Subira Katika Malezi
Ummu Hanaan
Subira ni moja ya jambo muhimu lilosisitizwa na kutiliwa mkazo katika dini yetu ya Kiislam.
Subira ndiyo inayomfanya mtu awe mbora kati ya watu wema ambao wameahidiwa malipo yaliyo bora na Mola wetu, kuna aya nyingi zinatutaka tuwe na subira.
Mwanaadamu ukiwa na subira ndio unapoyaona maisha yanakuendea vizuri na moyo wako hutulia hasa subira hiyo inapoelekea kwa Mola wako na ukawa kila jambo unalisubiria kwa ajili ya kupata malipo yalio bora kutoka kwa Mola wetu Subhaanahu wa Ta’ala.
Na sivyo kabisa tunavyoichukulia subira kwa kuridhishana na kusubiriana sisi kwa sisi katika kutendeana maovu na kumuasi Mola wetu, nasema hivi kwa sababu wengi wetu tunasubiriana katika umuhali na sio kwa ajili ya Mola wetu.
Mfano wetu sie kinamama na malezi ya watoto wetu tunakosa subra ya kuwalea kwa kuzingatia maagizo ya dini yetu ya Kiislam,kwa ajili ya kuepuka usumbufu wa kugandwa na watoto wetu. Utakuta tangu tukiamka tunawafungulia TV wanaangalia ati katuni (cartoon) na sie tunapata muda wa kufanya kazi zetu, tunajisahau kwamba tunawazowesha kusikiliza muziki na wanakuwa hata fahamu zao zimetekwa na hayo makatuni. Nasema hivyo kwani hamna la maana ndani ya programu hizo ila ni wingi wa upotovu na tabia chafu tu.
Hapo uchache wa subira wa kukimbia dhiki za kugandwa na watoto ndio inayotupelekea kuwapotoa watoto wetu kwa kuwa hatujaujua ujira wa mama atakapochukua uzito ule wa kulea mtoto kwa ajili kupata malipo kutoka kwa Mola wake, wengi wetu utakuta tunafanya khairati nyingi bila ya kuwa tunaelewa kuwa kuna malipo kutoka kwa Mola wetu.
Suala hili la Malezi ya watoto linataka subira ya hali ya juu na tuombe kwa Allaah Subhaanahu wa Ta’ala kila siku kwani tukumbuke kesho mbele ya Mola wetu tutakuja kuulizwa vipi tuliwalea watoto hao.
Napenda kuiusia Nafsi yangu pamoja na kinamama wenzangu tujue tumepewa watoto sio kwamba tunapendwa sana ila ni mtihani kwetu, tupunguze huruma katika malezi ya watoto wetu na tumuombe Mungu Atusaidie katika kuwaongoa watoto wetu. Tujue kunahitajika subra ya hali juu katika malezi ya vizazi vyetu, tufanye kwa nia ya kutaraji malipo bora tuliyoahidiwa na Mola wetu.
Na Allaah Ndiye Anayejua zaidi.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


