Skip navigation.
Home kabah

Sifa Za Mtu Wa Peponi

 

'Abdun-Naaswir Hikmany

 

 

Je, umeamka na Swawm leo?

Je, umehudhuria mazishi leo?

Je, umemlisha masikini leo?

Je, umemtembelea mgonjwa leo?

 

Tuchukulie kila suala hapo juu lina alama 25 na jumla yake ni 100. Hivyo kama umejibu yote 'ndio' basi unazo alama 100 kamili. Na hizo ndio sifa za mtu wa Peponi.

 

Bila ya shaka wapo wengine watashangaa kwa kuiona pepo ni nyepesi kwa kuyafanya hayo tu. Bal, Laa! Sivyo hivyo. Yatakikana vitendo hivyo kufungamana na kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala). Vitendo hivyo viwe huru na shirki na riyaa. Vifuatane na kuziweka kifuani nguzo za imani pamoja na kutekeleza nguzo za Uislamu bila ya upungufu wowote.

 

Matendo hayo manne ni mwenendo uliokuwa umeyapamba maisha ya Sayyidna Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu). Ambaye hakika alikuwa ni Swahaabah aliyebashiriwa pepo kabla ya kifo chake.

 

Huyu ndiye Sayyidna Abu Bakr aliyeitwa 'Mkweli Muaminifu' hakuacha kusadiki yale yote asemayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama yakiwa ni yenye kustaajabisha.

 

Alikuwa ni Swahiba wake wa mwanzo kuamini Utume wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakusita alipopatiwa da'awah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuingia kwenye Uislamu, mara moja alikubali bila ya kudadisi. Huyu ndiye wakala wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye shughuli zake nyingi azifanyazo. Abu Bakr alikuwa kifua mbele kuisadikisha ziara ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ya Israa na Mi’iraaj na ndiye aliyehama pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwenda Madiynah.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesimulia ya kwamba hayakutani mambo haya manne isipokuwa Muislam huyo atakuwa na sifa ya mtu wa Peponi:

 

Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza:

"Yupi kati yenu asubuhi ya leo amefunga?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: "Mimi".

Kisha akauliza tena:

"Yupi kati yenu aliyehudhuria mazishi siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: "Mimi."

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza tena:

"Yupi kati yenu aliyemlisha masikini siku ya leo?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: "Mimi."

Akauliza tena:

"Yupi katika yenu aliyemtembelea mgonjwa?"

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu) akasema: "Mimi."

Kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Hayajumuiki yote haya kwa mtu, isipokuwa ataingia Peponi."

[Imepokewa na Muslim]

 

Sifa ya mtu kufaulu masomo yake ni kuonekana akiwa na juhudi ya kusoma na bidii ya hali ya juu. Sifa ya kafiri ni kuacha Swalah na kuikana kalimah ya Uislamu. Na kwa hakika sifa za watu wa motoni ni kuwa waovu, makafiri au wanafiki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atuepushe na adhabu Zake. Na hizi sifa nne zilizotajwa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndizo sifa za mtu wa Peponi. Nazo ni:

 

1) Kufunga Swawm

2) Kuhudhuria mazishi

3) Kulisha masikini na

4) Kutembelea mgonjwa

 

Kama tutazichunguza kwa makini sifa hizo nne tutagundua kwamba ni la mwanzo tu lenye kufungamana na faida ya Muislam mwenyewe binafsi. Yaliyobaki yote ni ya kuitumikia jamii inayotuzunguka, bila ya kujali dini, rangi, umri, jinsia wala kabila.  Hivyo, asilimia 75% ya maisha ya Muislam ni katika kuitumikia jamii inayomzunguka na sio kujifunga kwenye ibada tu peke yake.

 

Ni kusema kwamba, Muislam anaposhikamana na sifa hizi, basi atakuwa ni mwenye kuisaidia mno jamii yake inayomzunguka. Ni tabia inayojijenga kidogo kidogo kwa uzuri kabisa kujizoesha sifa hizi hadi kujikutia ukimtumikia mgonjwa badala tu ya kumzuru ukaondoka.

 

Sifa hizi zinatudhihirishia kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) sio tu Anatoa malipo kwa zile ibada zinazofanywa kumuabudia Yeye tu kama Swalah na Swawmu, lakini pia Anatilia mkazo mno katika kuihudumia jamii. Lakini Waislam hivi leo wanaonekana kuwa ni wageni mno kwenye nyanja ya kuihudumia jamii inayotambulika kana kwamba ni sekta maalum inayohitaji kuhudumiwa na makafiri kutoka Magharibi.

 

Haya ni mambo ambayo kila Muislam yatakiwa kujipamba nayo iwapo anahitaji kidhati kuwa na sifa za mtu wa Peponi. Wapi utampata masikini au mgonjwa na wapi utahudhuria mazishi hilo ni suala lako kulifanyia uchunguzi kwa kina. Kwani Sayyidna Abu Bakr hakuambiwa ya kwamba kulikuwa na mazishi au mtu yule ni masikini anayehitaji kusaidiwa. Hakuombwa wala kunyenyekewa kutoa msaada wake kwenye masuala haya. Alitoa kwa ridhaa yake bila ya kinyongo na moyo wake ukiwa na lengo moja tu: kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

Sifa hizi zinaturudisha kwenye Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayosema:

 

((Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya wakati utakaoshughulishwa na mambo mbali mbali, na maisha yako kabla ya kifo chako.)) [Al-Haakim]

 

Ukweli unadhihiri kutokana na Hadiyth hiyo hapo juu kwamba, yatakiwa Muislam kujipamba na sifa hizi za mtu wa Peponi kwa kutumia afya yake kutembelea wagonjwa, kutoa mali yake kwa kulisha masikini, kutumia faragha yake kwa kufunga Swawm na kuhudhuria mazishi kabla ya kifo chake.

 

Baada ya kupata utangulizi kwa muhtasari kuhusu sifa hizi. Sasa ni vyema tukaanza kuchambua athari ya sifa moja baada ya nyengine ili Atakapopenda Allaah tushajiike kuyafanyia kazi.

 

 

1-Athari Ya Swawm

 

Swawm sio tu siku za Ramadhaan, bali ni vizuri zaidi Muislam akawa ni mwenye kuwa na Swawm za Sunnah nje ya Ramadhaan pia. Muislam anayeelewa lengo la kuumbwa kwake haachi kuhimizwa mara mbili. Ni yule anayefahamu fadhila za kumtumikia Mola ndio hujihimiza mwenyewe kufunga kwa kutaka radhi za Allaah tu.

 

Kabla ya yote, tuelewe kwamba lengo la Swawm, iwe ni ya faradhi au Sunnah ni kuwa mcha Mungu. Ni kumukhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pekee ndio azma inayotakiwa kuwemo ndani ya moyo wa mwenye Swawm.

 

Hapa ndipo Muislam anapopata kujitakasa mbele ya Muumba wake. Siku yake nzima huitanguliza kwa ajili Yake Yeye Pekee tu. Muislam anapofunga huwa hatamanishwi na lahwa za dunia hii, zilizokuwa mfano wa plastiki linapounguzwa huyeyuka mara moja tu. Plastiki ambalo linageuzwa kila umbo mwanaadamu analohitaji kutengeneza.

 

Swawm inampatia Muislam mafungamano baina yake na Muumba wake. Hakuna ajuaye ukweli wa Swawm ya Muislam isipokuwa nafsi yake na Muumba wake. Ni wakati huu ambao Muislam huzungumza na Mola wake akiomba radhi Zake na kughufuriwa dhambi zake zote. Halikadhalika, du'aah ya mwenye Swawm ni yenye kupokewa na Allaah.

 

Swawm humtakasa Muislam kwa kujizuia na maovu makubwa na madogo yake. Kupitia Swawm, huweza kuacha kuzungumza uongo na usengenyaji. Ndio wakati huu ambao huwa karibu na Qur-aan pamoja na kutekeleza amri zitokanazo humo.

 

Pia, Swawm huweka ulinganifu baina ya masikini na tajiri. Waislam wanapokuwa kwenye Swawm huwa kitu kimoja, kwani huacha kula na kunywa. Hahitaji chakula chake kitamu aliye tajiri na wala sahani iliyo tupu kwa masikini. Hapa ndio tajiri anapata kuwaza na kuwafikiria masikini na ndipo anapojitahidi kutekeleza ile sifa ya nne ya mtu wa Peponi kwa kumlisha masikini.

 

Swawm inafanana na mtu kukaa njaa siku nzima. Na kama njaa hii itaendelea kwenye mazingira ya dhiki na shida husababisha watu kukosa kula na kutumbukia kwenye janga la maradhi tofauti. Hapa ndipo ugonjwa unaposababishwa, na kuibuka mahitaji ya mgonjwa kuliwazwa na kuangaliwa kwa karibu mno.

 

Moja miongoni mwa faida kubwa za kiafya za Swawm ni kwamba, Swawm ni njia nzuri ya watu kuacha kula ovyo na kujiepusha na mambo ya upuuzi. Swawm inajulikana kuwa ina athari nzuri kwa baadhi ya maradhi kama saratani na kifafa.


Kuacha matamanio yako ili kwamba yaweze kutimizwa katika wakati unaofuata ni njia muhimu ya kuudhibiti mwili mzima. Inaufanya mwili pamoja na akili kuweza kupanga mambo vizuri kwa siku zinazokuja.


Hivyo, badala ya matendo yetu kutupangia, ni miili yetu inayotupangia. Swawm ipo ndani ya bongo zetu, na ni bongo hizi zinazotufanya kuwa ni binaadamu; wenye kubadilika na kuweza kupata mafanikio kwa kudhibiti mazingira yetu.


Bila ya shaka, maradhi makuu ambayo yanashauriwa kupatiwa matibabu ya Swawm ni kula kupita mpaka. Matatizo ya kula sana yapo zaidi nchi za Magharibi, ambayo yanasababisha maradhi ya moyo, sukari, saratani na mengineyo. Swawm ni njia bora ya kudhibiti maradhi haya, na muhimu zaidi ni njia ya kuzuia hayo maradhi.

 

2- Athari Ya Kuhudhuria Mazishi

Tumpwekeshe Mwenyezi Mungu Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Pekee na tujihadhari na kusahau mauti. Kusahau kwetu mauti ndio kunapelekea kutenda maovu chungu nzima. Ndipo hata Muislam anapofanana na kafiri kwa kuacha kwake kuswali. Yote hayo yanafanyika kwa sababu ya kujidai kusahau mauti.

Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuhimiza kujitahidi kukumbuka mauti;

((Zidisheni katika kukumbuka mauti)) [Imepokewa na At-Tirmidhy, Ahmad na Ibn Maajah]

Njia iliyo nzuri zaidi ya kukumbuka mauti ni kuhudhuria mazishi. Muislam anapofariki ni vyema kukumbuka mema yake na kumuombea du’aa na kumtakia maghfira katika wakati wa Swalah ya Jeneza. Hivyo ni muhimu kuhudhuria mazishi, kwani kila mmoja wetu atapita njia hii. Na hakuna asiyehitajia du'aah njema kutoka kwa ndugu yake.

Sifa hii ina ugumu wake kuitekeleza kuliko sifa zote tatu. Kwani yahitaji kujitolea na kupania kisawasawa. Yawezekana ukatimiza sifa zote tatu, likabakia hili na kujikutia unalala bila ya kulitekeleza. Usikate tamaa kwani 'kwenye nia pana njia'. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atakufunulia njia Atakapopenda.

Labda tutoe kisa cha kweli ambacho kimemkuta kijana Muislam:

Aliamka siku ya mwanzo ya Ramadhaan akiwa na shauku kubwa ya kutekeleza sifa zote hizo nne. Hivyo, alikuwa kwenye sifa moja ambayo ni Swawm. Alihitaji nyengine tatu. Siku ya nyuma yake alipokea maagizo kutoka kwa mzee wake akimtaka kwenda eneo fulani kwa ajili ya kutoa sadaka ya vitabu kwenye Madrasah moja. Wakati akielekea huko nyakati za saa sita mchana alipita eneo la msikiti na kukutia dalili ya mazishi. Hakurudi nyuma aligeuza na kuingia msikitini kuhudhuria mazishi.

Alipotoka mazikoni, alikwenda kutimiza sifa mbili zilizobaki. Ambazo ni kutembelea mgonjwa na kumlisha masikini. Hivyo, aliulaza mgongo wake kwenye kitanda akiwa ametekeleza yote manne 'Alhamduli Llaah'.

Sio hilo tu. Wapo ndugu wengine ndani ya jamii zetu wanafungua redio kwa ajili ya kusikiliza matangazo ya vifo ili kuisaka sifa hii tu basi. Na anapoikamata haiwachi hadi aitekeleze.

 

Ni kweli kwamba maeneo ya ughaibuni ni ngumu kulitekeleza hili kwani hakuna matangazo ya vifo na maeneo ni mbali mbali mno. Lakini kama tulivyosema 'penye nia pana njia'. Insha Allaah, Mwenyeezi Mungu Atakuongoza kama kweli unahitajia sifa hii.

 

Sio vyema kusubiri hadi rafiki au jamaa wako wa karibu afariki ndio uhudhurie mazishi. Kwani kila mmoja wetu atapita kwenye njia hii ya mawt, lililo bora ni kumswalia Muislam mwenzio hata kama humuelewi.

 

Kumswalia maiti kunamfutia maiti madhambi yake na huwenda kwayo ikapatikana nafuu insha Allaah.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakuna mtu Muislam aliyekufa, basi wakasimama (wakamswalia) katika jeneza lake watu arobaini, wasiomshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote, isipokuwa Atampatia (maiti) msamaha ndani yake" [Imesimuliwa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Muslim]

 

Pia amesema:

 

"Mnapomswalia maiti fanyeni wingi wa kumuwombea du'aa" [Imesimuliwa na Abi Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Abu Daawud]

 

Malipo hayapo tu katika kumuombea dua'ah maiti, bali pia kwa anayehudhuria mazishi:

 

"Mwenye kulifuata jeneza la Muislam kwa iymaan na kutaraji thawabu, na akawa nalo (jeneza) hadi akamswalia na kuingizwa ndani ya kaburi, basi hurudi na qiyraatun mbili, kila qiyraatun ni mfano wa mlima Uhud" [Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘Anhu) na kupokewa na Al-Bukhaariy]

 

 

3-Athari Ya Kumlisha Masikini

 

Hapa ndipo panapopatikana ladha ya kuona na kuhisi ile hali ya umasikini kwa ndugu yako. Hali hii yaweza pia kumkumba yeyote miongoni mwa matajiri. Kwani hakuna anayejua mwisho wake mtu.

 

Kulisha masikini kwa anayetaka Pepo ni muhimu kwa kila Muislamu mwenye uwezo. Dhahiri iliyopo ni kuwa Waislam wengi wasingependa kuona amali zao za khayr ni chache mbele ya Muumba Siku ya Hesabu kwa sababu tu ya kuacha sifa hii ambayo ni sehemu ndogo tu ya mali yao:

 

{{Wala wasidhani wale ambao wanafanya ubakhili katika Aliyo wapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni kheri yao. Bali hiyo ni shari kwao.}} [Suratul-Imraan: 180]

 

Kuna bishara njema ya malipo makubwa atayopata Muislamu anayemlisha masikini. Uislamu unatueleza kwamba anayelisha masikini:

 

§         Atapata malipo makubwa;

§         Atapata khayr;

§         Atakuwa amefanya wema;

§         Atapata ujira;

§         Hatakuwa na hofu;

§         Hatahuzunika;

§         Atakuwa amesafisha mali yake na

§         Kujenga uhusiano mwema na watu wengine.

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza kuwalisha masikini mpaka kwenye shughuli zetu. Na amekemea mno kwa waliymah kuacha kuwapatia nafasi masikini:

 

((Chakula kiovu kibaya kabisa ni chakula cha karamu ya harusi ambayo wamealikwa matajiri na kutengwa kando masikini.)) [Muslim na Al-Bayhaqiy]

 

Bila ya shaka, uwezo wetu wa kupanga kutokana na mafunzo ya Swawm ndio unatuwezesha kuwa ni wingi wa kutoa ndani ya maisha haya kwa lengo la kufanikiwa zaidi maisha ya baadaye ya Qiyaamah. Hivyo, kumlisha masikini kwa ajili ya kupata radhi za Allaah ni funzo bora la kwamba ni 'amali njema.

 

Kuna mgongano wa mawazo ndani ya nafsi ya mwanaadamu baina ya kumlisha na kutomlisha masikini. Hivyo, kuweza kuimiliki nafsi yako ni njia muwafaka ya kujiweka huru na utumwa wa nafsi.

 

 

4-Athari Ya Kutembelea Mgonjwa

 

Mwanaadamu ameumbwa na hali mbili kuu; uzima dhidi ya ugonjwa. Ni hali zinazoenda sambamba ndani ya maisha ya mwanaadamu. Hakuna shaka yoyote ya kwamba hakuna kiumbe kilicho kosa sifa ya kuugua.

 

Anayemukhofu Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) daima huwa anawaza baina ya hali hizi mbili na khofu yake inakuwa kwenye uzima na uhai. Kwani kila neema ni mtihani na utaulizwa kwayo na ni neema hiyo ndio huweza kumpoteza mja katika njia iliyonyooka. Anayemukhofu Muumba huwa daima yuwaza namna alivyo tofauti na ndugu yake mgonjwa; anayetaabika, kuteseka na kudhoofika kutokana na maradhi.

 

Dhiki ya mgonjwa inatulizwa kwa kiwango kikubwa pale anapotembelewa. Sio tabibu pekee anayeshiriki kumpatia huduma mgonjwa. Na ndio maana yakawekwa masaa maalum ya kutembela wagonjwa. Wakuu wa hospitali wamechunguza na kuelewa umuhimu wa wasio wagonjwa kuwatembelea walio wagonjwa. Na aliye mkuu wa matabibu hawa ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeamrisha kutembelewa wagonjwa miaka 1400 iliyopita!

 

Wangapi wapo vitandani wakiugua miaka nenda miaka rudi? Leo una uzima wako unashindwa kumtembelea hata jirani yako unayefahamu fika ya kwamba anaugua. Kunahitajika kuwepo mahusiano ya karibu baina ya mzima na mgonjwa.

 

Walipita watu maarufu ambao sasa wamekwishafariki. Hao hawakuwa tu Waislam peke yao, bali hata wasio kuwa Waislam walishikilia kamba barabara ya kufuata mwenendo wa Sayyidna Abu Bakr (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutembelea wagonjwa. Hawakwenda kuzuru tu wagonjwa, bali pia kuwahudumia. Hii ni hali inayokuja wenyewe (automatic) wakati wa kumtembelea mgonjwa. Muhali waondoka wenyewe, na unaanza mwenyewe kusukuma kiti cha maringi cha mgonjwa kumpeleka kwenye kitanda chake na mara wachukua kikombe kwa ajili ya kumsuuzia ili apate kunywa uji wake.

 

Haifai kuiga sifa za wanasiasa ambao wanatembelea maeneo haya ya wagonjwa vipindi vya uchaguzi au wakati wa maafa makubwa makubwa tu. Wanafanya hili ili kupata ridhaa ya macho ya wananchi wao ambao hawatosheki hata wakipatiwa milima ya dhahabu.

 

 

Hitimisho

 

Uislamu wetu ni njia bora ya kupata mafanikio hapa duniani na kesho Qiyaamah. Matendo ya Muislam yahitaji kufanywa kwa ikhlaasw bila ya kumshirikisha Mola Mlezi. Anayepokea amali hizi njema ni Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na yastahiki tuzitekeleze kwa ajili Yake tu.

 

Hayo mambo manne ni mepesi kabisa kama Muislam atajihimiza nayo, haswa ndani ya kipindi hichi cha Ramadhaan. Si vyema kuanza kupaka rangi vibaraza visivyo na khayr wakati wagonjwa wapo nyuma ya mgongo wako. Kuna mengi ya kufanya ndugu zangu wa Kiislamu, haya ni manne tu, bado hujasoma Qur-aan, bado hujaswali Sunnah na hata bado hujahudhuria darsa. Huo muda wenzangu munaupata wapi wa kukaa kuangalia TV au kuketi vibarazani kufanya yaliyokatazwa na Uislamu? Tumukhofu Allaah wala tusilinganishe ghadhabu na adhabu Zake dhidi ya mtu yeyote.