Skip navigation.
Home kabah

Wasiya Kumi Wa Allaah - Wasiya Wa 9 - Kutekeleza Ahadi Ya Allaah

 

Wasia wa tisa wa Allaah ni kutimiza ahadi ya Allaah kama Anavyosema (Subhaanahu wa Ta’alaa):

((... وَبِعَهْدِ اللّهِ أَوْفُواْ...))

((…Na ahadi ya Allaah itekelezeni…))  [Al-An’aam: 152]

 

Kutimiza ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kwa maana kutimiza amri Zake Alizotuamrisha na kujiepusha na makatazo yote katika Qur-aan na Sunnah. Vile vile kutimiza ahadi zote nyinigine tunazoahidiana sisi waja.  Ikiwa ni za kawaida au zile ahadi za kuapa kwa jina la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) mfano ahadi baina ya wanandoa, ahadi katika deni, ahadi katika kuamiliana kwa aina yoyote, kwani hayo ni majukumu yapasayo kutimizwa.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

(( وَأَوْفُواْ بِالْعَهْدِ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْؤُولاً ))

 

((Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa)) [Al-Israa: 34]

 

 

Ahadi baina yetu na baina ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ni ile ahadi iliyopokelewa na viumbe vyote kabla ya kuumbwa. Tokea Aadam na vizazi vyake vyote hadi siku ya mwisho. Tukashuhudia na kuchukua ahadi kwamba tutamtii Mola wetu na hatutamshirikisha.  

 

((وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَى أَنفُسِهِمْ أَلَسْتَ بِرَبِّكُمْ قَالُواْ بَلَى شَهِدْنَا أَن تَقُولُواْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ))

((Na pale Mola wako Mlezi Alipowaleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Ndiye! Tumeshuhudia (kuwa Wewe ndiye Mola wetu) (Allaah Akawaambia). Msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo)) [Al-A'araf : 172]

Anawaonya wanaovunja ahadi Zake kwamba watakuwa miongoni mwa waliokhasirika:

 

((الَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الأَرْضِ أُولَـئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ))

 

((Wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kwisha ifunga, na wakayakata Aliyoamrisha Allaah kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye khasara)) [Al-Baqarah: 27]

 

Kutimiza nadhiri pia ni katika kutimiza ahadi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

 

((يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْماً كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيراً))

 

 

((Wanatimiza ahadi, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea sana)) [Al-Insaan:]

 

Pia kutokutimiza ahadi ya aina yoyote hata kama kupeana miadi ya kukutana sehemu au wakati fulani kisha achelewa mtu kufika au asifike kwamwe. Tatizo hili ni sugu, wengi huona kuona ni jambo la kawaida, na imekuwa ni kawaida khasa katika jamii yetu inajulikana kuwa ni ‘miadi ya Kiswahili’ kwa vile mtu humwalika mtu au watu katika shughuli, badala ya kufika muda uliowekwa watu watachelewa hadi kupita  masaa mawili au matatu! Inafika hadi sasa wenye shughuli kutaja nyakati za uongo kwa kukhofu watu kuchelewa kisha wale wachache wenye kutimiza ahadi wanapofika mapema iwe wamepoteza muda wao kuwasubiri wale wasiotimiza miadi yao. Kisha watu huona kuwa miadi ya kweli ni miadi ya Kizungu na hali mafunzo haya tumepewa sisi Waislamu kabla ya hao Wazungu kuja kuyatimiza.  

 

Pia kutokutimiza ahadi kwa upande mwingine ni mfano kuahidi kumpa mwenzio kitu fulani, au kumuahidi kumsaidia tatizo lake fulani, kisha unapofika wakati anamkimbia mwenziwe mtu hata simu zake pengine asizipokee! Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):   

 

((الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللّهِ وَلاَ يِنقُضُونَ الْمِيثَاقَ))

((Wale ambao wanatimiza ahadi ya Allaah wala hawavunji maagano)) [Ar-Ra’d: 20]

Kutokutimiza ahadi ni alama za unafiki kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

 

((آية المنافق ثلاث : إذا حدث كذب ، وإذا وعد أخلف ، وإذا اؤتمن خان)) رواه البخاري ومسلم.

 

((Alama za Mnafiki ni tatu; anapozungumza huongopa, anapotoa ahadi huenda kinyume [hatimizi], na anapoaminiwa hufanya khiyana)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  

 

 

Itaendelea InshaAllaah…/