Umuhimu Wa Zakaah - 6: Zakaah Ya Mali Ya Haraam
Abu ‘Ammaar
Zakaah Ya Mali Ya Haramu
Uislamu haujakataza watu kutafuta rizki zao na hata kujitajirisha endapo tu njia zitakazotumika ni za halali. Na Mtume wetu Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam ametuhadharisha katika suala zima la kutajirika kwa njia zisizo halali kwa kusema:
"إن التجار يُبعثون يوم القيامة فجارًا إلا من اتقى الله وبر وصدق" رواه الترمذي وقال حديث حسن صحيح والحاكم وصححه
“Hakika wafanya biashara watafufuliwa siku ya kiama wengi wao wakiwa waovu isipokuwa yule atakaemcha Allaah na kutenda wema na kutoa sadaka” Attirmidhiy na anasema ni hadith hasan sahihi na Al Haakim ambae ameisahihisha.
Kwa hadithi hii tu inatupa picha kuhusu suala zima la biashara na madhara yake ikiwa biashara hii itasimama katika misingi ya haramu au kuwepo utata katika kusimamishwa kwake.
Na Allaah Subhaanahu Wata’ala Anatukumbusha katika Quraan Al Baqarah/ 267
" يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا أَنْفِقُوا مِنْ طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُمْ مِنَ الْأَرْضِ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنْفِقُونَ وَلَسْتُمْ بِآَخِذِيهِ إِلَّا أَنْ تُغْمِضُوا فِيه...ِ
“Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile Tulivyokutoleeni katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msingevipokea ila ingekuwa mmefumba macho…”
Mali ya haramu ni kila mali ambayo sheria yetu imehadharisha kutumika na kunufaika nayo ikiwa ni kwa dhati yake au kwa sababu ya kuwepo utata katika upatikanaji wake.
Mali ya haramu kwa dhati yake ni kama maiti, pombe, nguruwe na kadhalika. Iliyo haramu kwa kuwepo utata katika upatikanaji wake kama iliyoibiwa, kupatikana kwa njia za rushwa, kughushi, kupora na riba na kadhalika. Pia ikiwa mtu amedanganya katika hali yake ya kuishi katika nchi hii (Uingereza na kwengineko) kama hana mume na kulipwa malipo asiyostahiki kwa kuwa anae mume anaepaswa kumhudumia.
Mali hii ambayo Muislamu huitumia na hastahiki kufanya hivyo ni haki ya wengine ambao wanaikosa kutokana na kutumiwa na wasiostahiki. Si kigezo wala hoja kwamba ni mali ya serikali au mfano wake kwa hivyo si milki ya mtu kwa sababu wanaolipa kodi serikalini ndio wanaotoa fedha hizi kutumika kwa malengo ya kijamii yanayokubalika hata wakiwa si Waislamu.
Na kutokana na Hadithi iliyopokelewa na ‘Abdullaah Ibn Mas’uud, Allaah amuwie radhi, kwamba:
– أن رسول الله - صلى الله عليه وسلم - قال: "والذي نفسي بيده لا يكسب عبد مالاً
من حرام فينفق منه فيبارك له فيه، ولا يتصدق فيقبل منه ولا يتركه خلف ظهره إلا كان زاده إلى النار أخرجه أحمد
Hakika Mtume Salla Allaahu ‘Alayhi Wasallam amesema:
“Kwa yule ambae nafsi yangu iko mikononi mwake,Hatochuma mja mali ya haramu kisha akaitumia na huku akipata baraka na kuitolea sadaka ikakubaliwa na wala asiiache nyuma ya mgongo wake iispokuwa itamzidishia adhabu motoni.” Ahmad
Bidhaa/mali iliyopatikana kwa njia ya haramu haitolewi Zakaah kwani imekosekana sharti la umiliki umilikaji uliotimia - ni mwenye kuimiliki anaepaswa kutoa Zakaah.
Pia miongoni mwa malengo ya Zakaah ni kuitoharisha mali kwa mujibu wa kauli ya Allaah Subhaanahu Wata’ala katika Quraan Attawbah /103
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
“Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo”
Mali ya haramu haitakasiki kwa kutolewa Zakaah na wala haitohariki. Hubaki katika hali yake ya uharamu mpaka mtu ajiepushe nayo kwanza na kisha kurudi kwa Allaah Subhaanhu Wata’ala kwa toba.
Atawajibika mwenye kumiliki mali hii kujiepusha nayo kwa kuirudisha kwa mhusika na isipowezekana basi kutolewa sadaka kwa niaba ya mwenye kustahiki mali na si kutaraji thawabu wala ujira kutoka kwa Allaah Subhaanahu Wata’ala.
Ikishindikana kuirudisha mali yenyewe kwa kuwa imetumika na mfano wake basi ni wajibu wa alieitumia kutafuta mali inayofanana kuirudisha. Na hata ikitolewa Zakaah basi kisheria haitotambulika kama ni Zakaah bali itahesabika kujiepusha tu na sehemu ya mali asiyostahiki kuwa nayo.
Hivyo kwa mwenye kuwajibika kutoa Zakaah bado dhimma na jukumu la kuitoa litabaki kwake.
Mali ya haramu ikichanganyika na ya halali na kisha kutoweza kufahamika kiwango chake ni kama ifuatavyo:
1. Ima aikadirie mali ya haramu kwa jitihada zake binafsi na kwa kadri Allaah Subhaanahu Wata’ala Atakavyomjaalia na kisha kujiepusha nayo kwa kurudishwa wanaostahiki.
2. Kurudi kwa Mola kwa kuomba toba ya kikweli kweli kwa kosa alilolifanya na baada ya toba hiii atawajibika kuitolea Zakaah.
Itaendelea inshaAllaah…
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
