Ufafanuzi Wa Aayah: “Wakaana ‘Arshuu ‘Alaal-Maai 'Na Ikawa 'Arshi Yake Juu Ya Maji”

SWALI:

 

Naomba ufafanuzi wa aya ifuatayo wakaana arshuhuu ala lmaai....... 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunapenda mwanzo kurekebisha kuwa Aayah hiyo haipo katika Suratul Ambiyaa’ (21) bali ipo katika Surah Huud (11). Ni nasaha zetu kuwa tunaponukuu Aayah tuwe makini kutoa rejea sahihi na tutazame kuhakikisha hilo kabla ya jambo jengine lolote. Aayah yenyewe inasema hivi:

 

وَهُوَ الَّذِي خَلَق السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاء لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلاً وَلَئِن قُلْتَ إِنَّكُم مَّبْعُوثُونَ مِن بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُواْ إِنْ هَذَا إِلاَّ سِحْرٌ مُّبِين

Maana ya Aayah hiyo ni: “Na Yeye Ndiye Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita; na ikawa ‘Arshi Yake juu ya maji; (kakuumbeni) ili Akujaribuni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Na lau ukisema: “Nyinyi mtafufuliwa baada ya mauti”; bila shaka watasema wale waliokufuru: “Hakika haya si chochote isipokuwa ni sihiri bayana. (11: 7).

 

Hebu tutazame hii ibara imefasiriwa vipi na wanachuoni wa Tafsiyr.

 

1.      Mwenye Zubdatut Tafsiyr, Dkt. Muhammad Sulaymaan ‘Abdullaah al-Ashqar amesema: “Arshi ya Allaah ilikuwa juu ya maji kabla ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi” (uk. 284).

 

2.      Ibn Kathir naye amesema yafuatayo: “Allaah Aliyetukuka, Anatueleza kuhusu uwezo Wake na nguvu Zake, kuwa Ameumba mbingu na ardhi kwa siku sita. Ametaja kuwa kiti Chake cha enzi kilikuwa juu ya maji kabla ya hapo kama alivyonukuu Ahmad kutoka kwa ‘Imraan Huswayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ‘Kubalini bishara, enyi Bani Tamiym!’ Wakasema: ‘Hakika umetuletea bishara njema na tayari umetupatia’. Kisha akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Kubalini bishara, enyi watu wa Yemen!’ Wakasema: ‘Tumekubali. Hivyo tujulishe kuhusu mwanzo wa mambo na ilivyokuwa’. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Allaah Alikuwepo kabla ya chochote na kiti Chake cha enzi kilikuwa juu ya maji. Aliandika kwenye ubao uliohifadhiwa kila jambo’ …”

 

Muslim naye amenukuu kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Alikadaria riziki za viumbe wote kabla ya kuumba mbingu na ardhi kwa miaka elfu hamsini na kiti Chake cha enzi kilikuwa juu ya maji”.

 

Na al-Bukhaariy amemnukuu Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Je, mumeona kilichotumiwa kuanzia kuumbwa mbingu na ardhi? Hakiko hicho (kilichotumiwa) hakipunguzi kwa kilichomo Mkononi Mwake wa kuume (hata chembe) na kiti Chake cha enzi kilikuwa juu ya maji. Mkononi Mwake kulikuwa na mizani, Aliyokuwa Akiishusha na kuinyanyua” (juzuu ya pili).

 

3.      Al-Qurtwubiy amesema: “Allaah Amebainisha kuwa kuumbwa kwa kiti cha enzi na maji kulikuwa kabla ya kuumbwa kwa mbingu na ardhi” (juzuu 5, uk. 8)

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share