Tahadhari Na Madhara Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo - 1

 

Kutokana na maendelo ya wepesi wa mawasiliano, fitna za kusambazwa uzushi, visa vya uongo, na mengi mno yasiyopasa katika Dini yetu zimezidi mno. Wengi hutuma tu bila ya kuhakikisha kwanza usahihi wake. Na wengi hughilibika kwa kudhani ni jambo lenye manufaa madamu tu ametajwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), au ni jambo la kupendeza au la kujichumia thawabu, kumbe ni kinyume chake na ni mambo ya kupotosha watu na kuchuma dhambi. Hivyo basi ni muhimu kukumbushana ufisadi huu wa Dini kama tunavyoamrishwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عن أَبي سعيدٍ الخُدْريِّ رضي اللَّه عنه قال : سمِعْتُ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ : ((مَنْ رَأَى مِنْكُم مُنْكراً فَلْيغيِّرْهُ بِيَدهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطعْ فبِلِسَانِهِ ، فَإِنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبقَلبهِ وَذَلَكَ أَضْعَفُ الإِيمانِ)) رواه مسلم .

Kutoka kwa Abu Sa'iyd Al-Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu basi akiondoe (abadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) [Imesimuliwa na Muslim]

Ni muhimu mtu anapopata uzushi wowote wa dini baada ya kuhakikisha,   ampe nasaha mwenziwe aliyemtumia bila ya kusita, kuogopa au kujali lawama, kwani kupeana nasaha ni amri kwetu sote kwa ujumla, na sio kazi ya walinganiaji pekee.

  عَنْ تَمِيمٍ الدَّارِيِّ أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ :((الدِّينُ النَّصِيحَةُ قُلْنَا لِمَنْ قَالَ لِلَّهِ وَلِكِتَابِهِ وَلِرَسُولِهِ وَلِأَئِمَّةِ الْمُسْلِمِينَ وَعَامَّتِهِمْ)) مسلم .

Kutoka kwa Tamiym Ad-Daariyyi kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: ((Dini ni Nasiha, tukasema kwa nani? Akasema: kwa Allaah na kitabu Chake na Mtume Wake, na kwa Viongozi wa Kiislam na watu wa kawaida)) [Muslim]

Waislamu tunatakiwa daima tuwe katika kupeana nasiha na kuepushana na kila aina ya shari. Na kufanya hivi ndio kudhihirisha mapenzi baina yetu. Na kunasihiana katika jambo kama hili la kuepuka kusambaza Hadiyth dhaifu bila shaka ni muhimu zaidi kwani kuna hatari kubwa ndani yake kama tuonavyo maonyo yaliyomo katika Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).      

Nasaha hizi zinafuatia makala, Hadiyth, au ujumbe mbalimbali unaoenezwa kwenye mtandao au simu za mkono (mobile phones) na kusukumwa na kupeperushwa kwa mamia ya Waislam, kama hizi:

'HADIYTH YA ADHABU KUMI NA TANO ZA MWENYE KUACHA SWALAH'

'SIKU KUMI BORA MWEZI WA MFUNGO TATU'

'BARUA KUTOKA KWA SHEIKH AHMAD WA MADINA'

‘ACHA KUFANYA KILA KITU UNAPOSIKIA ADHAAN’

‘EWE ‘ALIY USILALE HADI UMEFANYA MAMBO MATANO’

na mfano wa hizo nyingi zikija kwa lugha mbalimbali.

Jambo muhimu kabisa ni kuwa Muislamu inapomfikia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi imeshakuwa WAAJIB kwake ahakikishe usahihi wa Hadiyth hiyo. Kama ni Sahihi anaweza kuwatumia wenzake ili apate fadhila za kupata thawabu za wale watakaofuata mafundisho hayo. Na kama ni dhaifu basi haimpasi kusambaza ili asije kubeba dhambi na dhambi za watakaotenda mafunzo hayo ya upotofu.

 

TANBIHI:

Ukipokea jambo lolote lenye mashaka na utata kuhusiana na Dini, tafadhali tuma maswali@alhidaaya.com lifanyiwe utafiti kabla ya kuwatumia wengine na kuenezwa, na utajibiwa haraka In shaa Allaah.

 

Itaendelea In shaa Allaah...

 

Share