Skip navigation.
Home kabah

Hatukuletwa Duniani Kucheza

 

'Abdun-Naaswir Hikmany


 
 
Ameumba Allaah ardhi siku ya Jumamosi na Akaumba ndani yake majabali siku ya Jumapili, na Akaumba miti siku ya Jumatatu, na Akaumba mambo mabaya siku ya Jumanne, na Akaumba nuru siku ya Jumatano, na Akaingiza ndani yake wanyama siku ya Alkhamisi, na Akamuumba Aadam baada ya Alaasiri, ndani ya siku ya Ijumaa ambaye ni kiumbe cha mwisho, katika wakati wa mwisho wa nyakati za Ijumaa, baina ya Alaasiri hadi usiku. ((Ameipokea Imaam Ahmad; Mukhtaar Ahaadiythun-Nabawiyy, uk. 72))


Hadiyth hiyo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inatuonesha dhahiri kwamba mwanaadamu alikuwa ni kiumbe cha mwisho kuumbwa, na akaletwa duniani hali ya kuwa kila kitu kishaumbwa kwa ajili yake. Akatunukiwa hadhi ya uongozi wa ulimwengu huu. Hivi sasa wanaadamu wapo kila pembe ya dunia hii, wakiwa mchanganyiko wa rangi na makabila tofauti.


Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hakuwaacha tu wanaadamu wakakosa muongozo na malengo ya kuumbwa kwao. Hivyo aliwaleta Mitume ('Alayhimus Salaam) ambao baadhi yao walikuja na maandiko matukufu. Qur-aan ni miongoni mwa maandiko hayo matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Ni muongozo wa maneno haya matukufu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ndiyo Muislamu anaweza kuelewa lengo la kuumbwa na asili ya kuumbwa kwake. Nayo Qur-aan yatueleza kwamba tumeletwa duniani kumuabudu Allaah tu:

 
{{Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu}} [51:56]
 
Kulala na kuamka kwetu, kula, kufanya kazi au mazoezi, kutimiza shahawa, kutembea, kuvaa nguo na mengineyo kadha wa kadha, yote yawe ndani ya taratibu bora kabisa za Uislamu. Kinyume cha kuelewa na kutekeleza maagizo ya Aayah hiyo juu, ndio tunashindwa kujinasua na matatizo tuliyonayo. Mashaka ambayo yamerudisha nyuma Uislamu na kutuacha tukikosa muelekeo.


Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mwingi wa Rahma Anatuongoza lakini sisi tunakaidi. Yeye ndiye Anayetupatia upenyo wa khitilafu za shughuli zetu na Anatupa riziki bila ya kuelewa inatokea wapi. Basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ameahidi kumnusuru yule ambaye atainusuru dini ya Kiislamu, ikiwa kwa jihaad ya vita, kujitolea kwa da'awah, matendo au matamshi.


Kwa masikitiko makubwa, tumedharau muongozo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), tukajichagulia mfumo tuutakao wa maisha. Maisha ambayo yamejaa ushirikina, dhulma, ulevi, riba, rushwa, uzinzi, liwaat na kadhalika. Dunia inakaribia kupasuka kwa madhambi yetu. Ghadhabu na laana za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) zinatuteremkia pasi na kutanabahi kwa kufikiri na kuzingatia.


Iweje ulimwengu huu, wenye wataalamu na wasomi wa kulla namna, washindwe kuzuia mfumko wa bei duniani? Wanashindwaje kuhimili mikeke ya mitihani ya dhoruba na mitetemeko? Kila tulifanyalo laenda arijojo. Iwapi heshima yetu wanaadamu?

 

Ubadhirifu na ulimbikizaji mali na haraam kutawala inatufanya hata sisi tunaojaribu kukumbushana japo kwa haya mawili matatu kushindwa kufanya hayo kutokana na kukosekana umeme kwa masiku na mawiki sasa katika nchi zetu. Suala kama umeme ni suala ambalo si la kuisumbua nchi nzima na hasa katika ulimwengu wa leo ambao unajulikana kama wa Teknolojia. Yote haya ni kuwepo na ufisadi na dhulma katika nchi zetu na kubwa ni kuacha mafunzo ya Uislamu na kufuata ya makafiri na mifumo yao michafu. Ni ajabu kuona leo visiwa vya Kiislamu vimetawaliwa na haraam katika kila kona ya ardhi yake kuanzia wenda uchi kwenye fuko za bahari za Allaah bila khofu wala wasiwasi, kuzidi wenye kubwiga unga na wenye kuuuza, ulevi umekuwa hadharani na mabaa hata mitaani, nyumba za wageni za wafanyao zinaa usiku na mchana, wanaosagana na wenye kulawitiwa wakijidhihirisha kwa fakhari kama ardhi wameumbiwa wao, na mengi mengi ya kumkhalifu Muumba wa mbingu na ardhi. Sasa vipi tutaokoka? Na vipi tutaipata Nusra ya Allaah Aliyetukuka?


Naye Muumba wa Mbingu na Ardhi, Anatujibu kwamba, hii mitihani inayotukumba ni kutokana na chumo la madhambi yetu. Anafanya hivyo, ili tu kutuonjesha adhabu ya baadhi ya ufisadi tunaofanza mchana na usiku.

 

“Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu” (30:41).

 

Sasa lengo la hii misukosuko ni nini? Tupate kurudi na kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwani katu hatukuletwa kufanya uharibifu .