Iogope Siku Hii

 

Naaswir Haamid

 

Ni ukosefu wetu wa kumbukumbu na dharau ndizo zinatupelekea kukosa nidhamu mbele ya Ukubwa wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na vile Alivyoviumba. Yareti kama mwanaadamu atakaa kuzingatia Ukubwa wa Yule Muumbaji, katu hatakhasirika kwa kukosa rahma za Mola Mlezi.

Mola Ametueleza kwa kina viumbe vyake vya Moto na Pepo ndani ya Qur-aan. Viumbe ambavyo vitashuhudiwa siku ya Qiyaamah macho kupe kupe. Watakaoingia Motoni watayaona mashaka yake na wale watakaorehemewa kuingia Peponi wataziona neema zake. Allaah Atujaalie miongoni mwa wenye kupata neema za Peponi.

Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatutahadharisha kuhusu Siku hiyo:

{{Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha viumbe wote watalipwa kwa ukamilifu yote waliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa}} [2:281]

Hiyo ndio Siku ambayo mimi na wewe sote tutaishuhudia, namna ambavyo mwanaadamu atashuhudia kifo chake. Jee umepata kufikiria hisabu yako itakavyokuwa Siku hiyo? Watakaonufaika na neema za Mola wao ni wale waliomcha na kutenda mema hapa duniani kwa ikhlaasw ya hali ya juu. Ama wale ambao wamegeuka tumbili kwa kukosa muongozo, watakiona cha mtema kuni.

Basi ndugu yangu Muislamu kumbuka kwamba hapo awali hukuwa chochote. Unamuonesha nani kibri chako hali ya kuwa wewe utakufa. Ewe nafsi... nafsi... Rudi kwa Mola wako kabla ya muda kuisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Je! Mwanaadamu hakumbuki ya kwamba Tulimuumba kabla (ya hali yake hii), hali hakuwa chochote? Basi naapa kwa Mola wako kwa yakini Tutawakusanya wao pamoja na mashetani; kisha Tutawahudhurisha pembezoni mwa Jahannam, wapige magoti (hapo). Kisha kwa yakini Tutawatoa, katika kila taifa, wale miongoni mwao waliomuasi zaidi (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema.}} [19:67-69]

Aya zinazofuatia hapo ni nzito zaidi, kwani zinaeleza kwamba sote tutaingia Motoni:

{{Tena hakika Sisi tunawafahamu sana wanaostahili zaidi kuunguzwa humo. Wala hakuna yeyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia (hiyo Jahannam). Ni wajibu wa Mola wako uliokwishahukumiwa.}} [19:71-72]

Lakini rahma za Allaah ni kubwa na hakika Atawanusuru wale waliokuwa wakimukhofu hapa duniani kwa siri na dhahiri na Atawaacha waovu wakiwa wenye kukhasirika:

{{Kisha Tutawaokoa wale wamchao (Mungu); na Tutawaacha madhalimu humo wamepiga magoti.}} [19:72]

Wahenga walinena: ‘Ukimuona mwenzio ananyolewa, wewe tia maji’. Jitayarishe na Siku hiyo kwa kutenda mema sio kumuasi Mola al-Jabbaari Ambaye adhabu na ghadhabu Zake Hazina mfano wa kitu chochote. Nakuusia usigeuke ngo’mbe aliyekata kamba, kwani kamba aliyofungiwa ilikuwa na maana na faida kwake. Halikadhalika kwako Muislamu, Qur-aan usiikimbie kwani ina faida na maana yake juu yako. Kuwa chini ya Shariah ya Mola sio juu ya Shariah, utaangamia.

Share