Umuhimu Wa Zakaah - 8: Wasiostahiki Kupewa Zakaah
Abu ‘Ammaar
Wasiostahiki Kupewa Zakaah
Kimsingi wanaopaswa kupewa Zakaah ni zile aina nane zilizotajwa katika aya ya Attawbah/60. Wasiokuwa hao, hawatopaswa kupewa Zakaah kama:
1. Wasiokuwa Waislamu
Kwa sababu hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam imefahamisha kwamba: “Huchukuliwa kutoka kwa matajiri na kurudishwa kwa mafakiri” miongoni mwa waislamu.
Isipokuwa waliozoezwa nyoyo zao tu wataweza kupewa kwa mujibu wa aya Attawabah/60.
Ama Sadaka nyenginezo wanaweza kupewa wasiokuwa Waislamu.
2. Wazazi na watoto na kuendelea
Kisheria kila atakaepaswa kumhudumia miongoni mwa watu wake wa karibu basi hastahiki kupewa Zakaah. Mume nae hawezi kumpa Zakaah mkewe - kumhudumia ni miongoni mwa majukumu yake. Hali Kadhalika mtoto maskini ambae mzazi wake ni mwenye uwezo ila hamhudumii pia hatopaswa kupewa mpaka atakapofikia baleghe.
Tanbihi
Hata kama waliotajwa ni mafakiri na kuwa sifa za kupewa Zakaah lakini haitojuzu ikiwa Zakaah hii itatoka kwa mtoto/mzazi.
3. Matajiri
Kwa kuweza kujitosheleza na mahitajio yao na kwa kutokana na Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam
لا تحل الصدقه لغني رواه أحمد وأبو دواد وابن ماجه
“Sadaka haimhalalikii Tajiri” Ahmad, Abu Daaud na Ibn Maajah
4. Kabila la Bani Hashim
Nao ni ukoo wa Abbaas, Ali, Jaafar, ‘Uqayl, Haarith na Abi Lahab ibn Abdil Muttalib. Kutokana na Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam: “Hakika Sadaka haipaswi kwa Aali (koo za) Muhammad…” Muslim
5. Mwenye nguvu (uwezo wa) kujitafutia rizki yake
Kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam :
ولا حظ فيها لغني ولا لقوي مكتسب رواه أحمد وأبو دواد
“Hana hadhi (fungu) kwa aliye tajiri na mwenye nguvu anayejitafutia rizki” Ahmad na Abu Daaud
Rizki ya kumtosheleza pamoja na wanaomtegemea
Hata hivyo aina zifuatazo bado zitapewa Zakaah hata kama ni wenye uwezo wa kujitafutia: Mwenye deni, Mwenye kupigana Jihadi, Mwenye kuifanyia kazi, Waliozoezwa nyoyo zao na Wasafiri.
Pia hawatostahiki kupewa Zakaah wale wenye uwezo na kuwa na mali ya kupita kiwango lakini si kwa ajili ya biashara na wala kutoihitajia katika matumizi yao ya kawaida.
Inaendelea…
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


