Skip navigation.
Home kabah

Kuna Maswahaba Waliokimbia Vitani Au Hao Ni Wale Wanafiki Walioahidiwa Adhabu?

SWALI:

Assalamu aleikum warahmatullahi taala wabarakaatuhu,niliwahi kusikia ktk darsa mbalimbali kuwa kuna maswahaba wengi ambao walikuwa si waislamu wa kweli kwa maana ya kuwa walikuwa wanafiqi, na hata ikafikia hatua ya baadhi yao kukimbia vitani jambo ambalo Mwenyezi Mungu Ameliweka wazi ktk Suratil-Ahzab, swali langu ni kutaka kujua hao maswahaba waliokimbia vitani ni akina nani, na ni katika vita gani walivyokimbia, naomba nisaidieni niwafahamu hao maswahaba waliokuwa wanafiqi kwani si wote walikuwa ni waislamu wa uhakika


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Maswahaba waliokimbia katika Vita. Awali ya yote tufahamu kuwa Swahaba ni yule mtu aliyekutana na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamuamini, akatekeleza ya Uislamu na akafa katika Imani. Wanafiki ni watu walioanza kuwa wafuasi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohamia Madiynah kwa maslahi yao ya kibinafsi na kumchimba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hawa walikuwa wakidhihirisha Imani lakini walikuwa maadui wakubwa wa Uislamu na Waislamu. Ni kwa ajili ya hiyo ndio Allaah Aliyetukuka Akaahidi kuwapatia adhabu kali kabisa na kuwaweka kuwa tabaka la chini katika Moto wa Jahanamu.

Pia tufahamu kuwa kukimbia vitani ni katika madhambi makubwa sana kwa Muislamu kufanya. Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) walikuwa msitari wa mbele katika kufuata yote waliyoambiwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili waweze kupata Pepo na kuridhiwa na Allaah Aliyetukuka. Kwa hivyo, si jambo ambalo lilifanywa na Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) wenye Imani thabiti na wasiokuwa na chembe ya nifaki.

Labda hapa tutoe mifano kuhusu hayo. Katika vita vya Uhud, inafahamika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka kwa ajili ya vita hivyo na Maswahaba elfu moja. Lakini kabla ya vita 'Abdullaah bin Ubayy bin Saluul, mkubwa wa wanafiki alitoa hoja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa anataka wapigane na maadui wakiwa Madiynah na kuwa rai hiyo haikuchukuliwa yeye na watu wake hawawezi kupigana. Kwa minajili hiyo, mnafiki huyo alirudi na wafuasi wake mia tatu (300) Madiynah, kumuacha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake 700. Yaliyotokea katika vita hivyo yanaeleweka vizuri sana kwani Waislamu walikuwa wanashinda lakini makosa yaliyofanywa na baadhi ya mujahidina yalifanya Waislamu wengi wawe ni wenye kuuliwa mpaka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa yuko hatarini. Uvumi ukatoka kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameuliwa, kwa uvumi huo baadhi ya Maswahaba wakaona hakuna haja ya kupigana tena na wengine wakaanza kurudi Madiynah lakini pindi habari thabiti zilipowafikia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yu hai walirudi ili kupigana tena.

Ama mfano mwengine ni katika Vita vya Ahzaab (makundi) ambapo wanafiki ndio waliomba ruhusa kuondoka katika vita hivyo ilhali mbali na shida kama anavyosema Allaah Aliyetukuka walibaki katika mapambano. Anasema Aliyetukuka:

"Walipokujieni kutoka juu yenu na kutoka chini yenu; na macho yalipokodoka na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkaanza kumdhania Allaah dhana mbali mbali" (33: 10).

Mbali na mtihani huo Waislamu walisimama imara,

"Hapo Waislamu walitiwa mtihani na wakatetemeshwa kwa matetemesho makali" (33: 11).

Lakini wanafiki walisema yafuatayo:

"Na taifa moja miongoni mwao liliposema: 'Enyi wenyeji wa Yathrib (Madiynah)! Hamna mahali pa kukaa nyinyi, basi rudini makwenu'. Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Mtume kwa kusema: 'Hakika nyumba zetu ni tupu (hazina watu)', lakini hazikuwa tupu, hawakutaka ila kukimbia tu" (33: 13).

Mfano mwengine ni katika vita vya Mu'tah ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwachagua majemadari watatu waongoze mmoja baada ya mwengine. Nao ni Zayd bin al-Haarithah, Ja'far bin Abi Twaalib na 'Abdallaah bin Rawaahah (Radhiya Allaahu 'anhum). Katika vita hivyo Waislamu walikuwa ni elfu tatu (3,000) dhidi ya Warumi laki moja (100,000). Majemadari wote watatu waliuliwa, na ujemadari ukashikwa na Khaalid bin al-Waliyd (Radhiya Allaahu 'anhu). Mbali na vita kuwa vikali siku hiyo Waislamu waliweza kusimama imara. Usiku wake Khaalid aliweka Shuura kuzungumzia suala hilo na ikaonekana kuwa Waislamu wawe ni wenye kuweka stratejia ya kuwatisha maadui zao kwa kupigana na kurudi nyuma pole pole. Siku ya pili wakafanya hivyo kuwatisha Warumi wasiweze kuwafuata wakiona kuwa labda hiyo ni stratejia ya kupata usaidizi kutoka kwa wenziwao hivyo wasiweze kuwafuata. Waliporudi Madiynah waliokuwepo mjini walianza kuwalaumu kwa kufanya hivyo, lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa Waislamu hao hawakukimbia bali watakutana tena na Warumi na watawashinda.

Na Allaah Anajua zaidi