Kilio Majumbani Mwetu
Ummu Hannaan
BismiLLaahir-Rahmaanir-Rahiym.
Naanza kwa jina la Mola wetu Aliyetumba waume kwa wake ili tumuabudu Yeye na Akazipanga sheria kwa mujibu wa darja zake, na kumpa mwanaume uwezo mkubwa wa kutuchunga na kutulinda sisi wanawake pamoja na familia kwa ujumla.
Nasikitika sana hapa katika jamii yetu Uingereza kila nikizungumza na kina mama wenzangu utasikia matatizo tuliyonayo yanafanana. Ni matatizo tanayowapata kutoka kwa waume zao ambao waume hao ndio wanatakiwa wawaongoze wake zao. Ni jambo la kusikitisha sana kukuta mama yeye ndiye kashika khatamu anaiongoza nyumba nzima pamoja na kumuongoza baba mwenye nyumba.
Ni hali ya kutisha sana na inafaa tuzingatie sana na wala tusiidharau, kwani utakuta hata watu waliosoma dini pia wanaongozwa na wanawake. Sio vibaya kuongozana lakini iwe kwa njia ya kusomeshana au kukatazana pale pindi mtu anapotaka kukosea lakini utakuta sio hivyo kabisa.
Baadhi ya majumba yetu wanawake wengi wako hatarini kwa kukosa uongozi mzuri wa waume zetu. Furaha inatoweka ndani ya nyumba kwa wanaume kukosa imani kwa wake zao na kujiona wao ni mabwana hawapaswi hata kutoa msaada mdogo unapohitajika. Je, nyumba kama hiyo itakuwa na mapenzi kweli au watu wataishi tu kuendeleza maisha kwa kuwa wamezaa?
Wanaume ndio wahimizwe kusali, wanawakejeli wake zao wanapofata sheria za hijaab, kutosikiliza muziki na hata kuwa hawaendi katika sehemu za starehe na kuacha marusha roho, kufikia hadi ya kuwaambia wanawake hao wamechanganyikiwa. Kweli hivi ndivyo tulivyoagizwa na Mola wetu na yako wapi mafunzo ya kipenzi chetu Muhammad Sallallaahu alayhi wasallam?
Nilikutana na mama mmoja na katika mazungumzo naye, alikuwa akilia kwa uchungu na kusema: “Sisi tumeolewa kwa ajili ya kuwa na furaha au kuwa ni wafanyakazi wao wa ndani hawa wanaume?” Anasema yeye kazi yake ni kufua, kupiga pasi kulea watoto na kupika. Mume akiingia ni kula kulala na kutoka kwenda kwa marafiki tu hana mapenzi hata ya kumwambia mkewe: “Mke wangu leo chakula kizuri”
Kwa upeo wangu naona yote haya yanasababishwa na ukosefu wa elimu.
Wanaume hawapewi mafunzo ya kutosha wanapotaka kufunga ndoa jambo ambalo ni muhimu sana wafunzwe vipi kuishi na wake zao, kwa kutolewa mfano mzuri kabisa wa Mtume Sallallaahu alayhi wasallam na Maswahaba.
Kisha juu ya hivyo, hawataki kuhudhuria katika mawaidha na madarasa pia ambayo yanachangia kusaidia katika kumfunza mtu elimu nyingi anazozihitaji katika kuendesha maisha yake.
Jambo hili limeghafilika kwa kwa Mashekhe ambao aghlabu yao wanatoa mawaidha mengi kuwaonya wanawake zaidi kuliko wanaume kiasi ambacho kinawafanya wanaume wasitambue makosa yao na waache kufanya ihsaan na wawe na Rahma kwa wake zao. Siku zote nyumba ikivunjika anashutumiwa mke tu ilhali pengine ukorofi unaaza kwa mwaname mpaka kufikia hali ya kuachana.
Tuna jukumu ya kulifikiria jambo hili hasa katika nchi hii tuliokuwepo kwani wanawake wanazidi kuwa wajeuri na kukosa nidhamu kwa vitimbi vya waume zao majumbani mwao.
Naomba samahani kwa yeyote atakayesoma makala hii na ikamgusa.
Kwa kweli sio kusudio langu kulaumu au kuyaeleza haya bali kutokana na malalamiko mengi yanazidi ya dada zetu. Hivyo imekuwa ni wajibu wetu kujaribu kuyasawazisha kwa kutoa nasaha kama hizi tukitegemea kuwa nasaha zetu zitasikilizwa na kufuatwa ili uweko uwezekano wa kusalimisha ndoa zetu majumbani na kubakisha majumba yetu kuwa katika furaha, mapenzi na amani InshaAllaah.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


