Skip navigation.
Home kabah

Nataka Kwenda Nchi Ya Kiislamu Kusoma Dini Wapi Niende?

SWALI:

 

Assalamu Aleykum ndugu zangu in Islam. Nataka kwenda nchi ya kiislam kusoma sina elimu na sina mahram nifanyaje? Nitaka kuwa alima inshaallah is my dream [make duua 4 me pls].


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu njia za kusoma nje. Hakika inakuwa ni vigumu kusaidika japo tutakupatia nasaha za jumla huenda zikakufaidisha kwa kiasi kikubwa.

 

InshaAllaah tuko pamoja nawe dada yetu kwa du’aa ingawa umetuandikia namba 4 hapo badala ya maneno na hali unauliza jambo muhimu. Kuandika kwa mtindo wa namba si jambo la kistaarabu na pia kunaangusha shakhsiyah ya mtu anayefanya hivyo.

 

Tumesema ni vigumu kukupa ushauri kirahisi kwa sababu hukutueleza wewe unaishi sehemu gani ya hii dunia. Sehemu unayoishi ni muhimu kwani ndio tungeweza kukupatia ushauri muafaka katika hilo. Hata hivyo, tutajaribu kukusaidia mbali inakuwa shida aina mbili kwa mwanamke. Jambo la kwanza Uislamu unakataza mwanamke kusafiri peke yake kuchunga maslahi yake ya kibinifasi. Pia kusafiri nje ya nchi ukitopata wasichana wengine wazuri huenda ukaghuriwa mara moja na ukatoka katika njia nyoofu kwa kudanganywa.

 

Ukiwa unaishi katika maeneo ya Afrika Mashariki unaweza kupata vyuo vya karibu vifuatavyo:

 

i.                    Chuo cha Elimu, Chukwani, Zanzibar. Chuo hicho kinachukua wanafunzi waliomaliza kidato cha 6 (A level) au kidato cha 4 kutoka Kenya.

ii.                   Chuo cha Masomo ya Kiislamu na Sheria, Thika, Kenya. Huko huchukua wanafunzi waliomaliza kidato cha 4 au 6 ikiwa wamefanya masomo ya kawaida. Wanafunzi hawa inawabidi wafanye mwaka mmoja, lugha ya Kiarabu. Ama wale waliomaliza sekondari ya madrasa inabidi wafanye mwaka mmoja lugha ya Kiengereza. Na kozi yenyewe ni miaka 4.

iii.                 Chuo cha wanawake cha Kiislamu (Ma’ahad al-Banaat), Nairobi, Kenya. Hiki kinachukua wasichana pekee, kulingana na kiwango chako cha elimu ya Kiislamu ima utafanya kozi yao kwa miaka 3 au 4.

iv.                Kisha ipo taasisi katika nchi inayoitwa, Munadhwamat ad-Da’wah al-Islaamiyah. Taasisi hii kila mwaka huwa inawafanyia mitihani wanafunzi wanaotaka kwenda Sudan kwa masomo. Na huwa wanachukua wanafunzi wengi na masomo yao si mabaya.

v.                 Chuo kikuu cha Zanzibar.

vi.                Chuo cha Kiislamu Morogoro.

vii.              Ni kufanya bidii kwenda katika balozi za Kiislamu na kuwaelezea unachotaka nao watakuelezea mahitaji yao ili uweze kusoma huko. Nchi ambazo zinaonekana nzuri kwa wasichana ni Saudia, Yemen, Sudan, Pakistan na Malaysia.

 

Tunatumai tutakuwa tumekusaidia kwa kiasi fulani.

 

Na Allaah Anajua zaidi