036 Yanayotengua Kupukusa (Kupaka/Kupangusa) Juu Ya Khufu Mbili
YANAYOTENGUA KUPUKUSA (KUPAKA/KUPANGUSA) JUU YA KHUFU MBILI
Imetangulia katika Hadiyth iliyoelezewa na Swafwan bin ‘Assal kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi waalihi wa sallam), alikuwa akituamuru tunapokuwa safarini, tusizivue khufu zetu siku tatu na masiku yake ila kwa janaba, lakini si kwa kwenda haja kubwa, au ndogo, au kulala.
Kwa Hadiyth hii, imejulikana kuwa haifai kupukusa juu ya khufu mbili linapotokea moja kati ya mambo yafuatayo:
1- Janaba na mengineyo yenye kuwajibisha kuoga
2- Kumalizika muda wa kupukusa.
3- Kuivua khufu na kupata hadathi kabla ya kuivaa.
Endapo ataivua khufu yake - ijapokuwa kabla ya kumalizika muda – kisha akapata hadathi, basi haitojuzu kuivaa na kupukusa, kwani anakuwa hakuivaa wakati huo akiwa na twahara.
Kwa hivyo, kama litatokea lolote kati ya mambo haya matatu, haitojuzu kwake kupukusa juu ya khufu mbili, bali linalopasa kwake anapopata hadathi, ni kutawadha na kuosha miguu yake miwili, kisha anaweza kuzivaa khufu zake na kupukusa juu yake
UZINDUSHI
Kubatilika kupukusa hakumaanishi kuwa wudhuu umetenguka. Mtu ambaye alikuwa anapukusa juu ya khufu zake mbili kisha akazivua bila ya kupata hadathi, Maulamaa wana kauli nne juu ya hukumu yake:
Ya kwanza:
Itampasa atawadhe upya. Haya ni madhehebu ya An-Nakh’iy, Al-Awzaa’iy, Ahmad, Is-haaq[1] na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu yake ya zamani. Wanasema kuwa sababu ya
Ya pili:
Itampasa aoshe miguu yake basi. Haya ni madhehebu ya Ath-Thawriy, Abuu Haniyfah na wenzake na Abu Thawr. Pia ni kauli mpya ya Ash-Shaafi’iy.[2]
Ya tatu:
Ni lazima aoshe miguu yake miwili baada tu ya kuzivua khufu. Ikiwa atachelewa, basi atatawadha upya. Haya ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth.[3]
Ya nne:
Hawajibiki kutawadha wala kuosha miguu. Hii ni riwaya iliyopokelewa toka kwa An-Nakh’iy. Haya haya yamesemwa na Al-Hasan Al-Baswriy, ‘Atwaa na Ibn Hazm. Aidha, yamekhitariwa na An-Nawawiy, Ibn Al-Mundhir na Ibn Taymiyah.[4] Haya ndiyo madhehebu yaliyo sahihi. Hii ni kwa vile, mtu huyu akiwa na khufu zake, kwa mujibu wa Hadiyth iliyothibiti, anakuwa na utwahara kamili. Na
Kisha imefanyiwa kipimo kwa mtu aliyepaka maji kichwani kisha akazinyoa nywele. Bila shaka wao hawasemi kuwa itapasa kupaka maji tena kichwani au kutawadha tena!! Na hii ndiyo sawa hasa katika suala hili. Anapozivua khufu zake bila ya kupata hadathi, basi anaweza kuswali Swalah zozote azitakazo mpaka pale wudhuu wake utakapotenguka.
Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
[1] “Ikhtilaaf Al-‘Ulamaa” (uk.31), “Masaail Ahmad” ya Ibn Haani’i (19/1) na “Al-Majmu’u” (1/557).
[2] “Ikhtilaaf Al-‘Ulamaa” (uk31) na “Al-Awswat” (1/458).
[3] “Al-Mudawwanah” (1/41).
[4] “Al-Muhalla” (1/105), “Al-Awswat” (1/460), “Al-Majmu’u” (1/558) na “Al-Ikhtiyaaraat” (uk.15).
[5] Isnad yake ni sahihi: Imetolewa na Al-Bayhaqiy (1/288) na At-Twahaawiy (1/58). Tazama “Tamaam Al-Minnah” (uk115).
- Login or register to post comments
- Email this page


