Tusikiapo Adhaana
Swaleh Suheil Abeid Bashamakh
(Dubai, UAE)
Bisimilahi naanza, Kwa jina lako Jaliya
Mola wa kila uweza, wa milele kubakiya
Ilahi naomba jaza, nasaha kuhubiriya
Niwezeshe kuwajuza, uma wapatesikiya.
Rabi swala na salamu, zitume kwake Nabiya
Na Swahabaze kiramu, na jamaze twasaliya
Tupate pepo adhimu, pamoja nao kungiya
Tunusuru ya Karimu, dua twakulinganiya.
Baada kukamilisha, dua nalolinganiya
Hamu ni kuwajulisha, waja wapatesikiya
Wale wanaopuzisha, Adhana wakisikiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya
Mtume metufundisha, sharuti katupangiya
Adhana inapokwisha, natumuombe Jaliya
Kazi kuzisimamisha, misikitini kungiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Nawakumbusha Kaumu, Mwadhini kitunadiya
Tujuwe yatulazimu, nyoyoni kunuwiliya
Kutawadha ni muhimu, tuswali sote jamiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya
Adhana yatuarifu, kuwa swala mewadiya
Ni Ibada ya Raufu, upesi kukimbiliya
Tuunge mwanzo wa swafu, Iqama kuingojeya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Mtume wetu kanena, lau watashuhudiya
Watu ndani ya Adhana, na swafu ya awaliya
Wangefanya hima sana, wasibaki kusaliya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Ama Swala bila shaka, kwa Isilamu jamiya
Wakati wake kifika, haraka kuiqimiya
Ni amri ya Rabuka, Quraani metwambiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Tumkumbuke Bilali, ni swahaba wa Nabiya
Alikua wa awali, Uma kuwaadhiniya
Alipendwa na Rasuli, kwa sauti kuvutiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Madukani twawaona, wale wenye tijariya
Wasikiapo Adhana, hamunazo hujitiya
Makini huwa hawana, hawawahi kutikiya
Wasikiapo Adhana, wapuza kuitikiya.
Wangapi barabarani, wengi twawashuhudiya
Simu zao mikononi, wakati zinapoliya
Huwa hawadirikani, upesi kuzitikiya
Bali kiwa ni Adhana, wapuza kuitikiya.
Na wenye tarikilishi, muda wakizitumiya
Swala hawasimamishi, kwa nyakatize kingiya
Shetwani huwashawishi, hasarani wakangiya
Wasikiapo Adhana, wapuza kuitikiya.
Na walo maofisini, kazi zisowaishiya
Mwadhini akiadhini, hawajali kutikiya
Huwa wamo shughulini, waghurika na Duniya
Wasikiapo Adhana, wapuza kuitikiya.
Na wenye telivisheni, ashiki huwazidiya
Vipindi vya Merikani, na mpira wa Ulaya
Hughurika na shetwani, Swala zikawapitiya
Wasikiapo Adhana, wapuza kuitikiya.
Wenzangu jitahidini, tuzifuate shariya
Tuilinganiye Dini, haki kuitangaziya
Tuheshimu Waadhini, Swala wakitunadiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Watamati ikhiwani, tosha nalohubiriya
Tumengiya hasarani, na sote ni masuliya
Tutakwenda sema nini, tufikapo kwa Jaliya?
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
Kitaka lolinakili, shairi kuwatungiya
Ni Swalehe wa Suheli, Hadhirami asiliya
Kijana msema mkweli, Dini kuitumikiya
Tusikiapo Adhana, twapuza kuitikiya.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
