Utafiti Juu Ya Mas-ala Ya Fatwa Iliyozua Mzozo Kuhusu Hukmu Ya Kumyonyesha Mtu Mzima
Shams Elmi (Abu ‘Ilm)
Katika Hadiyth iliyopokelewa na Imaam Muslim katika Sahihi yake kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema: Alikuja Sahla Bint Suhayl kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Akasema: Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi naona kitu (kuchukizwa) katika sura ya ya Abu Khudhayfah pindi Saalim -mtoto wa kulea- anapoingia nyumbani, akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), “Mnyonyeshe”, akasema (Sahla) vipi nimnyomyeshe hali ya kuwa yeye ni mtu mzima? Akatabasamu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akasema naelewa kuwa yeye (Saalim) ni mwanamume mkubwa).
Na katika Lafdhi nyingine; kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Saalim mtumishi wa Abu Khudhayfah alikuwa anaishi kwa Abu Khudhayfah na familia yake katika nyumba yao, akaja Bint Suhayl kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia; Hakika Saalim amekuwa kama wanavyokuwa wanaume, na amefahamu wanayoyafahamu, na hakika yeye anaingia sehemu tulizopo, na mimi nadhani kuwa ndani ya nafsi ya Abu Kudhayfya kuna kitu (kutoridhika) Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia mnyonyeshe atakuwa ni maharimu yako na kile kitu ndani ya nafsi ya Abu Khudhayfah kitaondoka. Akaenda kumnyonyesha na aliporudi akasema, nimemnyonyesha na kile kitu kilichokuwa katika nafsi ya Abu Khudhayfah kimeondoka.
KAULI ZA MAULAMAA:
Amesema Ibn Hazm kuhusu Hadiyth hii ya Sahla baada ya kuielezea katika riwaya zake tofauti anasema: “Maelezo haya yamekuja katika mfumo wa Tawaatur uliopokelewa na wake za Mtume kama ulivutujia, na huyu Sahla Bint Suhayl ni katika wanawake Muhaajiraat (waliohama kutoka Makkah) na maelezo yake yamepokelewa na wengi.”
Na Amesema Ash-Shawkaaniy: “Hadiyth hii imepokewa kutoka kwa Maswahaba na wake za Mtume na jopo la Mataabiiyna, na wakasema baadhi ya wanazuoni kuwa Sunnah hii imefikia daraja ya Tawaatur.”
KAULI ZA MAIMAMU WANNE:
Al-Hanafiyah: Msimamo wa Madh-hab ya Ki-Hanafi ni kuwa; kunyonyesha kunakomfanya mtu kuwa maharimu kwa aliyenyonya kwake ni kule kunakotokea wakati wa utoto, ama kunyonya ukubwani hakupelekei kumfanya mtu kuwa mahram kwa aliyemnyonyesha kwa mujibu wa kauli za Maulamaa na Maswahaba wengi na wake za Mtume isipokuwa tu yaliopokelewa kutoka kwa Mama wa waumini ‘Aaishah kuwa kunyonya kunamfanya mtu kuwa mahram udogoni na ukubwani.
Aidha Imaam Abu Haniyfah amebainisha kuwa muda wa juu kabisa wa kunyonyesha ni miezi thelathini, yeyote atakayenyonya baada ya muda huo, basi kunyonya kwake kutakuwa hakuna mazingatio yoyote ya kisheria.
Al-Maalikiyah: Mtazamo wa Madh-hab ya Ki-Maalik ni kuwa sharti la kuwa mahram kwa kunyonya ni kwa kipindi cha miaka miwili kama kilivyobainishwa katika Qur-aan, ama maziwa yaliyoingia tumboni baada ya miaka miwili hakuzingatiwi kisheria katika hukmu ya umahram.
Ash-Shaafi’iyah: Mtazamo wa Madh-hab ya Ki-Shafii hautofautiani na maimamu wengine kuwa kunyonyeshwa kunakozingatiwa kisheria ili sheria ya mahram izingatiwe ni kunyonya ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Al-Hanaabilah: Aidha Maulamaa wa Madh-hab ya Ki-Hambali nao wana msimamo huo huo wa maimamu waliotangulia.
Kwa mujibu wa misimamo ya maimamu wanne kuhusu hukmu ya kunyonyesha, wote wamekubaliana kutozingatia hukmu ya kunyonya baada ya miaka miwili, isipokuwa Imam Abu Haniyfah aliyeongeza muda wa kunyonya kwa miezi 30 ambayo ni sawa na miaka 2 na nusu.
Dalili waliyoitegemea katika msimamo wao huo ni ushahidi kutoka katika Qur-aan na Sunnah kama ifuatavyo:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
“Na akina mama wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kukamilisha kunyonya” [2: 233]
Na Akasema katika Aayah nyingine:
“Na kubeba mimba na kuacha kunyonyesha ni miezi thelathini” [46: 15]
Katika ushahidi wa Sunnah:
Imepokelewa kutoka kwa Mama wa waumini Ummu Salamah alisema, Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kunyonya kunakofanya mahram ni kule kunakopanua utumbo kwa kunyonya katika titi kabla ya kuachishwa ziwa”
Aidha ushahidi mwengine ni Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Kunyonya ni kule kunakootesha nyama na kukuza mifupa” [Abu Daawuud]
Ushahidi huu ndio uliotolewa na Ibn Mas’uud pale alipoulizwa na mtu mmoja kuwa; kuna mtu wa jangwani mkewe alipata mtoto na akafa mtoto huyo, matiti ya mwanamke huyo yakavimba kutokana na kujaa, yule mtu akaanza kuyanyonya matiti ya mkewe na kuyatema, lakini kwa bahati mbaya funda moja likaingia kinywani, akamuuliza Abu Muusa Al-Ash’ariy naye akamwambia, mke huyo amekuwa haramu kwako, yule Bedui akamwendea Abdullaah bin Mas’uud na kumuuliza, Ibn Mas’uud akamuuliza, je, umeishamuuliza mtu mwengine kabla yangu? Yule bedui akasema ndio nimeishamuuliza Abu Muusa naye akaniambia kuwa mke huyo amekuwa haramu kwangu. Ibn Mas’uud akamuendea Abu Muusa na kumfahamisha kuwa, je hujui kuwa kunyonya kunakoharamisha ni kule kunakootesha nyama? Abu Muusa akasema; msiniulize jambo wakati Ibn Mas’uud yupo miongoni mwetu.
MADH-HAB YA ADH-DHWAAHIRIYAH:
Msimamo wa Adh-Dhwaahiriyah upo tofauti na msimamo wa Jumhuur, wao wanasema kuwa kunyonyesha mtoto au mtu mzima kunapelekea katika umahram, na msimamo huu ndio aidha msimamo wa Mama wa waumini ‘Aaishah, ‘Atwaa, na Al-Liyth, na ushahidi wao ni kuwa:
Maelezo ya Abu Muusa Al-Ash’aariy kwa yule bedui aliyemuuliza, pamoja na kuwa Abu Muusa alisitisha Fatwa yake baada ya kupata maelezo ya Ibn Mas’uud.
Ushahidi mwengine ni ule uliopokelewa kwamba Sa’ad bin Al-Ja’ad mtumishi wa Al-Ashja’iy kuwa baba yake alimueleza kwamba siku moja alimuuliza ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa, “nilitaka kuoa mwanamke lakini alikuwa ameninyonyesha maziwa yake nikiwa ni mkubwa kwa ajili ya dawa, ‘Aliy bin Abi Twaalib akamwambia usimuoe, na akamkataza. (Lakini maelezo haya yana udhaifu ndani yake kama yalivyoelezwa na wataalamu wa Hadiyth.)
Ushahidi mwengine ni ule uliopokewa na Ibn Shihaab kuwa yeye aliuliza hukmu ya kumnyonyesha mkubwa, akasema, aliniambia Urwaa bin Zubayr kuhusu Hadiyth ya Mtume aliyemuelekeza Sahl bint Suhayl amnyonyeshe Saalim mtumishi wa Abu Khudhayfah mara tano hali ya kuwa ni mkubwa, na Sahla akafanya hivyo, na akawa anamuona ni sawa na mtoto wake. Mama wa waumini ‘Aaishah naye akachukua mafundisho hayo na akawa anawaamrisha dada yake Ummu Kulthum na mabinti wa kaka zake wawanyonyeshe wanaume ambao Mama wa waumini ‘Aaishah alikuwa anataka waingie kwake bila kizuizi.
Ushahidi mwengine ni ule uliosimuliwa na Ibn Jurayj amesema; nilimsikia ‘Atwaa Bin Abiy Rabbaah akiulizwa na mtu kuwa, amenyonyeshwa na mwanamke maziwa yake hali ya kuwa ni mkubwa, je, naweza kumuoa? ‘Atwaa akamwambia Hapana (huwezi kumuoa) nikamwambia, hiyo ni rai yako? Akasema ndio, na Mama wa waumini ‘Aaishah alikuwa akiwaamuru mabinti za kaka yake kufanya hivyo.
MTAZAMO WA SHAYKHUL ISLAAM IBN TAYMIYAH:
Mtazamo wa Ibn Taymiyah na mwanafunzi wake Ibn Al-Qayyim ni kuwa Hadiyth ya Sahla bint Suhayl ipo hai, haikufutwa, wala sio khaaswa wala sio kwa ajili ya watu wote, isipokuwa ni ruhusa iliyotolewa kwa dharura kama ilivyokuwa hali ya Saalim na mke wa Abu Khudhayfah, na hukmu inakuwa mwanamke akilazimika kwa dharura kumnyonyesha mtu mzima basi anakuwa mahram yake, lakini akimnyonyesha kwa sababu nyingine hakuzingatiwi isipokuwa anapokuwa mtoto mdogo. Na hii ndio rai ya Ash-Shawkaniy vilevile.
HITIMISHO:
Suala hili ambalo ni la muda mrefu limezua tena mjadala katika masiku ya hivi karibuni kutokana na Fatwa iliyotolewa na mmoja miongoni mwa Mashaykh wa Al-Azhar kutaka itumike katika kuhalalisha mchanganyiko wa maofisini baina ya wanaume na wanawake.
Baada ya kupitia Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu suala hili na kuangalia kauli za Maulamaa wa Kiislamu wa zamani na wa sasa, imetubainikia kuwa:
1. Hadiyth ya Sahla bint Suhayl ni sahihi haina mgogoro wowote na haijuzu mtu kuikataa au kuidhoofisha kwani itakuwa nu kukataa Sunnah iliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
2. Haijuzu kuichukulia Hadiyth hiyo kuwa ni sheria inayofaa kwa watu wote, bali hiyo ni hali maalumu iliyotokea kwa tukio maalum, kama ilivyofahamika na wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
3. Msimamo wa mama wa waumini ‘Aaishah ni Ijtihaad yake kutokana na uelewa wake wa Hadiyth ya Sahla, na hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa alimuamuru dada yake na mabinti za kaka zake kuwanyonyesha watu wazima, tena kwa kutumia chuchu zao, bali kuna baadhi ya maelezo yanayotolewa na baadhi ya Maulamaa kuwa alikuwa akiwataka wawanyonyeshe watoto ambao aliwaona watakuwa na umuhimu baadae wa kuingia nyumbani kwake kama mahaarim. Aidha hamna ushahidi kuwa walikuwa wakiwanyonyesha kupitia chuchu za matiti
4. Aidha hata Maulamaa wanaokubaliana na ushahidi huo kuwa mtu mzima akinyonya maziwa ya mwanamke anakuwa mahram wake, kama ilivyobainishwa na Hadiyth ya Sahla hawakusema kuwa maana ya kunyonya ni kufyonza titi la mwanamke kama inavyofahamika na wengi, bali mazingatio ni maziwa kuingia ndani ya mfumo wa mwili kwa njia yoyote ile.
5. Kauli ya Jamhuri ya ndio yenye nguvu na ushahidi wenye vishiko kutoka katika Qur-aan na Sunnah na ndio ambayo inafaa kuzingatiwa katika mas-ala haya, pamoja na kuheshimu Ijtihaad za Maulamaa wengine.
Wa Allaahu A’alam
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


