Skip navigation.
Home kabah

Ni Ajabu

‘Abdun-Naaswir Hikmany

 

Ni mengi ambayo tumeelezwa ndani ya Qur-aan na Sunnah kwa lengo la kupata uongofu. Lakini ni wachache mno wanoelewa hayo. Hata kwa wanaosadiki ukweli huu, kwa namna fulani wanashindwa kuyatekeleza kwa matendo.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tumewaweka kando na tunawajua kuwataja kwa nyakati za dhiki au kejeli. Utamuona Muislamu ni mwenye kumsujudia mno Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pindi shughuli zake za rizki zinapoharibika. Zinapotengenea, huacha ibada hizi kana kwamba hakuwahi kukutwa na mashaka hayo. Wengine wanasubiri hadi ugonjwa uwagongee mlango au Malakul-Mawt awatembelee ndio waanze kuomba msaada kwa kuzitaja kulla aina ya tasbiyh. Si hayo tu, bali tunashuhudia utovu wa nidhamu kwa Mola Mlezi kwenye miziki.

 

Sauti zapandishwa kumtaja Mwenyezi Mungu,

Mwanamke aitoa sauti chini ya mvungu;

Huku ala za muziki zikifunguliwa pingu,

Wana hao wa Shaytwaan wanalipika jungu;

Linalojazwa dhambi na laana za Mwenyezi Mungu,

Wasahau kabisa kuwa wamkasirisha Mola wa Mbingu.

 

 

 

Tutambuwe ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameruhusu matumizi ya mashairi katika arusi na siku ya ‘Iyd kwa masharti kwamba mashairi hayo yasiwe na kejeli, matusi, wala kashfa, na kusiwemo ndani yake ala za taarabu mfano gita na firimbi[i]. Sasa kwa wale Waislamu wakike na wakiume wanaoimba taarabu kwa kutumia majina ya Mungu na sifa Zake, wameipata wapi ruhusa hiyo?

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hakutuumba bure bure tu. Tumeletwa hapa kumuabudu Yeye tu, Mola wa ‘Arshi yenye hadhi kubwa kabisa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

{{Je! Mlidhani ya kwamba Tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi Kwetu hamtarudishwa?
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa Haki, hapana mungu ila Yeye, Mola Mlezi wa ‘Arshi Tukufu.}}
[23:115-116]

 

Alichokuja nacho Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni lazima tukifuate, na yeye ni Mwonyaji miongoni mwa Waonyaji wa zamani waliopita. Dalili zilizo nyingi kuhusu Qiyaamah zimeshatokea. Ni lazima tuachane na matamanio ya nafsi kwa kuichezea shere hukumu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

{{Je! Mnaastajabia Hadithi hii?

Na mnacheka wala hamlii;

Na mmeghafilika tu!

Basi msujudieni Mwenyezi Mungu na mumuabudu.}} [53:59-62]

 

Tunafupisha hapa kwa kueleza: Ni wajibu wa Waislamu kurejea katika hukumu tukufu za Shariah ya Kiislamu.




[i] Uswuulul al-Mu’asharata az-Zawjiyaah, Qaadhi ash-Shaykh Muhammad Ahmad Kan’aniy, uk. 52.