Skip navigation.
Home kabah

Nani Muhammad Abdul-Wahhaab Na Kundi La Twariqa Ni Kundi Gani?

SWALI:

 Assalaleikum warahmatullah. Amma baad, ndugu katika iman ninafuraha zisizo na kifani kupata website ya dini kama hii ambayo itasaidia wengi ambao watakayo ithamini. Inshaallah Mwenyezi Mungu atawabariki wale waliofanya juhudi ya kuleta tuzo kama hii kwa ummati Muhammad s.a.w.

Swala langu ni kuhusu historia ya Muhammad ibn Abdulwahab r.a.nataka unieleze tarekh yake kwa jumla na huku alikozaliwa Najd  je ni ile nadj aliyoitaja Mtume (saw) kuwa ndiko alikotoka shetani?

Pili hili kundi la twarika ni kundi gani inafungamana vipi na mashia  au ithna shari? Na limetimbuka kutoka wapi?

 

 



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaana wa Ta'aala)   Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Shukrani kwa swali lako hili zuri ambalo kwayo baadhi ya watu wameona kuwa wamepata fursa ya kuweza kuwadharau na kuwatweza wanachuoni ambao wameipigania dini hii. Hakika watu ambao wanafuata matamanio yao wamempaka matope Shaykh huyu mwema na mtukufu.

Muhammad bin Abdul-Wahhaab ni MUJADDID (mwenye kukirejesha kitu kwenye upya wake) katika Dini yetu hii ya Kiislamu. Maana ya kujadidisha katika Dini ni kuyafufua upya mafundisho yaliyo fichika kwa kuwarejesha watu kwenye mafundisho sahihi yenyewe kama yalivyo.

Jina lake kamili ni Muhammad bin Abdul-Wahhaab bin Sulaymaan bin ‘Aliy bin Muhammad bin Ahmad bin Raashid at-Tamiymiy alizaliwa mwaka 1703 katika mji wa Uyaynah, Saudia. Alikuwa ni mtu mwenye akili kali sana hivyo kuweza kuhifadhi Qur-aan akiwa na umri wa miaka chini ya 10. Alisoma Fiqhi ya madhehebu ya Imaam Ahmad bin Hanbal akiwa mwanafunzi wa babake. Kuanzia ujana wake alivutiwa sana kusoma vitabu vya tafsiri na Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na vitabu vya Tawhiyd. Alivutiwa na kuathiriwa sana na vitabu vya Shaykh Ahmad bin Taymiyah na vya Ibn al-Qayyim. Alisafiri sana kwa ajili ya kutafuta ilimu.

Baada ya kusoma Uislam vizuri, Shaykh aligundua kuwa mambo mengi yanayofanywa na Waislam hayaambatani na mafunzo sahihi ya Uislam. aliona kuwa uharibifu huo uko kwao Najd na uko kila alipotembelea. Huo ni upotevu uliowapata Waislam kwa kuitakidi itikadi mbovu na kushikamana na ada chafu. Shaykh aliyaona maovu mengi na akachukulia kuwa ni wajibu wake wa kidini wa kujitolea na kusimama kinyume nayo kwa kubaini haki. Alipata misukosuko kwa sababu ya msimamo wake.

Alitumia mbinu mbali mbali ya kufanya kazi hiyo kama kuandika vitabu, barua, makala, kuwahutubia watu na kuweka halaqah za mafunzo na darasa kwa ajili ya kubaini Imani sahihi na ‘Ibaadah za kisawa. Allaah Alimpatia umri mrefu ulio tumiwa wote kwenye amali za kheri na kuitakasa Dini ya Kiislam na uchafu na mambo ya uzushi. Katika uhai wake aliwahi kuona matunda ya juhudi zake kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka katika sehemu tofauti. Aliaga dunia mwaka wa 1792. Alikufa kifo cha kawaida lakini ulinganizi wake ulibaki na kuwa ni ulinganizi wa haki wa kufuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) utaendelea kwa sababu nuru ya Uislam haizimiki.

Haya aliyoyafanyia bidii si kuwa alianzisha Dini mpya bali aliendeleza ile Dini ya Allaah Aliyetukuka iliyokamilishwa kupitia kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Msimamo wake ulikuwa ni Qur-aan na Sunnah, na kwa juhudi zake leo Waislam wengi wameweza kufungua macho na kuona haki.

Maadui kuanzia enzi zake walijaribu kulipaka matope na kuliharibu jina lake lakini walishindwa kwani Allaah Aliyetukuka hulinda waja wake wema. Jina lake litaendelea kutajwa kwa wema na tunamuombea Allaah Amrehemu na Amwingize Pepo ya al-Firdaws ya juu.

Najd ni hiyo hiyo ambayo ipo Hijaaz na ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuomba Allaah Aibariki.

Lakini katika Hadiyth ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliashiria kwa mkono wake kuwa atatoka shetani au pembe ya shetani, ishara hiyo kwa vitabu vyote inasemwa ni Iraq. Na hakika Iraq kama tulivyoona kwenye historian a hadi leo hii, kumetokea balaa nyingi na fitna nyingi kupita kiasi. Hata hivyo haiimanishi kuwa Iraq yote ina fitna, la! Kuna mazuri na historia kubwa ya Uislam na kuna wema wengi waliokuwa huko. Maelezo zaidi kuhusu Hadiyth hiyo ambayo Mashia wamezusha kuwa alikusudiwa Shaykh Muhammad, ina uchambuzi mpana mzuri kutoka kwa Maulamaa, na inshaAllaah itaandaliwa kwenye ALHIDAAYA.  Mashia kwa uovu wao mkubwa wanadai pia kuwa Mtume alipotaja Hadiyth hiyo aliashiria kwenye nyumba yake!!! Kweli Mtume ataashiria kuwa shetani anaweza kuwa katika ambalo leo hi ni kaburi lake (maana Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kazikwa nyumbani kwake). Allaah Awakhizi wote wenye kumtusi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wake zake na Maswahaba na wema wote.

Ni kawaida kuwa katika jamii wapo walio wazuri na wapo mashetani wa kibinadamu. Lakini unaposoma maisha ya Shaykh huyu tabia na maadili yake ni tofauti kabisa na shetani. Kawaida shetani anaamrisha mabaya lakini tunaona Shaykh alifanya juhudi kufufua Sunnah ambazo zilikuwa zimekufa na kupiga vita bid‘ah (uzushi) katika Dini hii yetu tukufu.

Kwa maelezo zaidi ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi ya historia yake na mengineyo yanayomuhusu:

 HISTORIA YA IMAAM MUHAMMAD 'ABDUL-WAHHAAB'

MAREKEBISHO YANAYOHUSIANA NA KUELEWA KIMAKOSA TARIYKH (HISTORIA) YA 'UWAHAABI'

UWAHABI: UFAFANUZI NA MAJIBU JUU YA MAJUNGU DHIDI YA SHAYKH MUHAMMAD 'ABDUL-WAHHAABf

Kundi hili la Twariqah ni kundi la KISUFI na ambalo wafuasi wake zaidi wanafuata matamanio ya nafsi zao kinyume na Uislam. Wanakuwa ni wenye kufanya mambo mengi ya uzushi na hata ushirikina. Kwa mfano ni watu ambao wanapenda sana Mawlidi, Khitmah, matanga na mengineo japokuwa katika mas-ala ya Ibaadah wanakuwa hawaonekani. Katika ushirikina ni kuwa wanawatukuza Mitume na mawalii kwa sifa za uungu au saa nyingine zaidi ya Mungu. Kisa kimoja ambacho kimeenea ni kile cha Shaykh ‘Abdul-Qaadir Jaylaaniy ambaye aliweza kurudisha roho za waliokufa siku moja kutoka kwa Malakul Mawt. Na malaika huyo alipokwenda mbele ya Allaah na jicho lake likiwa mkononi kwa kupigwa ngumi na ‘Abdul-Qaadir, (tunamuomba msamaha Allah kwa kunukuu hayo), lakini Allaah Aliyetukuka Alimwambia Malaika kwa nini hukumpatia roho hiyo moja aliyoitaka angalia sasa roho zote zimerudi uhai. Akaendelea Aliyetukuka kusema na kama angekuja huku kwetu basi angetuchafua sote, Naudhu Billahi!!! Na visa kama hivyo vimejaa sana kwenye vitabu vyao wanavyoandika Mashaykh wao.

Itikadi nyingi za watu wa Twarika zinafanana na Rawaafidh (MASHIA) Ithna ‘Asheri mbali nyengine ni mbaya zaidi. Allah Aliyetukuka Atuepushe na itikdai hizo. Wa kwanza katika kufuata na kueneza Twarika za Kisufi ni al-Husayn bin Mansuur anayejulikana zaidi kwa al-Hallaaj aliyezaliwa mwaka 244 H. huyu alikuwa na itikadi ya kwamba Allaah Hushukia ndani ya mwanadamu. Akaendelea kusema kuwa yeye na Mungu ni kimoja, yeye na Mungu ni roho mbili zilizoushukia mwili mmoja. Katika hayo alikuwa na beti za mashairi aliposema:

 

Mimi nimpendae naye ni mimi kwa kweli,

Sisi kwa atambuae ni roho mbili kwenye mwili mmoja.

Unaponiona basi umemuona,

Na unapomuona basi umetuona sote (wawili).

Mwengine aliyechupa mipaka katika itikadi mbaya ni Muhyid Diin Muhammad bin ‘Aliy bin Muhammad bin Ahmad bin ‘Abdallah ibn al-‘Arabiy aliyezaliwa mwaka 560 H. Madai yake makuu yalikuwa:

 

1.    Alidai “Wahdatul-Wujuud” yaani viumbe na Muumbaji ni kitu kimoja.

2.    Yeye hupokea ilimu yake moja kwa moja kutoka kwa Mwenyeezi Mungu.

3.    Alizua dini yake aliyoiita kwa jina “Dini ya Mapenzi”.

Hiyo ni kwamba yeye hapingani na dini yoyote wala hawachukii wafuasi wa dini yoyote.

Naye alikuwa na beti zisemazo:

   Umekuwa moyo wangu,                   Wakubali kila dini.

   Ya wana paa kwangu,                      Na kanisa la kasisi.

   Majumba ya masanamu,                  Na al-Ka‘bah dawamu.

   Na mbao za Taurati,                         Na msahafu wa Qur-aan.

   Dini niifuatayo,                                 Ya mapenzi yendapo.

   Ibadah yangu ni hiyo,                      Na Imani ipo hapo.

 

Ukiyapima haya utaona ni ukafiri mtupu, tunamuomba Allah Aliyetukuka Atulinde.

Na Allah Anajua zaidi