Nani Mwenye Haki Kuchukua Vyombo Vya Mume Wangu Aliyefariki?

Nani Mwenye Haki Kuchukua Vyombo Vya Mume Wangu Aliyefariki?

 

 

 www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Ni haki kuchukua vyombo nilivyokuwa na tumia na aliyefariki mume wangu. Vyombo hivyo viko kwa baba wa aliyefariki mume wangu. Na mimi nimesharudi kwetu, na watoto wanaishi na babu yao. Mimi sijachukua kitu chochote. Na Mali za Mume wangu ni pamoja na gari na linafanya kazi. Ni haki nami nipate senti.

 

Watoto ni wanne. Babu yao anasema yeye ndie atawalea watoto hao. Naomba Ushauri

 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 Hakika ni kuwa mara nyingi wanawake wanadhulumika au wanadhulumiwa na jamaa za mume pindi mume anapoaga dunia. Hili ni jambo ambalo ni kinyume na sheria ya Kiislamu.

 

Mwanzo ni kuwa mume anapokufa inatakiwa vyombo na vitu vyote ambavyo mume alimpatia mkewe kama zawadi, hidaya, tunu au kwa sababu nyengine yoyote vinabakia kuwa ni vya mke. Na haifai kabisa vitu kama hivyo kuchukuliwa kutoka kwake kwa njia yoyote ile.

 

Jambo la pili ni kuwa kwa vitu vyengine alivyoacha mume kila mrithi anafaa apate haki yake kama Alivyogawa Allaah Aliyetukuka. Mke amepatiwa fungu lake la thumuni (1/8) kwa vilivyoachwa na mume. Allaah ('Azza wa Jalla) Anasema:

Na wake zenu watapata robo mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Mkiwa mna mtoto basi sehemu yao ni thumuni ya mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni” (4: 12).

 

Kwa hiyo, aliyofanya baba mkwe si sawa kisheria kabisa.

 

Ili kusaidika unatakiwa uende kwa Qaadhi kama uko katika nchi ambayo ina ma-Qaadhi ili uwasilishe kesi yako. Na ikiwa uko sehemu ambayo hakuna Qaadhi basi itabidi uende kwa Shaykh anayeaminika ili kuwasilisha hiyo kesi.

 

Tunakutakia ufanisi na kupata haki yako unayostahiki.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share