Tahadhari Na Madhara Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo -2

 

Dalili zifuatazo zinaonyesha madhara ya kutoa mafunzo ya uongo na upotofu:

Hadiyth ya kwanza:

عن أَبِي هُرَيْرَةَ, أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  (( مَنْ دَعَا إِلَى هُدًى, كَانَ لَهُ مِنْ الْأَجْرِ مِثْلُ أُجُورِ مَنْ تَبِعَهُ, لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أُجُورِهِمْ شَيْئًا, وَمَنْ دَعَا إِلَى ضَلَالَةٍ, كَانَ عَلَيْهِ مِنْ الْإِثْمِ مِثْلُ آثَامِ مَنْ تَبِعَهُ, لَا يَنْقُصُ ذَلِكَ مِنْ أوزارهم شَيْئًا))    رواه مسلم

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

Hadiyth ya pili:

عن أبي مسعود الأنصاري رضي الله عنه يقول النبي صلى الله عليه وسلم : (( من دل على خير فله مثل أجر فاعله)) خرجهما مسلم في صحيحه .

Kutoka kwa Abu Mas’uud Al-Answaariy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kuongoza katika kheri atapata thawabu kama za mwenye kufanya)) [Muslim katika Sahihi yake]

Hadiyth ya tatu:

((من سن في الإسلام سنة حسنة كان له أجرها وأجر من عمل بها من بعده لا ينقص ذلك من أجورهم شيئاً ومن سن في الإسلام سنة سيئة كان عليه وزرها ووزر من عمل بها من بعده لا ينقص من أوزارهم شيئاً)) خرجه مسلم في صحيحه

((Atakayefanya kitendo chema  katika Uislam atapata ujira wake na ujira wa yule atakayekitenda baada yake  bila ya kupungukiwa  thawabu zao. Na atakayetenda kitendo kibaya katika Uislam atabeba (mzigo wa) dhambi zake na dhambi za yule atakayetenda wala hapungukiwi kitu katika (mzigo wa) dhambi hizo)) [Muslim]

Kusambaza Hadiyth bila ya kuhakisha kama ni Sahihi kutasababisha hatari na madhara yafuatayo:

Kwanza:  Hatari Ya Kujiandalia Makazi Ya Moto:

Ataangukia katika miongoni mwa wenye kumuongopea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo katika Hadiyth:

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

Kama tunavyoona kwamba hatari yake ni kujitayarishia makazi motoni (tunamuomba Allaah Atuepushe na hilo), juu yake tutakuwa tumewaingiza na wenzetu ambao nao wataendelea kuzisambaza hizo Hadiyth na itaendelea hivyo hivyo kuwaingiza ndugu zetu wengi katika hatari kama hii. Na hatari zaidi ni kwamba kila watu wanapozidi kuzisambaza, basi dhambi huzidi kuongezeka kwa waliotuma wote nyuma yao na haswa zaidi kwa aliyeanzisha, (maana kwamba, wingi wa dhambi unazidi kuongezeka na yule mtu wa mwanzo kabisa aliyeanza kueneza ndiye mwenye kubeba dhambi za watu wote).

TANBIHI:

 

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na utajibiwa haraka InshaAllaah.

 

 

Itaendelea InshaAllaah..../

Share