Sadaka Inafaa Kupewa Ndugu Na Jamaa?

 

Sadaka Inafaa Kupewa Ndugu Na Jamaa?

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalam aleikum

Kwanza shukran ndugu zangu kjwa munayo yafanya katika hii website jazaa yenu aijua Allaah Azowaj Allaah, Allaah awape afya imaan na umri muendeleze kazi.

Nina swali kuhusu sadaka, je sadaka waweza kuwapa familia na ikawa kama sadaka ama itakuwa ni wajib kuwapa familia. Shukran wa jazakumAllaah bil kheir wa Allaah izidkum.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kutoa sadaka ni wajibu aliopatiwa Muislamu na Mola wake. Hivyo, inatakiwa tuitoe kwa misngi ya Uislamu. Sadaka haifai tu kupewa mtu mwenye nguvu ya kufanya kazi na tajiri.

 

 

Ama watu ambao ni katika familia basi unapowapa sadaka huwa unapata thawabu mara mbili; thawabu ya kutoa sadaka na ya kuunga kizazi. Hii ni kutokana na kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Sadaka yenu kwa jamaa ni sadaka na pia kuunga ukoo)) [Ahmad, Ibn Maajah, An-Nasaiy, At-Tirmidhiy] 

 

Hao jamaa unaweza kuwapatia na hasa ikiwa utawapatia ili wasaidike kimaisha basi utakuwa umefanya jambo zuri sana mbele ya Allaah Aliyetukuka. Kwa hivyo, sadaka anaweza kupatiwa yeyote miongoni mwa watu ila hao tuliowataja hapo juu.

 

Kwa muhtasari ni kuwa hakuna tatizo wala katazo na kumpatia sadaka jamaa yako wa karibu au wa mbali ni thawabu zaidi. Wale ambao hufai kuwapatia, ni jamaa wa karibu ambao wanakutegemea wewe kwa yale majukumu uliyopatiwa na Allaah (‘Azza wa Jalla)   Mfano ni wazazi, mke, na watoto ambao kisheria unabidi uwatimizie mahitaji yao. Mbali na kuwa mke anaweza kumpatia Zakaah yake mumewe kama ilivyokuja Hadiyth Sahihi katika Riyaadhw Swaalihiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share