Skip navigation.
Home kabah

Umuhimu Wa Zakaah - 7: Wanaostahiki Kupewa Zakaah

 

 

Abu ‘Ammaar

 

Wanaostahiki Kupewa Zakaah

 

Miongoni mwa mambo ambayo dini yetu imeyaeleza bayana katika kitabu chake Allah Subhaanahu Wata’ala ni aina na sifa za wanaostahiki kupewa. Takriban wote wanaostahiki wametajwa katika Attawbah/160

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ

Wa kupewa sadaka ni mafakiri, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika Njia ya Allah, na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Allah. Na Allah ni Mwenye kujua (na) Mwenye hekima.

 

Kimsingi, Zakaah lazima wapatiwe wale wanaostahiki kisheria ili nguzo hii ikamilike. Ni wajibu kwa mwenye kutoa Zakaah kuhakikisha inawafikia walengwa. Ikithibitika kwamba haikuwafika waliokusudiwa na wanaostahiki itambidi mtoaji aitoe tena kwani utekelezaji wake bado haujakamilika. 

 

1.     Mafakiri

Ni wale wasiokuwa na chochote cha kuweza kuwatosha katika maisha yao.

 

2.     Maskini

Ni wale wasiokuwa na uwezo wa kumiliki cha kuwatosha katika maisha yao.

Maneno haya mawili yanafanana kimaana na hapo hapo kutofautiana kama ilivyo Uislamu na Iman. Yakitajwa kwa pamoja huwa na maana tofauti ila likitajwa moja tu basi hujumuisha maana zote mbili.

 

Kwa ufupi wanaostahiki Zakaah kwa msingi huu ni wafuatao:

·         Asiekuwa na uwezo kabisa wa kujitafutia rizki yake mpaka wengine kufikia kuomba.

·         Mwenye uwezo kidogo lakini haumtoshi katika kukidhi mahitaji yake upo chini ya asilimia 50.

·         Mwenye uwezo kiasi ambao unazidi asilimia 50 ya mahitaji yake lakini haukamilishi mahitaji yake na wanaomtegemea.

Wote hawa watastahiki kupewa Zakaah kwa mujibu wa hali zao.

 

Tanbihi:

Vigezo vya umaskini vinaweza kutofautiana kati ya nchi na nchi au sehemu na sehemu na maana ya umaskini inaweza kutafsiriwa vyenginevyo hivyo kwa Muislamu ni kuiangalia sheria yetu vipi imemtambulisha Maskini na Fakiri na kuwa kigezo chake wakati wa kutoa Zakaah ili iwafikie waliokusudiwa.

 

3.     Wanaoifanyia kazi

Ni wafanyakazi walioajiriwa katika kitengo cha Zakaah ambao huikusanya na kuisimamia pamoja na kuifikisha kwa wanaostahiki. Hupewa Zakaah kwa mujibu wa mahitajio yao ikiwa tu hawalipwi mshahara rasmi na kitengo walichoajiriwa (wamejitolea). Si sharti kwamba lazima awe ni maskini. Sababu ya kupewa Zakaah ni kule kuitumikia na kuifanyia kazi.

Kama ni dola ya kiislamu, kunakuwa na Baytu Zakaah (Afisi ya Zakaah) ambayo husimamia suala zima la makusanyo, utafiti na masurufu au kuwepo taasisi zinazosimamia Zakaah kwa nchi zisizofuata rasmi sheria za kiislamu.

 

4.     Waliozoezwa nyoyo zao

Ambao wameonesha mwelekeo wa kuingia katika dini ya kiislamu na wamegawika katika makundi yafuatayo:

·         Ambao ndio kwanza wameingia katika dini na bado wana udhaifu wa imani.

·         Ambao bado hawajaingia lakini kuna mwelekeo kwamba wanaweza kuingia.

Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam aliwahi kuwapa Zakaah mfano wa aina hizi wakati wa uhai wake ili kuwapa nguvu na kuwavuta kuja katika Uislamu.

 

5.     Kukomboa watumwa

Ni watumwa ambao wameandikiana mkataba na mabwana wao wajikomboe lakini wameshindwa kupata fedha za kujikombolea.

Ingawa suala la utumwa halipo kwa sasa ila inawezekana kutumika endapo Muislamu ametekwa nyara na anahitaji kukombolewa, Zakaah inaweza kutumika.

 

6.     Wenye madeni

Ni wale wenye madeni na hawana njia wala uwezo wa kuyalipa. Kinachoangaliwa zaidi hapa ni kuwepo deni ambalo limeshindikana kulipwa bila ya kujali hali ya mwenye deni.  Kwa mfano ana vitu ambavyo labda ataweza kuuza ili aweze kuyalipa madeni yake. ikiwa vitu hivyi ni vya kimsingi na anavihitaji katika kumuendeshea maisha yake ya kila siku kama nyumba, gari, fanicha, nguo na kadhalika.

Ikiwa deni limepatikana kutokana na njia za haramu, mwenye deni hatostahiki kupewa Zakaah kulipia deni hili na pia ikiwa ni deni la kujitakia kwa kujiingiza katika mikataba ambayo anajua fika itamuingiza katika madeni.

Ni vizuri jitihada za ziada zikafanyika katika kungalia hali ya mwenye deni na deni lenyewe.

 

7.     Katika njia ya Allah Subhaanahu Wata’ala

Wanaokusudiwa kwa mujibu wa ushahidi katika Quraan ni wapiganaji jihadi wa kiislamu waliojitolea na hawalipwi na dola – serikali. Hata hivyo Maulamaa wamefafanua zaidi kwa kuwahusisha wafuatao pia:

·         Wanaotafuta elimu na hawana mahitaji ya kutosha katika jitihada yao hii.

·         Wanaofanya Da’awah kwa ajili ya kuitangaza dini kwa kujitolea huku wakisumbuka katika kuzihudumia familia zao kwa mahitaji ya kimsingi.

·         Wanaoifanya kazi ya kuifundisha dini – Walimu – kama katika Madrasah na vituo vya kiislamu lakini hawapati pato la kuwatosha kukidhi mahitaji yao.

 

8.     Wasafiri

Wasafiri ambao kwa bahati mbaya wamefikwa na mitihani ya kuishiwa na masurufu (matumizi) na wako mbali na nyumbani kwao kwa:

·         Kuibiwa au kupoteza mali zake na kujikuta hawana kitu cha kuwawezesha kurudi walikotoka.

·         Mwenye kwenda Hajj na alikuwa na masurufu ya kumtosha ila kutokana na mambo ambayo yapo nje ya uwezo wake kama gharama zilizokisiwa na zilizopo kuwa kubwa na kujikuta ameishiwa au kujitosheleza.

Wasafiri hupewa Zakaah ya kuwatosheleza gharama za usafiri kuwarudisha walikotoka tu na pia inawezekana ni wenye uwezo ila wakati huu wa safari tu ndipo walipofikwa na majaribu ya kikosa matumizi.

 

FAIDA

Wakati wa kutolewa Zakaah na kupewa wanaostahiki Maulamaa wamependekeza ikiwa mali iliopo ni ya kutosha na aina zote hizi zilizotajwa zipo basi wagawiwe wote. Ila tu katika kugawiwa si lazima iwe sawa kwa sawa bali itategemea na hali na mahitaji ya mpewa. Na kama ni kidogo, inawezekana kupewa aina mojawapo kwa kuzingatia iliyo muhimu na yenye kuhitaji kwa wakati ule.

Pia itakubalika kisheria ikiwa mali ya Zakaah itapewa kwa baadhi tu ya aina hizi ikiwa kutakuwa na kuna maslaha yanayokubalika kisheria.

Pia katika kugawiwa, ni kuzingatia kuwapa maskini na mafakiri kwanza kabla ya aina nyengine. Kwa  sababu ya kutangulizwa kutajwa katika aya na pia kuelezwa na Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwamba ni lengo kwa kuchukuliwa kutoka kwa matajiri na kurudishwa kwa  mafakiri.

 

Inaendelea…