Skip navigation.
Home kabah

Ahadi Isiyotimizika

 

‘Abdun-Naaswir Hikmany

 

 

Kuna tawi moja la sayansi lenye kuelezea kwamba mwanaadamu ni lazima aathirike na mazingira yanayomzunguka ecology. Mazingira yanayojumuisha vitu vyenye uhai na visivyo uhai. Kuanzia kwa mkulima kuhitaji tabibu hadi jembe kuhitaji ardhi ya kulimia.

 

Mwanaadamu pia ni mwenye kuhitajia hata vitu vyenye hatari ndani ya maisha yake na vyenye kuleta matatizo chungu nzima. Kwa mfano maradhi ni lazima yawepo kwa mwanaadamu, kwani kutokana nayo atavumbua dawa. Kuna dalili za vifo ambazo tunaamini zinachangia kwa namna moja au nyengine, mfano ajali. Hivyo, atajikinga na ajali ili kuokoa maisha yake.

 

Na namna hiyo, Muislamu pia anahitaji ushiriki wa washirikina kwa namna ambayo wao wanatuhitajia sisi pia. Kaa ufikirie yareti dunia ingelikuwa yote ni yenye Waislamu wenye imani madhubuti, wapi tungelitoa da’wah? Hata haya maandishi unayosoma sasa yasingekuwepo. Bila ya shaka kusingekuwa na ushindani wala harakati zenye manufaa.

 

Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Akatuumbia mitihani ya kila namna. Kutokana nayo tujiepushe na tujifunze tusiteleze kwayo. Ndani ya mitihani hii ndimo kunapatikana haja ya Muislamu kuwa karibu na Mola Mlezi. Na hakuna mtihani mkubwa alioumbiwa mwanaadamu zaidi ya Shaytwaanur Rajiym.

 

Kiumbe Shaytwaan kila mmoja anaye ndani ya nafsi yake. Wapo Waislamu wanaoathirika naye mno kiumbe hichi kupita mpaka. Hufanywa kuwa ni pumba kwa kupelekeshwa kwenye maovu makubwa makubwa. Utashangaa mno kumkutia Muislamu ni mwenye kulewa, kuzini au kuiba jicho kupe kupe bila ya woga kabisa! Huyo ameathirika kutokana na laghai za Shaytwaan.

 

Urafiki baina ya Shaytwaan na mwanaadamu hudumu kutokana na kiwango cha madhambi anachotenda Muislamu. Pale tu atakaporudi kwa Mola wake kidhati kabisa, ataikuta himaya (ulinzi) wa Mola Mlezi ukiwa upo tayari kumpokea kwa furaha na hamu ya hali ya juu.

 

Ni urafiki baina ya Muislamu na Mola wake ndio huzaa matunda na humpatia utetezi bora kabisa mbele ya Siku ya Hisabu. Urafiki mwengine wowote huzaa uadui tu. Na ni hasara iliyoje kwa mwanaadamu kufuata mkumbo bila ya kuangalia khatima yake. Wale vibaraka vya wakubwa na wanafiki wa kugeuza Aayah za Mola kwa manufaa yao binafsi watakiona cha mtema kuni Siku Hiyo:

 

{{Na wote watahudhuria kwa Mungu (ili Awalipe). Hapo wanyonge (waliopotea kwa ajili ya kuwafuata wakubwa wao) watasema kuwaambia wale (wakubwa wao) waliojivuna (wakaikataa haki): “Sisi tulikuwa tukikufuateni nyinyi; basi je, nyinyi mnaweza kutuondolea kitu kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu?” Watasema: “Angalituongoza Mwenyezi Mungu bila shaka tungalikongozeni. (Lakini sasa) ni mamoja kwetu: tukipapatika au tukisubiri; hatuna pa kukimbilia.”}} [14:21]

 

Kwa wale waliomfanya Shaytwaan kuwa ni rafiki wa dhati ndani ya nafsi zao. Wakaacha kufuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) hadi kutenda maasiyah ya kila namna, hawatamkuta Shaytwaan kuwa ni mtetezi wao kama alivyowarubuni duniani kwa ahadi kemkem. Bali watamruka na hata akihitaji kumpatia msaada wowote, atashindwa tu:

 

{{Na Shaytwaan atasema itakapokatwa hukumu (ya wema kwenda Peponi na wabaya kwenda Motoni; atawaambia wale waasi watakaomng’ang’ania): “Mwenyezi Alikuahidini ahadi ya kweli (na leo Ameitimiza), nami nilikuahidini; lakini sikukutimizeni. Wala sikuwa na mamlaka juu yenu (ya kukulazimisheni kunifuata); isipokuwa nilikwiteni tu, nanyi mkaniitika. Basi msinilaumu, bali jilaumuni wenyewe siwezi kukusaidieni wala nyinyi hamuwezi kunisaidia. Hakika mimi nilikataa kunishirikisha kwenu toka zamani.” Kwa yakini madhalimu watakuwa na adhabu iumizayo.}} [14:22]

 

Hiyo ndio hali ya walioathirika na vitimbi vya Shaytwaan watakavyokuwa Siku ya Hisabu. Shaytwaan si rafiki wa kuwa naye hata kidogo! Hawezi kutupatia ahadi yoyote ya kutusaidia Siku ya Hisabu. Yeye mwenyewe atakuwa mashakani. Tujiepushe naye kwa kila hali. Tuwe macho na vitimbi vyake na tuwe tayari kupigana naye kwa kujiweka karibu na himaya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Himaya ambayo itapatikana tu kwa kutomshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pamoja na kutenda matendo mema.