Ndoa Na Sababu Za Kuchokana - 1
Shams Elmi (Abu 'Ilmi)
Takriban katika maisha ya wanandoa walio wengi kama sio wote, ndoa zao hupitia katika vipindi tofauti. Kama ulivyo umri wa Binadamu, ndoa hupitia katika kipindi cha utoto, ujana na uzee, na kila kipindi kina mambo yake na taratibu zake ambazo kama wanandoa watashindwa kuzifuata basi huenda ndoa hiyo ikakumbwa na mtihani mkubwa, nao ni mtihani wa kuchokana.
Utoto wa Ndoa:
Wengine hukiita kipindi hiki (Honey Moon) mwezi wa asali, kipindi cha raha, utulivu, mapenzi, maelewano baina ya wanandoa. Si lazima kiwe mwezi mmoja kama watu wengi wanavyoamini, bali kinaweza kikawa chini ya mwezi mmoja au zaidi ya mwezi mmoja.
Ujana wa Ndoa:
Hiki ni kipindi kinachofuatia baada tu ya utoto wa ndoa, ni kipindi ambacho kila mmoja miongoni mwa wanandoa anakuwa tayari ameshamtambua mwenzake katika shaksia yake (personality) kwa maana ya jinsi anavyoangalia mambo, jinsi anavyofikiri, mitazamo yake, mielekeo yake na matarajio yake.
Uzee wa Ndoa:
Kipindi hiki ni kipindi ambacho wanandoa wanakuwa tayari wameishaingia katika majukumu ya kulea kwa kupata matunda ya ndoa yao ambayo ni mtoto au watoto.
Kuchokana kwa wanandoa ni tatizo ambalo linatokea kwa familia nyingi, na kusababisha migogoro mingi na hata kufikia familia kuvunjika au kuishi kwa ajili tu ya kulea watoto na si vinginevyo.
Utakuta katika baadhi ya familia, Baba na Mama wanaishi katika nyumba moja, ukiwaona utadhani ni mume na mke wanaopendana, kumbe wanaishi kwa ajili tu ya kuwalea watoto wao na kuogopea maneno ya watu, hali hii ni hali ya talaka ya kimapenzi (emotional Divorce) na ni hali mbaya ambayo mara nyingi humpa msukumo mwanamume wa kuoa mke wa pili katika harakati za kutafuta utulivu na sehemu ya kukimbilia
Tatizo hili la kuchokana kwa wanandoa linasababishwa na wanandoa wote wawili kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki za mume na mke kama zilivyobainishwa na Uislamu.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika Qur-aan:
)ومن آياته أن خلق لكم من أنفسكم أزواجا لتسكنوا إليها وجعل بينكم مودة ورحمة إن في ذلك لآيات لقوم يتفكرون) الروم 21
(Na katika ishara zake ni kuwa Amekuumbieni wake zenu katika jinsi yenu ili mpate utulivu kwao, Naye Amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Bila shaka katika haya zimo ishara kwa watu wanaofikiri) 30:21
Ayah hii ambayo ni miongoni mwa ayah zinazosomwa mara nyingi katika ndoa zetu inatuwekea bayana nguzo zinazosimamisha nyumba ya ndoa, nazo ni nguzo kuu tatu:
1. Utulivu (( السكينة
2. Mapenzi (المودة)
3. Huruma ((الرحمة
Utulivu huletwa na mwanamke, na ndio maana aya ikatafsirika “ili mpate utulivu kwao”. Utulivu huzaa mapenzi na huruma baina ya wanandoa, kwa maana nyingine, mwammke ana nafasi kubwa ya kujenga au kubomoa ndoa, hii haina maana kuwa mwanamume hana nafasi ya uharibifu, bali nafasi ya mwanzo inachukuliwa na mwanamke bila ya upinzani.
Kwa hekima za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), amewaumba wanawake tofauti kabisa na wanaume kimaumbile (Physical), kihisia (emotional), na kinafsi (Psychological), hii yote ni kwa ajili ya wadhifa na majukumu yao katika jamii. Allaah Anasema:
(وليس الذكر كالأنثى..) الأنعام 36
(….Na Mwanamume si sawa na Mwanamke…) 3:36
Hivyo basi, sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa kuleta utulivu katika ndoa yao, na hapa nitajaribu kujadili baadhi ya visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana visababishi ambavyo huwa vinadharaulika na kuonekana vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.
a) Kuzoeana: kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususan kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla. Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano: siku za utoto wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini. Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Anasema :
(خير النساء من إذا نظرت إليها سرتك، وإذا أمرتها أطاعتك...) رواه النسائي
M’bora wa wanawake (wake zenu) ni yule ambae ukimwangalia anakufurahisha, na ukimuamrisha anakutii …) An-Nasaaiy
b) Mazungumzo: Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake. Kwa mfano: Mwanamke ambaye kila anapoongea na mume wake huanza mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu anayependa kusikia matatizo tu wakati wote. Mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Anasema:
عن أنس رضي اللــه عنه عن النبي صلى اللـه عليه وآله وسلم قال: (يسروا ولا تعسروا وبشروا ولا تنفروا ) البخاري
(Fanyeni wepesi msiwatie (watu) uzito, na toeni habari za furaha, wala msiwakimbize watu) Al-Bukhaariy
c) Kusomana Tabia: ni udhaifu mkubwa kwa wanandoa ambao wana mwaka mmoja katika ndoa yao wakawa bado hawajasomana tabia, au wakawa wameishasomana tabia, lakini kila mmoja akawa anataka tabia zake ndio ziwe dira. Kwa mwanamke mwenye busara na mwenye kuithamini ndoa yake, husoma tabia za mumewe na kuangalia jinsi gani anavyoweza kuzioanisha na zile zake ili kuepusha migongano, aidha hutafuta fursa muafaka ya kumkinaisha mumewe juu ya fikra fulani au tabia fulani ambayo yeye haridhiki nayo. Ni muhimu kwa mwanaume vilevile kuzisoma tabia za mke wake, vitu gani vinamuudhi, na vitu gani vinamfurahisha. Mtume alikuwa anajua tabia za mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) wakati gani anakuwa amekasirika na wakati gani amefurahi, kama ilivyokuja katika athar Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia mama wa waumini ‘Aaishah:
)إني لأعرف غضبك من رضاك ! قالت: وكيف تعرفه ؟ قال: إذا رضيت قلت: لا، وإله محمد،وإذا غضبت قلت:
لا وإله إبراهيم(
(Hakika mimi najua wakati ukikasirika na ukifurahi, (‘Aaishah) akasema; unajuaje? Ukiwa na furaha husema, Laa naapa kwa jina la mola wa Muhammad, na ukiwa umekasirika husema, Laa naapa kwa jina la mola wa Ibraahiym)
Itaendelea inshaAllaah…
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
