Skip navigation.
Home kabah

Faida Ya Taqwa

 

 

 

((...  وَمَن يَتَّقِ اللَّهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا ))     

   ((  وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لاَ يَحْتَسِبُ ..))

((Na anayemcha Allaah Humtengezea njia ya kutokea))

 ((Na Humruzuku kwa jiha asiyotazamia))

[At-Twalaaq: 2-3]

Haya ni maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyotuletea katika uongofu kamili kwenye kitabu ambacho hakitafikia batili  mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye Hikma  Mwenye Kuhimidiwa.  

Maneno yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)ni kuli ya  haki (ni kweli) kama Anavyosema

((وَمَنْ أَصْدَقُ مِنَ اللّهِ حَدِيثًا))

((Na ni nani msema kweli kuliko Allaah?)) [An-Nisaa: 87] 

 

Aayah hiyo ya juu tukufu imetanguliza sharti mwanzo kwa kupatikana yale Aliyoyaahidi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).  Sharti hiyo ni kuwa na taqwa (Kumcha Allaah) ili jazaa yake ni Kujaaliwa njia (upenyo, kivuko) na Kuruzukiwa pale asipotegemea. Basi itakapopatikana sharti hiyo, yatapatikana hayo yaliyoahidiwa.

Tujiulize swali, vipi kufikia taqwa? Au Nini maana ya taqwa?  Jibu ni katika sentensi fupi iliyokamilisha kila kheri. Nayo ni "Kutekeleza yaliyoamrishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume  na kujiepusha makatazo Yao na kubakia katika mipaka".  Hapo ndipo itakapopatikana taqwa.  Na kuwa na taqwa ndio sababu ya furaha na kufuzu duniani na akhera,  na pia ni sababu ya kuondoshewa shida na dhiki zote.

Taqwa ni wasiya wa watu wa mwanzo na wa mwisho na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  aliwausia Maswahaba wake wapenzi :

  عن أبي ذَرٍّ جُنْدُب بِن جُنَادَة، وأبي عبد الرحمن مُعَاذ بِن جَبَلٍ رضي الله عنهما، عن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((اتق الله حيثما كنت، وأَتْبِعِ السَّيئةَ الحسنةَ تَمْحُها، وخالقِ الناسَ بخُلُقٍ حسنٍ)).  رَوَاهُ التِّرْمِذِيُّ   وَقَالَ: حَدِيثٌ حَسَنٌ، وَفِي بَعْضِ النُّسَخِ: حَسَنٌ صَحِيحٌ.

Kutoka kwa Abu Dharr Jundub Ibn Junaada na Abu Abdur Rahmaan Mu'adh Ibn Jabal (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambao wamemnukuu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema:

((Mche Allaah popote pale ulipo, na fuatisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri kitafuta (kitendo kibaya), na ishi na watu kwa uzuri)) [Imesimuliwa na At-Tirmidhiy na kasema kuwa ni Hadiyth Hasan na katika maandiko mengine imesemwa kuwa ni Hasan Swahiyh]

Na Taqwa haihitajii kuhakikishwa kuwa mahali fulani au wakati fulani, bali taqwa ya hakika  ni pale mtu anapokua yuko peke yake, akajiepusha na yaliyo haraam japokuwa hakuna mtu anayemuona. Na ndipo aliposema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kuwa 'Taqwa iko hapa' akiashiria kwenye kifua chake palipo na moyo na kusema mara tatu.