Mwanamume Kufanya Kazi Ya Kuonyesha Mitindo Ya Mavazi

 

SWALI:

Ama baada ya kumshukuru M/Mungu S.W na kumtakia rehma Alhabib Almustaffa S.A.W. A/alkm ndugu muislamu, naomba kupata jawabu la swali lifuatalo.

Ni halali ama ni haramu kwa Mwanamume kufanya kazi ya modelling? Yaani kuonesha mitindo ya mavazi, na mavazi yenyewe ni yale yenye kustiri.

A/alkm.

 


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Kawaida ambayo inafaa kufuatwa katika kustarehe na vizuri vyote vikiwa ni katika vyakula, vinywaji au mavazi, ni kujiepusha na kufanya ubadhirifu na majivuno katika matumizi. Israfu ni kukeuka mipaka katika kustarehe na vya halali, na kiburi ni jambo la moyoni zaidi kuliko machoni kwani linahusika na niya ya mtu nacho humfanya mtu kukusudia kujivuna na kujifakhirisha mbele za watu, na Allaah Aliyetukuka Hampendi mtu kama huyo kama isemavyo Qur-aan: "Na Allaah Hampendi kila ajivunaye, ajifakharishaye" (57: 23).

 

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mwenye kuburuta nguo yake kwa majivuno, Allaah Hatomtazama mtu huyo Siku ya Qiyaamah" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa hiyo, ili Muislamu ajiepushe na kudhaniwa kuwa ni mwenye kiburi, Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) alikataza kuvaa nguo za fakhari ambazo zitasababisha watu kufakhiriana na kushindana na kujivunia mapambo yao, kama alivyosema katika Hadiyth ifuatayo: "Mwenye kuvaa nguo ya fakhari hapa duniani, Allaah Atamvisha nguo ya idhlali kesho Akhera, kisha Ataiwashia moto" (Ahmad, Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

Baada ya maelezo hayo hapo juu utapata uwiyano na yale yanayofanyika katika kazi ya mtindo wa mavazi ‘modelling’. Nayo ni kama yafuatayo:

  • Kunafanyika ubadhirifu (israfu).

  • Kuna uburuzaji wa nguo.

  • Utapata mchanganyiko wa jinsiya (wanaume kwa wanawake).

  • Pia utapata utumiaji wa pombe na muziki (kwa sababu inaonyesha swali lako linahusu mitindo ya mavazi yasiyo ya Kiislam wala yanayoendeshwa kwa nidhamu ya Kiislam).

  • Nguo zenyewe si za kawaida bali ni za upeo wa fakhari.

  • Huenda akaingia katika kiburi kwa kuingia katika mambo yaliyokatazwa.

  • Kutembea kwa wenye kuonyesha hiyo mitindo wakati wa uonyeshaji mitindo ni kwa njia iliyokatazwa. Wanatembea kwa maringo na kujilegeza mwili wao wakiuita mwendo huo ‘mwendo wa paka’, hali ya kuwa Allaah Amekataza watu kutembea hivyo. Tazama Surah Luqmaan Aayah 18. Allaah Anasema: “…wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika Allaah Hampendi kila anayejivuna na kujifakharisha Na Anasema tena Allaah Aliyetukuka katika Surah Al-Israa (Banuu Israaiyl) Aayah ya 37: Wala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima

Kwa vidokezo na maelezo yaliyo hapo juu, ufanyaji wa kazi hii haukubaliki katika Sheria.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share