Skip navigation.
Home kabah

Radhi Ya Mama Inapasa Katika Hali Gani?

SWALI:

Asalaam alaikum, Swali langu radhi ya mzazi inatolewa vipi? Na kwa sababu gani haswa? Mzazi anakutishia kukutolea radhi kila mara ina maana gani? Napenda nipate majibu ya haya mswali halafu nitaelezea historia vipi ilivyo mpaka kufikia kiwango hichi za mzazi, naomba majibu upesi.

Ndugu yenu katika uislamu.


 JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu radhi za mzazi. Hakika inatakiwa ifahamike kwa kila mmoja kuwa wazazi wana haki kwa watoto wao. Hivyo, wanafaa watiiwe katika mema na mazuri na wasiasiwe kabisa katika hilo. Haki hiyo inakuja tu baada ya kumuabudu Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Amekariri hilo mara kadhaa katika Qur-aan Yake, mfano ni, Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo:

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na tuwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyonilea utotoni”. (17: 23 – 24).

Ni maumbile ya mwanadamu anapokuwa ni mzazi kutekeleza majukumu kwa watoto wake – majukumu ya msingi. Hata hivyo, watoto mara nyingi hujitazama wao wenyewe bila kujali kama mzazi anacho au hana. Mwanadamu kimaumbile anapopata watoto hamu yake kubwa ni watoto wake na sio wazazi ambao ndio sababu ya kuja kwao. Kwa ajili hii Allaah Aliyetukuka Akatoa ufafanuzi mrefu kuhusu majukumu ya watoto kwa wazazi wao. Ukumbusho huu umekaririwa mara kadhaa ili kumpatia hisia mtoto atekeleza majukumu yake kwa mzazi wake.

Kiislamu sio hivyo bali kila wazazi wanapokuwa wazee ni nafuu kwetu kwa kiasi kikubwa. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

Amekhasirika, kisha amekhasirika, kisha amekhasirika yule ambaye atawakuta wazazi wake wawili wakiwa wazee, mmoja au wote kisha asiingie Peponi?” (Muslim).

Hakika wazazi kuwa wazee ni neema na ni mlango wa mtu kuingia Peponi.

Na hakika ni kuwa kumuasi mzazi au kumpenda mtu mwingine kama mke kuliko wao kunakupelekea katika madhambi na pia huenda ukaingia Motoni kama kisa cha Alqamah (Radhiya Allaahu 'anhu). Bahati yake njema ni kuwa mamake alimsamehea akiwa katika kukata roho (adh-Dhahabiy).

Utiifu kwa wazazi unakuja baada ya utiifu kwa Allaah Aliyetukuka lakini utiifu kwa wazazi una mipaka. Ipo hali moja ambayo mtoto hafai kumtii mzazi wake nayo tumefahamishwa na Allaah katika Qur-aan. Allaah Anasema:

"Na wazazi wako wakikushurutisha kunishirikisha na yale ambayo huna elimu nayo usiwatii; lakini kaa nao kwa wema hapa duniani" (31: 15).

Hii ni hali ambayo hufai kuwatii kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba".

Hata hivyo, katika hali yoyote ile ni lazima uwatii na hata wakikuamrisha mabaya wewe hufai kuwatii tu lakini unatakiwa usuhubiane nao kwa wema hapa duniani. Sababu ni kuwa haki yao ya uzazi haipomoki (haiondoki) kwa wao kufanya ubaya au kuamrisha mabaya.

Tatizo tulilo nalo sisi ni kuwa huwa tunakaidi amri zao katika mema kwa sababu tu tumekuwa sisi tunajiweza kutekeleza ya kwetu na hilo sio sawa kwetu. Ikiwa tutakosa kuwatii katika mema basi wakitoa radhi zao huwa Allaah Aliyetukuka Anawaitikia hivyo kukuweka wewe mahali pabaya.

Wakati mwengine wazazi nao huwa wana makosa wanataka watoto wao wawatii katika maasi na maovu na wakikosa kutiiwa basi huwa wakali na kutishia kutoa radhi zao. Katika hili la pili hata wakitoa radhi zao huwa bado wewe uko katika radhi za Allaah Aliyetukuka.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atupe masikilizano na wazazi na Atufishe hali wakiwa radhi nasi, nasi pia tuweze kuwatimizia katika mema wanaotuamrisha.

Na Allaah Anajua zaidi