazo hatutazichambua na nyengine tunaziachia ukumbi uzijumuishe ni kama hivi:
-Haki ya kuwa ni sehemu ya umma.
-Haki ya ibada usawa mbele ya sheria.
-Haki ya kuishi (kosa la kuua mtoto hai wa kike).
-Haki ya kumiliki na kufanya biashara.
-Haki ya kushiriki katika ujengaji wa ustaarabu na maendeleo ya umma wa kiislam kwa maana pana ya maendeleo pasina kuchupa mipaka ya sheria na adabu za uislam.
-Haki ya mirathi (na kufahamu vyema hekima zake za tofauti ziliomo)
-Haki ya elimu.
-Haki ya ndoa (kuanzia uchumba, ).
- -Haki ya kusafiri kwa kuweko vidhibiti vya kisheria.
-Haki ya kutunzwa na mumewe akiwa yuko na mume (kustarehe na mumewe,mavazi, kula, matumizi mengine kiujumla).
-Haki ya kuheshimiwa (kutofanywa chombo cha kujistarehesha nje ya ndoa ).
-Haki ya kujistiri mwili wake asiwe ni kichochezi cha maasi.
-Haki ya kiafya.
0.7 HAKI ZA MTOTO
Kwanza tukumbuke kuwa familia katika uislam ni yenye kuanza kwa kukutana mke na mume kwa njia ya kisheria ya ndoa, pia tunaweza kuongezea kwamba familia katika uislam inaanza mapema kabla ya hapo yaani tangu pale pande mbili zinapotafuta rafiki bora wa kuoa au kuolewa nae, ambae kupitia huyo na maana ya kuoa au kuoana itakamilika na maslahi yatapatikana, kama alivyotutaka Mtume SAW kutafuta konde nzuri za kupanda mbegu zetu, pamoja na kuthibitisha kwamba ameangamia yule atakaemtafutia mtoto wake wa kike mume mbaya, na hapa ndipo inapokuja ile misingi mikuu ya kujenga familia katika uislam.
Katika kutafuta kusimamisha misingi mikuu ya familia hatuna budi kwanza kuangalia umuhimu wa misingi ya haki za kibinafsi ambazo zikijengeka vyema haki zote nyengine ziwe za mume kwa au mke kwa mume au haki za wanawake au haki za watoto zitasimama. Ama misingi ya haki za mtu binafsi zinabainika katika vipengele hivi:
Kabla hatujavitaja tujikumbushe tena lengo la mafunzo ya Quran na Sunna ambalo ni kuleta mabadiliko ndani ya nafsi na akili ya mwanadamu na kumpata mwanadamu mwenye imani na tabia njema, mwenye elimu inayompelekea kwenye woga halisi na utendaji ulio madhubuti utakaopelekea uimarishaji wa ardhi hii na kuufanya ustaarabu wake na alama za ustaarabu huo ikiwa ni fasihi, majengo na kadhalika ni vyenye kuonyesha sura safi ya itikadi na fikira pevu zenye kutambua lengo la mwanadamu duniani, na ndio maana tukawa tunasisitiza upatikanajia fikira safi kabla utendaji, na vipengele vyetu muhimu vya haki za mtu ni kama hivi:
1-Malezi muhimu ya kiroho yakizingatia sifa kuu ambazo uislam daima umekuwa ukizifundisha kupitia Quran na Sunnah:
· -Taqwa.
· -Kupendelea kheri.
· -Udugu.
· -Usamehevu.
· -Huruma.
· -Ushujaa na kujiamini.
2-Baada ya sifa hizi sita kuu unakuja wajibu na haki za mtu binafsi ndani ya jamii kuanzia jamii ndogo ya nyumbani na kumalizikia jamii kubwa inayomzunguka mfano:
· -Haki za wazazi wawili.
· -Haki za ukoo (kuunganisha).
· -Haki za ujirani.
· -Haki za kuitumikia nchi kwa ajili ya maendeleo.
· -Haki ya kuamrisha mema na kukataza maovu.
· -Haki na adabu katika mazungumzo kunywa kula ……
Suala jengine muhimu baada ya kuangalia misingi ya haki kwa mtu binafsi ni misingi mikuu ya kujengea familia na tunaweza kuijumlisha kwenye vipengele hivi:
· -Kwenye kuchagua wa kuolewa au kumuoa.
· -Hukumu za kuposa na ndoa na yanyaambatana nayo.
· -Kuishi vyema ndani ya nyumba na mahusiano ya kimwili.
· -Mimba na vipi ilelewe.
· -Hukumu zinazoambatana na mtoto baada ya kuzaliwa (jina, kunyonya, kuadhiniwa, kurambishwa kitu kitamu n.k).
· -Malezi .
Mifano bora bora ya kuanzisha familia na vipi ziwe tunaikuta ndani ya Quran. Tukizingatia vyema na kufaidika na kisa cha Nabii Mussa kuanzia kunyonya, kulelewa kwake na kadhalika kama tunavyosoma katika Surat Alqasas , Kisa cha nabii Issa , kisa cha Nabii Yousif kama kilivyokuja kwa ukamilifu katika surat Yousif, visa vyote hivi vina mafunzo mengi ya misingi ya familia pamoja na haki za watoto katika uislam, na tunarudia tena kusema kwamba sio lengo letu kutaja kuwa vimo tu lakini lengo kuu ni kutumia faida hiyo kivitendo na kuwa ni wenye kutekeleza majukumu yetu zaidi, ili kujiepusha na fikira zitakazotupelekea katika kuvunja mshikamano wa kifamilia na kujenga familia zenye kukataa ndoa, kukataa watoto, kukataa wazazi na kuwaweka kwenye majumba ya wazee na kuwapelekea zawadi siku za sikukuu, tukawa tayari tumo kwenye kuvutwa na mastarehe, lazima tujihadhari na kuutazama ulimwengu kuwa ni uwanja wa fujo na starehe kuliko kuwa ni jukumu kabla ya kila kitu.
Mtoto katika uislam ni chumo la mahusiano sahihi ya ndoa, kwa kuwa uislam umechunga atafutwe vyema kabla ya ndoa kama tulivyoonyesha na wakati wa kutafutwa iwe kwa dua maalum, hivyo hivyo ndio umemuekea haki haki zake ili aje kuwa mtoto bora wa kuweza kumuombea dua nzuri mzee wake pale anapokuwa mkubwa au amekufa, na wawe hao wazee wawili ni sababu ya kuingia kwake peponi.
Tatizo kubwa linalowakabili wengi ya watoto leo ni kwamba wanaishi wakiwa ni mayatima ndani ya nyumba zaidi, hii inatokana na mashirikiano na mahusiano madogo yaliyopo baina ya wazee, mambo yanayowakoroga watoto na kujenga mitazamo mibaya ima kwa wazee wote wawili au mmoja wao, hivyo kuanza kubadilika na bila shaka mabadiliko haya hayatakuwa kuendelea kwenye uzuri bali moja kwa moja ni kuendea kwenye ubaya. Wakati mwengine uyatima huu wa ndani ya nyumba inawezekana wazee ni wenye kuishi pamoja vizuri lakini wakawa hawana nafasi ya kukaa na watoto wao kwa sababu ya kazi nyingi hivyo mayaya na walezi wakawa ndio wanaochukua nafasi ya malezi kama vile wanavyotaka wao na fikira zao. Haya ni matatizo yanayotukabili katika umma huu wenye kutaka watu wake wafanye kazi. Wakati huo huo dini na miongozo yake vinataka vifuatwe, haya ni yenye kuhitaji ufumbuzi wenye kwenda na maisha yetu ya leo na kwa mujibu wa dini.
Baadhi ya mifano ya haki za watoto
· -Kutafutiwa mama na baba wazuri.
· -Kupewa jina zuri.
· -Kunyonyeshwa.
· -Kusomeshwa na kufunzwa kutambua yale yenye kumfaa duniani na akhera.
· -Kujua haki za kijamii na wajibu wake.
· -Kumpatia mtoto wasaa wa kucheza.
· -Kumfunza vipi kutumia wakati wake wa faragha kwa ajili ya manufaa .
· -Kumtafutia njia bora za kukuza akili zao.
· -Kutambua uhodari na udhaifu wao na kubuni njia bora za kuwasomesha.
· -Kufunzwa umuhimu wa ibada.
· -Kumpongeza anapofanya zuri na kumrekebisha anapokosea na ikiwa kosa linastahiki kuchapwa iwe ni kwa mujibu wa kosa sio kumkandamiza.
UMUHIMU WA HAKI YA KUNYONYESHA
Haki zote hizi ni muhimu na zinahitaji maelekezo mengi lakini tuchukue mfano mmoja wa kunyonyesha:
Tukichukua mfano huu na kutaka watu wageuke na kufuata vyema hasa katika zama zetu hizi ambapo suala la kunyonyesha limekuwa likijengewa falsafa kubwa kubwa, kama vile kunyonyesha kunaharibu uzuri, tunaweza kufanya benki ya maziwa ya mama kama vile ilivyo benki ya damu, jee haya hayataharibu sheria za udugu wa kunyonya. Masuala haya na mengi mengine tunapaswa kuwa na elimu nayo pamoja na kujua faida za kunyonya kwa mama moja kwa moja kiafya na kijamii kutambua elimu za afya pia kutasaidia leo kuwafahamisha watu umuhimu wake.
0.8 HITIMISHO
Natarajia kwa waraka huu mwepesi wa fikira mwingi wa matumainio utachangia katika kuibua haki tofauti za wanawake na watoto katika uislam na kuzitafutia misingi madhubuti ya kiutendaji, jambo ambalo limeupa ugeni uislam. Hakika watakua ni wenye chumo zuri wale watakaourejeshea uislam nafasi yake katika jamii, licha ya kuonekana ni wageni machoni mwa wengi, anasema SAW “Hakika umekuja uislam katika ugeni na utarejea tena katika ugeni na bishara njema kwa watakao kuwa wageni (watendaji).”
Wabillahi Tawfiq
[1] Zuhudi kwa maana ya kuacha dunia na kutumikia akhera
[2] ziada ya haya yamo katika makala yetu ndugu yangu mwanamke wa kiislam amka)
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


