Mtukufu Ramadhani Tujumuike Kaumu
‘Abdaallah ‘Alwi Bafagih
(Toronto, Ontario, Canada)
Jamii nawajieni Na ujumbe maalumu
Nataka mupulikeni Muzidi kutakalamu
Waingiya Ramadhani Mwezi wetu wa saumu
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Kati ya nguzo zetu Tukumbuke Ramadhani
Sisi na vizazi vyetu Tulihimizwa ayani
Na hata Mtume wetu Katuhimiza jamani
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Saumu ina makuu Sababuze taweleza
Mwili wapata nafuu Mlitambule la kwanza
Yatuonyesha matuu Masikini wasoweza
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Nao waso Isilamu Kuijuwa walitaka
Maana hino saumu Isilamu waloshika
Walipoona kaumu Wote wameamarika
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Awali walielezwa Mola katuamrisha
Ni shuruti kufuatwa Katu hatuto kanusha
Na adhabuye n'kubwa Wasiyo imairisha
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Wakazidi uchunguzi Kwa wingi na tahayuri
Wakajitweka makazi Yaso yao makafiri
Wakaona ni vizazi Wafungao kwa hiari
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Hapo hawakukomeya Ushupavu kuzidiwa
Saumu kuikemeya Ina madhara makubwa
Kumbe wamekoseya Ndio tiba yetu kubwa
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Imedhihiri zamani Tiba nzuri saumu
Uchafu wa matumboni Na viini maalumu
Hata wana wavyuoni Amri wame salimu
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Miskitini Khalaka Jamii huongezeka
Madarasa kadhalika Elimu kuelimika
Sote twafaidika Hili ni kweli hakika
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Kuna haya madhumuni Ambayo 'taka wajuza
Imani tuzidisheni Dini kutoipuuza
Si sharuti Ramadhani Ndipo tukajitokeza
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Wasiya n'nawapeni Jamii i'l Islamiya
Tuwesote Ikhwani Dini kuisimamiya
Tamuepuka shetwani Wallahi nawaapiya
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
Kikomoni mewasili Tamati nahitimiya
Jina langu la kamili Abdalla Al'Sharifiya
Wa Takaungu asili Kilifi nimekuliya
Mtukufu Ramadhani Tujumuike kaumu
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
