Baina Ya Sheikh Na Shaytwaan
Swaleh Suheil Abeid Bashamakh
(Dubai, UAE)
Katika usiku sana,
Shekhe yuko kitandani
Kihamaki kapambana,
na shawishi za shetwani
Alo na nyingi laana,
aduwi wa Rahamani
Wakaanza ushindani
Na wakati washindana,
ilihali wako ndani
Ikasikika Adhana,
kutoka Msikitini
Shetwani mara kumwona,
Shekhe atoka chumbani
Kazidi kushika kani…
Sheikh
Wakati umewadiya,
wa kwenda Msikitini
Heri kukimbiliya,
niwe wa kwanza swafuni
Wajibu natiya niya,
ni amri yake Manani
Taswali Msikitini
Shaytwaan
Nini zako harakati,
zisokuwa na makini?
Ungali mwingi wakati,
usingizi wajikhini!
Lako kero huliwati,
rudi kwako kitandani!
Kheri uswali nyumbani!
Sheikh
Mimi huwa na maudhi,
nadhikika nafusini,
Fikira zanibughudhi,
najiona mashakani,
Kipitiwa na faradhi, siku kenda kaburini,
Kiulizwa tasemani?
Shaytwaan
Wajali nini kijana,
mbona nyingi tafishani?
Ni kama unavyo ona,
watu bado wako ndani,
Wakati mrefu sana,
wasiwasi ni wa nini?
Hebu jitulize ndani!
Sheikh
Sichoki kufikiriya,
daima n’napo kaa,
Kila mara hunuwiya,
nipate kujiandaa,
Swala inapowadiya,
niiswali ya Jamaa,
Nipate zote Rakaa!
Shaytwaan
Nakuona na mawazo,
wajitiya wahakani,
Usiifanye mikazo,
na kushika sana kani,
Kwa nini mifululizo,
ya kwenda Msikitini?
Swala itakufaani?
Shetwani akamuweza,
Shekhe hakutamakani,
Kabakiya kujilaza,
hakwenda Msikitini
Hadi jua kuchomoza,
akangiya hasarani,
Akashindwa na Shetwani
Shaytwaan
Haina haja kuwaza,
wasiwasi ni wa nini?
Wakati wowote waweza,
asubuhi na jioni
Si haja kujihimiza,
swala haiwezekani
Taswali siku ya thani
Alipovuta nyiradi,
akaja tena shetwani,
Na kitabu maridadi,
cha kupamba fikirani
Kukawa hakuna budi,
wakaanza ubishani,
Shekhe hakujimakini
Sheikh
Nataka kukuuliza,
nipate kwako yakini
Kwa nini waniliwaza,
katu hunipi makini?
Dua sikuzimaliza,
za kumuomba Manani!
Wanizuwiya kwa nini?
Shaytwaan
Kuomba haikulazimu,
ngojea hadi jioni
Tena sana si muhimu,
wajisumbua kwa nini?
Naona una wazimu,
Dua zitakufaliani?
Faida yake sioni!
Sheikh
Sasa nimeazimiya,
kujitowa madhambini
Nataka kwenda tubiya,
kumlekeya Manani
Niyepuke ya Duniya,
yasokuwa na thamani
Tamuomba Rahamani!
Shaytwaan
Wewe ungali kijana,
jipumbaze wangojani?
Tumiya wako ujana,
ishi uwe furahani
Duniya navyoiona,
ndiyo yako burudani
Sasa wangojeya nini?
Sheikh
Nayaogopa mauti,
na kutiwa kaburini
Naupoteza wakati,
kufwata ya Duniyani
Faida yake sipati,
narudi kwa Rahamani!
Niitakase imani!
Shekhe kutoka kazini,
akanuwiya moyoni
Atapofika nyumbani,
atakaa kwa makini,
Ahifadhi Quraani,
mara akaja shetwani
Ukaanza ubishani…….
Shaytwaan
Wapitwa ewe mwendani,
uko hivyo mpaka lini?
Fungua telivisheni,
kuna nyingi burudani!
Vipindi vya Merikani,
na nyimbo za Arabuni!
Ona kama huamini!
Sheikh
Nyimbo zote ni haramu,
faida yake sioni!
Kusikiza si muhimu,
zinanighasi moyoni,
Wamepinga Maimamu,
na wote Wanazuoni!
Nizisikize kwa nini?
Shaytwaan
Ni wengi Maulamaa,
waliyatowa maoni,
Na bado wanakataa,
kuimba si makosani,
Nyimbo zina manufaa,
huwatibu majununi!
Zapumbaza nafusini!
Sheikh
Kuna hadithi zilioko,
nyingi zimeharamisha,
Katika vitabu ziko,
waziwazi zaonesha,
Muziki kwangu ni mwiko,
sitaki naukomesha!
Nyimbo zanikirihisha!
Shaytwaan
Pulika nikuarifu,
utowe shaka moyoni
Naona wajikalifu,
wajitiya mashakani
Hadidhi hizo dhaifu,
mezisikiya zamani
Muziki ni burudani!
Na wakati washindana,
machoni kawatokeya
Alipita msichana,
shekhe hakumwangaliya
Na shetwani hapo tena,
uzuri kumswifiya,
Binti alowapitiya…
Shaytwaan
Mbona hukumwangaliya,
ni kwa nini hutaki?
Mwana yule avutiya,
amenitiya ashiki
Katu sijashuhudiya,
kwenye wote makhuluki!
Ni mzuri hawatiki!
Sheikh
Takuwa kwenye hatari,
kianza kumwangaliya
Namuogopa Qahari,
popote ashuhudiya
Daima natahadhari,
sije nikatumbukiya!
Haramu kumwangaliya!
Shaytwaan
Fikiri wake uzuri,
wala hufanyi vibaya
Ni halali kufikiri,
mara moja hata miya
Basi hakuna hatari,
sana ukimwangaliya!
Jito halina paziya!
Shekhe alipoamuwa,
Umra kutekeleza
Alipoanza khatuwa,
shetwani kajitokeza
Akaja kumsumbuwa,
hakuwata kuuliza
Kaanza kumsemeza…
Shaytwaan
Nakuona hima hima,
kwa kuazimu safari
Hebu mwendani simama,
usende kwanza fikiri
Unipe jawabu njema,
ni kwa nini wasafiri?
Usende nakushauri!
Sheikh
Umra ibada njema,
ni swababu ya safari
Nalekeya nyumba njema,
nitubu kwa Qahari
Hivi sasa nishakoma,
kwake tasitaghafari
N’na madhambi chakari!
Shaytwaan
Wajitiya hatarini,
huna sababu ya sawa
Mimi n’navyo baini,
pesa nyingi utatowa
Kheri nyengine huoni,
kwa nini wachachawa?
Umra huja jaliwa!
Sheikh
Lazima yetu amali,
vyema tuitekeleze
Na katika kula hali,
ovyo ovyo tusicheze
Tumuogope Jalali,
Mema yote tutimize,
Tuzipate Rehemaze!
Shaytwaan
Elewa uyapulike,
maneno yangu sikiya
Tena moyoni uyaweke,
ukae kuzingatiya
Mtu kwa vitendo vyake,
Peponi hataingiya!
Kama urongo nambiya!
Shekhe nyumbani katoka,
kwenda kuwatembeleya
Niya yake ni kutaka,
nasaha kuwatoleya
Waifahamu hakika,
waja alokusudiya
Shetwani akamwambiya…
Shaytwaan
Mbona wajibabaisha,
mwenzangu nakukhofiya
Mno wajihangaisha,
kwa mambo yaso na ndiya
Hebu kweli nijulisha,
lipi ulokusudiya?
Tafadhali niambiya!
Sheikh
Nasaha natakawapa,
wamuogope Jaliya
Waja wasiwe na pupa,
kuitapiya Duniya
Na Mola atanilipa,
haya nalokusudiya,
Ndiyo njema yangu niya!
Shaytwaan
Huko ni kudhoofisha,
waipoteza afiya
Jambo lisonufaisha,
vipi walikimbiliya?
Wasije kufedhehesha,
Waja watakuchukiya!
Aibu watakutiya!
Sheikh
Ni jambo la manufaa,
iwapo wazingatiya
Tawandokeya balaa,
za akhera na duniya
Na ndipo hajiandaa,
Waja kuwalinganiya
Ni hakika nakwambiya!
Shaytwaan
Usijepata hasadi,
ikakufikiya shari
Niogopalo zaidi,
ni kwa wako ujabari
Kiini cha ufisadi,
ni mwingi umashuhuri
Waja watakuaziri!
Shekhe kawa na maswali,
kumuuliza shetwani
Ajuwe zake amali,
za kushawishi nyoyoni,
Kuwapotozeya mbali,
Waja wema Waumini,
Kauliza kwa makini
Kwake ana rai gani,
kwa waliyo mashuhuri
Na atamwambiya nini,
kwa wasiyo mashuhuri
Shetwani hakumukhini,
kajibu kwa ujasiri
Kasema kwa uhodari…
Sheikh
Nakuomba tafadhali,
na mushikili usije
Unondolee muhali,
uambe wafikirije
Imamu wetu Hanbali,
wewe utamsemaje?
Nifahamishe yukoje?
Shaytwaan
Amenimaliza kweli,
naona hawezekani
Kaniuwa kwa kauli,
“Daima shikamaneni
Kwa Suna yake Rasuli,
na mwendo wa Quraani”
Amenishinda zamani!
Sheikh
Kizidi kuuliziya,
jengine talijibuje?
Na Ibni Taymiya,
hebu sema wamwonaje?
Vipi utaniambiya,
elimu yake ikoje?
Nangoja utasemaje?
Shaytwaan
Hajanipapo khatuwa,
kwake sikujimakini
Yeye amenisumbuwa,
meniroga akilini
Sana yamenisumbuwa,
mapigo yake kichwani
Nayeye siwezani!
Sheikh
Na hebu nipa khabari,
ilo kweli utamke
Kuna mwengine hodari,
anayo na sifa yake
Ndiye Imamu Bukhari,
tupashe khabari zake
Wazijuwa swifa zake?
Shaytwaan
Meichoma nyumba yangu,
kwa vile vyake vitabu
Walisoma watu wangu,
waaswi vikawatibu
Na wakarudi kwa Mungu,
dhambi zao wakatubu!
Meshindwa kumjaribu!
Sheikh
Vipi yule mujirimu,
Hajaaj utanambiya ?
Alivyoimwaga damu,
na kuwatesa raiya
Lau wewe ni hakimu,
nini ungemfanyiya?
Amua yako shariya!
Shaytwaan
Lau leo wangekuwa,
kama yeye humu mwetu
Elifu moja wakawa,
kwenye ulimwengu wetu
Ingekuwa yetu dawa,
ya sera yake kwa watu
Yeye ndiye mtu wetu!
Sheikh
Hebu tena niambiya,
kumuhusu Firauni
Ni wengi twamtukiya,
alivyokuwa khaini
Mno kajikufuriya,
kuwa m’ngu Duniyani
Mbona kafa baharini?
Shaytwaan
Sisi twamshajiisha,
kumsaidiya mno
Alivyo tunufaisha,
kwa mambo mengi manono
Yote alokamilisha,
hakuna wake mfano
Ni kweli yangu maneno!
Sheikh
Sema wakumbuka nini,
kuhusu yule shujaa
Bwana Salah Uddini,
asokuwa na tamaa
Alolinganiya dini,
na kuondowa balaa
Kwa nini wamkataa?
Shaytwaan
Tuachane naye huyo,
katuvuruga zamani
Kachafuwa zetu nyoyo,
