Tahadhari Na Madhara Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo-3

 

Tunaendelea kutaja madhara ya maudhui hii:

Pili: Kupoteza Wakati Kwa Amali Zisizokubaliwa:

Hadiyth hizo zitazidi kusambaa na wengi wasioweza kupambanua baina ya Hadiyth Sahihi na Hadiyth Dhaifu watakuwa wanaona ni sawa kwao na watakuwa wanapoteza wakati wao kufanya ‘Ibaadah zinazotajwa fadhila zake katika Hadiyth hizo dhaifu na wasipate thawabu yoyote, wakati wangeliweza kuutumia wakati wao na nguvu zao kwa ‘Ibaadah zilizokuwa na uhakika zilizothibiti kwa ushahidi sahihi na wakapata ujira. Hivi itawathibitikia watakapokutana na Mola Mtukufu katika kuhesabiwa amali zao walizotenda:

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

((وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا))

((Na Tutayaendea yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, Tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika)) [Al-Furqaan:23]

Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

(( من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa na mafunzo ya dini yetu basi kitarudishwa.)) [Al-Bukhaariy] 

Jambo Muhumu Kuzingatiwa:

‘Ibaadah zetu zote ikiwa ni kwa vitendo au kauli LAZIMA zitimize sharti mbili muhimu kabisa nazo ni:

  1. Ikhlaasw – Iwe kwa kutaka Ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   na sio yenye Riyaa au sio yenye kutendeka kwa ajili ya maslahi ya kidunia.

  2. Iwe ni tawqifiy, kwa maana: kufanyika kwa mujibu wa mafunzo kutoka katika Qur-aan na Sunnah)

Tatu: Kupoteza Mafunzo Swahiyh Na Kuenezea mafunzo ya Uzushi: (Bid’ah)

Dhara jingine la  jambo hili ni kwamba, kila zinapoendelea kusambaa Hadiyth hizo dhaifu, ndipo Hadiyth Swahiyh nazo zinaachwa kutumika na kujulikana, na mwishowe ni kuenea mafunzo yasiyo sahihi ya uzushi (Bid'ah) na kupotea yale yaliyo sahihi.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    

(( وأياكم ومحدثات الأمور فإن كل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة))

((Jihadharini na mambo ya uzushi kwani kila uzushi ni Bid'ah na kila Bid'ah ni upotofu)) 

 

TANBIHI:

 

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na utajibiwa haraka InshaAllaah.

 

 

Itaendelea InshaAllaah…

Share