07 Wasiya Kumi Wa Allaah Wasiya wa Kwanza Kutokumshirikisha Allaah – 3
Shirki Ndogo
Shirki ndogo haimtoi mtu katika Uislamu bali anahesabika ni mwenye kutenda dhambi kubwa ambayo anapaswa mtu kutubia haraka. Nayo ni mambo yote yaliyokatazwa katika sheria yanayohusiana na aina za shirki kubwa,
قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ حَلَفَ بِغَيْرِ اللَّهِ فَقَدْ كَفَرَ أَوْ أَشْرَكَ)) رواه الترمذي وأبو داود وصححه الألباني في صحيح الترمذي .
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeapa pasi na Allaah, atakuwa amekufuru au ameshiriki [amemshirikisha Allaah])) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud na ameipa daraja ya Swahiyh Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy]
Shirki ndogo nyingine ni riyaa ambayo imefafanuliwa kwa maana ya: ‘‘Kufanya matendo ambayo ni ya kumpendezesha Allaah lakini kwa nia ya kumridhisha asiye Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)”. Au ni kufanya amali njema kwa makusudio ya kuonesha watu, ili aonekane mtu kuwa ni mzuri au mwema kuliko alivyo, ama apate kupendeza machoni mwao au apate kilicho mfukoni mwao au cheo. Riyaa hii ni aina ya shirki na kadhalika ni namna ya unafiki au wizi. Hivyo basi yoyote mazuri yafanywayo kwa kutaka na kutaraji manufaa ya kilimwengu na sio kumridhisha Muumba, basi yanageuka kuwa ni matendo ya kishetani.
Mifano michache ifuatayo ambayo mtu sio kawaida yake kufanya anapokuwa pekee:
- Kurefusha Swalah, unaposwali mbele ya mtu au watu.
- Kuomba du’aa ikiwa katika kurefusha sidja au nje ya Swalah.
- Kusoma kwa sauti ya kupendezesha Qur-aan au adhkhaar mbele za watu uoneshe umahiri wako.
Zote hizo ni riyaa na pia alama za unafiki Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((وَإِذَا قَامُواْ إِلَى الصَّلاَةِ قَامُواْ كُسَالَى يُرَآؤُونَ النَّاسَ وَلاَ يَذْكُرُونَ اللّهَ إِلاَّ قَلِيلاً))
((Na wanapoinuka kuswali huinuka kwa unyong’onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Allaah ila kidogo tu)) [An-Nisaa: 142]
- Kutoa sadaka kwa wingi hasa hadharani.
- Kumfanyia wema mtu ili ujulikane ni mwema.
- Kufunza watu dini ili uwe maarufu.
- Kujitumbukiza katika mauti ili ujulikane kuwa ni shahiyd.
- Amali zozote kwa ujumla ambazo mtu huzipamba kwa watu ili asifike, ilhali sio kawaida yake
Shirki hii ametutahadharisha nayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( إنَّ أَخْوَفَ مَا أَخَافُ عَلَيْكُمْ الشِّرْكُ الْأَصْغَرُ الرِّيَاءُ يَقُولُ اللَّهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إذَا جَزَى النَّاسَ بِأَعْمَالِهِمْ : اذْهَبُوا إلَى الَّذِينَ كُنْتُمْ تُرَاءُونَ فِي الدُّنْيَا اُنْظُرُوا هَلْ تَجِدُونَ عِنْدَهُمْ جَزَاءً )) مَا رَوَاهُ أَحْمَدُ :
((Hakika ninachokiogopea zaidi kwenu ni shirki ndogo, ambayo ni riyaa. Atasema Allaah, siku ya Qiyaamah watakapopewa watu malipo
Mwenye kutaka kujiepusha na riyaa basi atekeleza ‘Ibaadah zake kwa ikhlaasw ili aweze kupata malipo yake kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
((فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا))
((Mwenye kutaraji kukutana na Mola wake Mlezi basi na atende vitendo vyema, wala asimshirikishe yeyote katika ‘Ibaadah ya Mola wake Mlezi)) [Al-Kahf: 110]
Bila ya shaka kutenda amali kwa riyaa haitamfaa Muislamu Akhera, bali ni kupata manufaa machache duniani na madhara makubwa Akhera.
Du’aa ifuatayo ikisomwa kila siku asubuhi na jioni itamsaidia Muislamu kujitoa katika riyaa:
اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ أَنْ أُشْـرِكَ بِكَ وَأَنا أَعْـلَمْ، وَأَسْتَـغْفِرُكَ لِما لا أَعْـلَم
“Allaahumma inniy a’uudhu Bika an ushrika Bika wa ana a’alam, wa Astaghfiruka limaa laa a’alam”
“Ee, Allaah, hakika mimi najilinda Kwako kutokana na kukushirikisha hali ya kuwa najua na ninakutaka msamaha na nisilolijua”
Itaendelea inshaAllaah…/
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


