Tahadhari Na Madhara Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo - 4

 

Tunaendelea kutaja madhara ya maudhi hii:

Nne: Ukosefu wa Mapenzi Ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

Tutambue kuwa kuhakikisha kwamba Hadiyth Sahihi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinabakishwa na Hadiyth dhaifu zinafutwa ni ishara ya mapenzi makubwa kwa anayempenda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa dhati kwani hakuna mtu apendaye kumzulia mpenzi wake maneno asiyoyasema. Na kinyume chake ni kudhihirisha ukosefu wa mapenzi ya kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Na kumpenda Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni sawa sawa na kumpenda Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  ((قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللّهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللّهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ)) 

((Sema: Ikiwa nyinyi mnampenda Allaah basi nifuateni mimi, Allaah Atakupendeni na Atakufutieni madhambi yenu. Na Allaah ni Mwenye kufuta madhambi na Mwenye kurehemu)) [Al-'Imraan: 31] 

 

Nani asiyempenda Mola wake Mtukufu? Na nani asiyetaka kupendwa Naye? Na nani katika sisi mwenye kumpenda khaswa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Ni yule mwenye kumuenezea tu uzushi bila ya kuwa na hadhari au yule mwenye kujali na khofu ya kumsambazia uzushi?  

Mwenye kutaka kujisalamisha na madhara haya, basi tekeleza yafuatayo pindi unapopata ujumbe wowote wa dini wenye tata:

 

Kwanza:

Ikiwa ni Hadiyth isemwayo kuwa ni ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), hakikisha kwanza usahihi wake. Ikiwa ni kisa pia hali kadhalika tafuta usahihi wake. Ikiwa huwezi kufanya utafiti na kutambua usahihi wake, basi tafadhali tuma kupitia maswali@alhidaaya.com kuuliza ili ifanyiwe utafiti na jibu litatolewa kwa dalili ya kutanabahisha udhaifu wake na katika hali nyingine kubainisha yaliyo sahihi badala yake.   

Pili:

Itakapokudhihirikia kwamba ni Swahiyh, unaweza kuwatumia wenzio ili wapate kunufaika, nawe ujichumie thawabu za kufikisha ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

Ama ikiwa ni dhaifu basi ni waajib kumrudishia aliyekutumia na kumtambulisha udhaifu wake, kumpa nasaha kwa kumtumia makala hizi. Naye ni waajib wake kumjulisha aliyemtumia, iendelee hivyo hadi imfikie aliyeanza kutuma uzushi.

Nasaha hizi tumezitoa kwa dhati kwa kuwakhofia ndugu zetu wasitumbukie katika makosa na kupata madhara haya tuliyotaja yote, na pia kufanya Jihaad kuibakisha dini yetu iwe safikama tulivyoletewa bila ya kuwa na ufisadi ndani yake. 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie nuru ya elimu Yake na Atuonyeshe yaliyo ya haki tuyafuate na yaliyo ya batili tuepukane nayo.

TANBIHI:

 

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na utajibiwa haraka InshaAllaah.

Share