Skip navigation.
Home kabah

Wasiya Kumi Wa Allaah - Wasiya Wa 8- Kusema (Yaliyo Haki) Kwa Uadilifu Japokuwa Dhidi Ya Jamaa Wa Karibu

 

Wasia wa nane wa Allaah ni kusema (yaliyo haki) kwa uadilifu japokuwa dhidi ya jamaa wa karibu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa):

((... وَإِذَا قُلْتُمْ فَاعْدِلُواْ وَلَوْ كَانَ ذَا قُرْبَى...))

((...Na msemapo semeni kwa uadilifu ingawa ni kwa jamaa…)) [Al-An’aam: 152]

Amri ya kusema ukweli na haki katika kushuhudia jambo dhidi ya watu walio karibu kwa uhusiano au urafiki n.k. Uadilifu huu unaweza kuwa katika kutoa hukmu, au kushuhudia jambo, au kuelezea lolote au pia katika kugawa kitu kwa waliohusika wenye haki nawe.

 

Kupata ufafanuzi zaidi, na kauli ifuatayo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاء لِلّهِ وَلَوْ عَلَى أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقَيرًا فَاللّهُ أَوْلَى بِهِمَا فَلاَ تَتَّبِعُواْ الْهَوَى أَن تَعْدِلُواْ وَإِن تَلْوُواْ أَوْ تُعْرِضُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ))

 

((Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu, mtowao ushahidi kwa ajili ya Allaah ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au masikini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkajitenga nao basi Allaah Anajua vyema mnayoyatenda)) [An-Nisaa: 135]

 

Mtu anaweza kumtetea mtu uongo, au kutoa ushahidi wa uongo kwa sababu kama zilizotajwa kwenye hiyo Aayah, ima labda kujitetea nafsi yake mtu, au kumtetea aliyehusiana naye kwa damu, au rafiki, au tajiri kwa kutaka manufaa kwake, au masikini kwa kumuonea huruma. Yote hayo Ameyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Hata ikiwa kutoa ushahidi dhidi ya mtu uliye na chuki naye au uadui, madamu tu ni haki basi lazima useme ukweli. Hivi ndivyo Dini yetu ya Kiislamu inavyojulikana katika kutimiza haki za binaadamu wote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ لِلّهِ شُهَدَاء بِالْقِسْطِ وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى وَاتَّقُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُون))

 

((Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na ucha Mungu. Na mcheni Allaah Hakika Allaah Anazo khabari za mnayoyatenda)) [Al-Maaidah: 8]

 

 

Kutekeleza amri hii inaweza kuwa ni kauli kama maelezo ya juu, yaani kutoa ushahidi wa jambo, au pia inaweza kuwa kwa vitendo, kwa maana kufanya uadilifu baina ya watu katika kugawa kitu wenye haki ya kupata usawa kwa maana nyingine kumpendelea mmoja zaidi ya mwengine.   

 

 

عَنْ النُّعْمَان بْن بَشِير أَنَّهُ قَالَ : نَحَلَنِي أَبِي نُحْلًا فَقَالَتْ أُمِّي عَمْرَة بِنْتُ رَوَاحَةَ : لَا أَرْضَى حَتَّى تُشْهِد عَلَيْهِ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَجَاءَهُ لِيُشْهِدهُ عَلَى صَدَقَتِي فَقَالَ  ((أَكُلَّ وَلَدِك نَحَلْت مِثْلَهُ ؟))  قَالَ لَا قَالَ:  ((اِتَّقُوا اللَّه وَاعْدِلُوا فِي أَوْلَادكُمْ)) وَقَالَ – ((إِنِّي لَا أَشْهَد عَلَى جَوْر))  قَالَ فَرَجَعَ أَبِي فَرَدَّ تِلْكَ الصَّدَقَة"  البخاري و مسلم

 

Kutoka kwa An-Nu’maan bin Bashiyr ambaye amesema: “Baba yangu alinipa zawadi lakini mama yangu ‘Amrah bint Rawaahah hakuridhikia hadi ashuhudie Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Baba yangu akaenda kwa Mjumbe wa Allaah, akamtaka ashuhudie kunipa kwake zawadi. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: ((Je, umewapa hivyo hivyo kwa watoto wako wengine?)) Akajibu. Hapana. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mche Allaah, na adilisha [timiza haki] kwa watoto wako)) Akasema: ((Mimi sishuhudii dhidi ya dhulma)) Kisha baba yangu akarudisha zawadi yake: [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hivyo kufanya uadilifu kwa kauli na vitendo ndivyo ipasavyo katika amri hizi.

 

 

Itaendelea InshaAllaah…/