Umuhimu Wa Zakaah - 9: Masaail Ya Ziada Kuhusu Zakaah
Abu ‘Ammaar
Masaail Ya Ziada Kuhusu Zakaah
1. Jamaa wengine wanaweza kupewa Zakaah kama Kaka, Dada, Mjomba, Shangazi, na kuendelea ikiwa watatimiza masharti yafuatayo:
- Wawe ni miongoni mwa wanaostahiki kupewa Zakaah
- Wasiwe ni miongoni mwa anaopaswa kuwahudumia kama ni wajibu kwa mwenye kutoa Zakaah.
2. Maiti haipewi Zakaah kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kuimiliki. Hivyo Zakaah haiwezi kutumika katika kununulia Sanda wala kumlipia deni alilokuwa akidaiwa enzi za uhai wake.
3. Zakaah haitolewi kwa ajili ya kujenga, kukarabati au kuikimu Misikiti kwa sababu Misikiti ni sehemu ya Ibada na haimilikiwi na mtu - ni nyumba za Allah Subhaanahu Wata’ala.
4. Wakati wa kutoa Zakaah, ndugu na jamaa wa karibu ni bora kuwatanguliza. Kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam:
الصدقة على المسكين صدقة وعلى ذي القرابة صدقة وصلة رواه ابن ماجه
Sadaka kwa Maskini ni Sadaka tu na kwa jamaa wa karibu ni sadaka na kuunga udugu. Ibn Maajah
Na si lazima wanaopewa wajue kwamba hii ni Zakaah (huu ni wajibu wa mwenye kutoa kwani itabidi iambatane na nia lakini si wajibu kwa anaepewa)
1. Ikiwa Zakaah amepewa asiestahiki na kufahamu kwamba si miongoni mwa wenye kupewa Zakaah ni wajibu kwake kutoipokea. Na kama alikabidhiwa kwa bahati mbaya, atakuwa na jukumu la kuirudisha kwa alieitoa.
2. Mwenye kutoa Zakaah ikiwa hana uhakika na hali ya mwenye kupewa kama ni miongoni mwa wanaostahiki, hatopaswa kumpa mpaka awe na yakini kwa kufanya utafiti na kuthibitisha hali yake.
3. Zakaah haitokamilika kwa kununuliwa vitabu kwa ajili ya chuo au Madrasah au kwa kununuliwa ardhi kwa ajili ya matumizi ya Waislamu kama Wakf na kadhalika.
4. Zakaah haitumiki kwa kujengewa Mahospitali, Mashule, Barabara na hata sehemu za kusaidia Waislamu.
5. Haijuzu kuifanyia biashara au kuifanya kitega uchumi mali iliyokusanywa kwa ajili ya Zakaah ili ipate kuongezeka. Kwani si lengo lililokusudiwa. Ikikusanywa tu ni wajibu kuhakikisha inawafika walengwa bila ya kucheleweshwa.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
