Skip navigation.
Home kabah

Mzazi Na Malezi Ya Watoto: Jinsi Ya Kudhibiti Magomvi Na Ushindani Wa Watoto

Imefasiriwa na Ummu Ashraf

 

Pale ambapo pana watoto wawili au zaidi katika familia, ushindani baina au kati yao ni jambo lisiloweza kuepukika. Husuda ni sifa ya kawaida katika nafsi za wanadamu. Watu wanapoyatazama mafanikio ya wengine, huwa na hisia za aina mbili;

Baadhi hutamani na wao wapate mafanikio kama hayo waliyoyapata wenzao na hivyo hujitahidi kufanya kazi ili watimize tamaa hiyo. Lakini wengine hutamani wenzao waharibikiwe. Nafsi zao zinaumia wanapoona mafanikio ya wenzao.

Watu hawa hawapendi kabisa kuona fulani kafanikiwa bali hufurahi kuona fulani kaharibikiwa. Nafsi zao hufarijika wanapoona wenzao wakiharibikiwa. Hii ni aina mbaya sana ya husuda ambayo dini ya Uislamu imekataza kabisa.

Mtume (Salallahu alaihi wasalam) amesema: “Jihadharini na husuda kwani husuda huteketeza mema kama moto unavyoteketeza kuni”.

Si jambo la ajabu kwa watoto kuoneana wivu. Jukumu la mzazi ni kuudhibiti wivu huo na kuuweka ndani ya mipaka sahihi. Kwa kweli ni muhali kuufuta kabisa wivu huo. Kuna kazi kubwa ya kisaikolojia katika kuweka sawa mizani ya hisia ndani ya nyoyo za watoto ili kila atakayepata kitu, basi mwingine aone pia ni cha kwake na hivyo asione husuda.

Kisaikolojia, mzazi makini anaweza kugundua hisia za watoto bila wao wenyewe kujua na kuzitafutia njia sahihi ya kuziweka sawa. Ukiona mtoto anahamanika kuona mwenziwe kapata kitu fulani au ukiona mtoto kanyongea kwa sababu mwenziwe kapata kitu fulani, jua kwamba una kazi ya kusawazisha hisia za mtoto huyo ili  ahisi kuwa cha nduguye ni chake. 

Mzazi akifanikiwa kufuta husuda miongoni mwa watoto wake, atakuwa ameandaa watoto wenye nyoyo ambazo hazitadhikika kwa kitu cha mtu. Na kwa mujibu wa Hadith ya Mtume (Salallahu alaihi wasalam) tuliyoinukuu, hawa ndio watoto ambao nyoyo zao zitakuwa makazi ya imani sahihi ya Kiislamu.

Ni watoto ambao hawatababaika au kuhamanika kwa chochote cha mtu. Wataridhika na ‘kidogo’ au ‘kibaya’ chao, na kukinai ‘kingi’ au “kizuri” cha wenzao. 

Moyo wenye husuda si moyo wa Kiislamu. Muislamu hata akiswali Swala zote za faradhi na za Sunna, bado atakuwa na upungufu mkubwa katika uchaMungu wake ikiwa moyo wake hauna uwezo wa kujiepusha na husuda.

Maswahaba walikaa na Mtume (Salallahu alaihi wasalam), akapita mtu fulani, Mtume akasema, “mmemuona mtu wa Peponi”. Mtu huyo akapita tena zaidi ya mara mbili na kauli ya Mtume ikawa hiyo hiyo. Swahaba mmoja akatumia mbinu za kwenda kumpeleleza mtu huyo ili kuona ana nini cha mno cha kumuingiza Peponi.

Akakaa nyumbani kwa mtu huyo pasina kuona mambo mazito sana ya kiimani. Hatimaye ikabidi amuulize vizuri kuhusiana na ile kauli ya Mtume. Mtu huyo hakuwa na sifa kubwa sana bali moja ya sifa chache alizokuwa nazo ni kwamba moyo wake haukuwa na husuda.

Mantiki ya mfano huu ni kwamba, ilikuwa ni changamoto ambayo Mtume (Salallahu alaihi wasalam) aliwapa Maswahaba. Kwamba mambo yote mazito ya kiimani waliyoyafanya yalikuwa na shabaha ya kuutakasa moyo, uwe safiglasi, uepukane na kila aina ya uchafu ikiwemo husuda.

Kinyume chake kama wangeshindwa kuepukana na husuda, basi licha ya mambo mazito ya kiiamni waliyokuwa wakiyafanya, bado wangezidiwa ubora na yule mtu mwenye mambo machache tu lakini ameepukana na husuda.

Hivyo, kimsingi, jambo hili lishughulikiwe mapema utotoni. Hisia za husuda zipunguzwe makali kama si kufutwa kabisa tangu utotoni. Jambo ambalo wazazi wanapaswa kuwa makini nalo ni kwamba, wakati mwingine mzazi anaweza kumpenda mtoto mmoja zaidi ya mwingine kutokana na sifa fulani ambazo mmoja anazo na mwingine hana.

Mzazi lazima awe makini sana, asidhihirishe hisia zake japo hana namna ya kuepukana nazo. Asioneshe hata ishara ndogo kuwa anampenda mmoja kuliko mwingine.

Katika kisa cha Nabii Yusuf, Qur’an inatupa mfano wa ushindani wa ndugu. Nduguze Yusuf waliona kuwa baba yao alimpenda zaidi Yusuf kuliko wao. Baadhi ya Mufasiruna wanasema kuwa Nabii Yaqub alikuwa na mapenzi na uangalizi maalum kwa yusuf.

Labda kwa sababu alikuwa mziwanda (kitindamimba) au kwa sababu alikuwa amefiwa na mama yake au kwa sababu Yaqub aliona ishara kubwa kwa Yusuf juu ya maisha yake ya baadae.

Vyovyote ilivyokuwa, nukta yetu ni kwamba nduguze Yusuf walidhikika kwa husuda juu ya mapenzi ya baba yao kwa mwenzao kiasi kwamba wakaona labda ufumbuzi ni kumpoteza Yusuf kwa kumtumbukiza Kisimani, wakiamini labda kutokuwepo kwa Yusuf kungerejesha mapenzi ya baba yao kwao.

Kwa hatua hii ya kuthubutu kufanya mauaji, tunaona kuwa husuda ni uovu wa hatari unaoweza kuleta maafa. Mtume (Salallahu alaihi wasalam) amehimiza kuwa watoto wote watendewe sawa sawa. 

Labda mzazi hatalaumiwa ikiwa ataonesha mapenzi zaidi kwa mtoto mwenye tabia njema ili yule mwenye tabia mbaya ajirudi na kuweza kupata mapenzi ya mzazi wake kama mwenziwe.

                                            Sababu za husuda

Wanasaikolojia wanasema kuwa pale anapozaliwa mtoto, yule mtoto ambaye alikuwa wa mwisho kabla ya kuja kichanga hicho, huingiwa na hofu. Yeye alishakuwa amezoea ile hali ya mzazi kumtazama au kumjali zaidi lakini sasa kaja mtoto mwingine wa kuhamisha hali hiyo kutoka kwake.

Wazazi sasa wanahamishia mapenzi yao kwa mtoto mpya. Hali inakuwa hivyo kwa mtoto kwa sababu ya kutojua kuwa mzazi ana mapenzi ya kutosha kuwagawia sawasawa watoto wake wote.

Wanasaikolojia wanapendekeza njia zifuatazo katika kupunguza wivu unaoweza kuzaa husuda kwa watoto:

1)  Ongea na mwanao kabla mtoto mpya hajaja. Muandae kwa maneno mazuri ili awe tayari kumpokea mtoto mpya. Nyumba yaweza kupatwa na hamasa kubwa kiasi kwamba mtoto huanza kumpenda mdogo wake kabla hajaja. Kwa hali hii sio tena yeye apiganie nafasi yake katika mapenzi ya mama yake, bali  na yeye atachangia mapenzi yake kwa mtoto. Sio tu mzazi atakayemuangalia na kumbembeleza mtoto bali mtoto naye atakuwa makini kumuangalia mdogo wake na kumbembeleza  aliapo. Mtoto huyu atakuwa na tuuma kubwa mdogo wake anapoumwa na atakubali mzazi wake atumie muda wote kumuuguza mdogo wake ili apone.

2)  Mtoto mchanga anapofika tu, mshirikishe mtoto kwa kadri iwezekanavyo. Anaweza kufanya vijikazi vidogo vidogo kulingana na umri wake kama vile kuleta nepi, taulo na kadhalika. Hisia za ukaka au udada humkweza mtoto na kuona kuwa kumbe hakupoteza nafasi yake bali kapanda cheo. Atajiona kuwa yeye sasa sio wa kushindana na mdogo wake bali yeye ni wa kufanya majukumu makubwa zaidi kulingana na nafasi yake ya juu.

3)  Ongea na mtoto muda wote kuhusu mdogo wake. Mueleze jinsi mdogo wake anavyolia usiku, anavyocheza kitandani. Mwambie am-busu (amshumu)      kidogo, amchekee.

                                             Kufananisha watoto

Wanadamu wote wana vipawa na haiba tofauti. Zipo pia tofauti za tabia. Wazazi wengi hufanya makosa ya kulinganisha watoto. Ingawaje nia ni kumfanya mmoja aige tabia nzuri ya mwenziwe lakini matokeo ya hili, mara nyingi, huwa ni mripuko wa chuki na husuda.

Kufananisha watoto hupunguza hadhi kwa wale ambao mara zote hujikuta wakizidiwa na wenzao. Wakati mwingine watoto hupachikwa majina, “kivivu”, “Goigoi” na kadhalika.

Majina haya yanaporudiwa-rudiwa, hatimaye hukubalika kiasi kwamba “goigoi” huamini kuwa yeye ni goigoi kweli na katu hawezi kuishinda tabia hiyo. Pale wazazi wanapowalinganisha watoto wao, kweli ni muhimu kutaja sifa nzuri za mmoja wao, lakini ni kosa kumsifu mmoja na kumponda mwingine.

                          Mzazi aepuke kuusifu ujinga mbele ya watoto

      Wakati mwingine baadhi ya watoto wanaweza kuwa mahodari katika mambo yasiyofaa. Kwa mfano mtoto hutokea kucheza mziki “vizuri.” Si busara kwa mzazi kusema, “mwanangu unacheza mziki vizuri”, “mtoto kwa kupigana huyu, tena ana ubavu kweli!”

    Huku ni kuusifu ujinga jambo ambalo linaweza kumuharibu yule anayefanya hivyo na kuwakatisha tamaa wale wasiojihusisha na tabia hizo. Wataona mbona mwenzetu kasifiwa na baba au mama. Ni rahisi wao kushawishika kuiga jambo hilo na kuitupa tabia yao njema.

 Kwa hiyo mzazi aepuke kusifu mambo ya kijinga na badala yake asifu mambo mema ili watoto wayapende na kuyatenda kama vile “mwanangu huyu hodari kwa kuswali!” Au “mwanangu huyu ni hodari kwa kufunga!”

Au mwanangu huyu ni hodari kwa masomo darasani! Au “mwanangu huyu ni hodari kwa kazi”, “mwanangu huyu ni hodari kusoma Qur’an”. Haya ndiyo mambo ya kusifu mbele ya watoto.

                         Kuepuka kumkejeli mtoto mbele ya wenziwe

Wazazi, mara nyingi, hucharuka na kumkaripia mtoto mbele ya wenziwe. Mtoto kama alivyo mtu-mzima, asingependa kudhalilishwa mbele ya wenziwe. Maneno makali yanayosemwa na mzazi hata kama yanastahili kusemwa, yanaweza kutumiwa na wenziwe kumkejeli mwenzao.

Ingawaje wakati mwingine, ni jambo la kimaumbile mzazi kupandwa na hasira dhidi ya mtoto aliyekaa pamoja na wenziwe lakini hatua kali za kumkanya zichukuliwe faraghani.

                                 Kuepuka mapenzi ya jinsia                              

Baadhi ya wazazi huwapenda zaidi watoto wao wa kiume kuliko wale wa kike. Hii ni tabia isiyokubalika kabisa katika Uislamu. Kuwapendelea wavulana na kuwahudumia tofauti na dada zao si sahihi hata kidogo.

Kuna baadhi ya wazazi ambao huwapa wasaa mkubwa zaidi watoto wa kiume na kuwanyima nafasi wale wa kike. Hili ni kosa japo uhuru wa mtoto wa kike unapaswa kuchungwa kwa faida yake mwenyewe.

Kwa ujumla, kwa jamii zetu za leo zilizokufa kimaadili, si sahihi kuwapa uhuru mkubwa sana watoto wa jinsia zote mbili. Nukta muhimu ni kwamba wazazi wawahudumie sawa watoto wao wa kike na wa kiume.

Maneno mazuri kuhusu malezi ni haya aliyoyasema Mtume (Salallahu alaihi wasalam)     “Watendeeni sawa wanenu mnapowapa zawadi”

Familia ni taasisi yenye mchango muhimu mno  katika ujenzi wa jamii bora ya wanadamu. Taasisi hii ikishindwa kutimiza wajibu wake, jamii huwa jaa la maasi, kila mwenye uchafu wake huutupia humo.