06 Wasiya Kumi Wa Allaah Wasiya wa Kwanza Kutokumshirikisha Allaah – 3
Shirki ziko aina mbili; shirki kubwa na ndogo.
Shirki Kubwa
Shirki Kubwa humtoa mtu katika Uislamu na kumuingiza mtu motoni milele ikiwa hakutubu kabla ya kufa kwake,
((إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللّهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللّهُ عَلَيهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَار))
((Kwani anayemshirikisha Allaah hakika Allaah Atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru)) [Al-Maaidah: 72]
Shirki kubwa ni
1- Kumshirkisha katika Ar-Rubuubiyyah (Uola Wake)
Kuamini kwamba kuna mwingine pasi na Allaah katika uumbaji, na hali Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ndiye Muumba wa kila kitu, Muumba wa mbingu na ardhi, na Muumba wa viumbe vyote na Ndiye Mfalme Anayemiliki vyote hivyo mbinguni na ardhini hapa duniani na kesho Akhera. Shirki hii ni
((فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَى))
((Akasema: mimi ndiye Mola wenu Mlezi mkuu kabisa)) [An-Nazi’aat: 24]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akamgharikisha Fir’awn, hivyo basi vipi ikiwa yeye ni mungu agharikishwe na Mwengine?
2- Kumshirikisha katika Uluuhiyya (Uungu Wake)
Kuelekeza ‘Ibaadah kwa mwingine pasi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Anaweza kuwa mtu anaamini Allaah kuwa Ndiye Muumba wake na Muumba wa mbingu na ardhi na viumbe vyote, lakini anatumia vinavyomkaribisha Kwake katika ‘Ibaadah zake
((قُلْ إِنَّ صَلاَتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ))
((لاَ شَرِيكَ لَهُ وَبِذَلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَاْ أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ))
((Sema: Hakika Swalah yangu, na ‘Ibaadah zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah Mola Mlezi wa viumbe vyote))
((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An’aam: 162-163]
3- Shirk ya Swifaat na AsmaauLlaahil-Husna (Sifa na Majina Ya Allaah)
Kujinasibisha mtu na sifa au majina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), na kuamini kwamba anao uwezo
((وَلِلّهِ الأَسْمَاء الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُواْ الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَآئِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُواْ يَعْمَلُونَ))
((Na Allaah Ana Majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina Yake. Hao watakujalipwa waliyokuwa wakiyatenda)) [Al-A’raaf: 180]
Shirki kama hii wengi hutumbukia kwayo, khaswa katika jamii yetu. Bila ya shaka hawatanabahi madhara yake hayo kwamba huenda yakamtoa mtu nje ya Dini yake. Mfano wachawi, na wale wanaokwenda kwa watabiri wa mambo ya ghayb, (elimu iliyofichika), wanaokwenda kwa waganga kuwaamini kwamba wao watawaponyesha n.k.. Wanaotenda na wanaotendewa wote watakuwa wamo katika fungu hili la shirki kubwa. Kufru na shirki kubwa hii ni sawa na kukanusha mafunzo yote aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((من أتى كاهناً فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل على محمد صلى الله عليه وسلم)) رواه أبوداود
((Atakayemwendea mchawi na kuamini aliyoambiwa, basi amekufuru yale aliyoteremshiwa Muhammad [Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam])) [Abu Daawuud]
Mwenye kumkufuru Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila shaka ni mwenye kumkufuru Allaah, na hivyo anatoka nje ya Uislamu.
Vile vile shirki hii inahusiana na wale wanaoamini nyota (horoscope) mawe ya rangi fulani kuwa yanahifadhi au kinga, wanaotumia hirizi zinazoandikwa na waganga watakayo n.k.
Aina zote za shirki hizo amezijumuuisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipouulizwa kuhusu shirki akasema:
(( أن تجعل لله ندا وهو خلقك)) متفق عليه
((Kumfanyia Allaah mshirika na hali Yeye Ndiye Aliyekuumba)) [Al-Bukhaari na Muslim]
Hivyo ni waajib wa Muislamu kujisalimisha na shirki kubwa na abakie katika tawhiyd bila ya kumshirikisha na yeyote au chochote bali kumkabili Yeye kwa kila zuri na baya, ili ajisalimishe na ghadhabu za Mola Mtukufu na moto mkali Aliouandaa kuwaingiza wale wanaomshirikisha wadumu humo milele.
Itaendelea InshaAllaah…/
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha



ASSALAM ALAIKUM
ASSALAM ALAIKUM WARAHMATULLAHI WABARAKATUH
Mashallah Kazi Nzuri Munazojitahidi nayo Allah Azza Wa Jalla Awazidishie Kulla Khayr fi Dunia Wal Akhera. AMIN.
Mimi wenu Naaman Idris kutoka Kenya lakini sasa niko chouni WALES UNIVERSITY OF GLAMORGAN na kwa furaha website hino imetuchukua kwa dhoruba kali mno kwani twakumbuka Radio Iqra (NAIROBI). Inshallah kama twaweza kuongezewa mawaidha za Muhammad Yuunus kwa mbili zilizopo nimoja imerudiwa!
Maasalam na Allah(SWT) Awaongoze Katika Njia Iliyonyooka na kutukutanisha Jannah tul Firdaus AMIN
JAZAKALLAHU KHAYRAN