Wanawake Kuhudhuria Mazishi Makaburini
SWALI:
Assalam alaikum, mimi nawa andikia nikiwa mgeni katika dini hiyi ya ALLAAH ninayo mswali ambayo ningelipenda kujua majibu yake kwani yatachangia kuniweka sawa na kuifuata vyema dini ya ALLAAH.
SABABU GANI WANAWAKE WA KI ISLAMU HAWARUHUSIWI KUHUDHURIA MAZISHI HUKO MAKABURINI? (YAANI KWENDA KUZIKA)
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kama tunavyokariri kusema kuwa Uislamu ni njia kamili ya maisha ya mwanadamu akiwa hapa duniani. Na miongoni mwa agizo ni la kufuata jeneza kwa wanaume. Katika Uislamu, mwanaume na mwanamke wanasaidia katika kutekeleza majukumu. Hivyo, katika suala hili wanaume wameruhusiwa kufuata jeneza mpaka makaburini na wanawake wamekatazwa. Katazo hilo ni kulingana na Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyyah (Radhiya Allaahu ‘Anha) ambaye amesema: “Tumekatazwa kufuata jeneza” (al-Bukhaariy na Muslim). Hakika ni kuwa wanawake wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuwa ni wenye kufuata jeneza.
Hivyo kufuata agizo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni wajibu wetu kwa kauli ya Aliyetukuka: “Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho” (59: 7).
Ama baada ya maiti kuzikwa inapendeza kwa Waislamu kuwa ni wenye kuzuru makaburi ili kuwaombea dua maiti na pia maghfira. Hiyo ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Nilikuwa nimewakatazeni kuzuru makaburi lakini sasa yazuruni kwani yanawakumbusha Akhera” (Muslim). Lakini kukithiri kwa mwanamke kuzuru makaburi kumekatazwa kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Allaah Amemlaani mwanamke mwenye kuzuru sana makaburi” (al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad).
Mbali na ruhusa hii kwa wanawake kuzuru makaburi wanatakiwa wasiwe ni wenye kutenda mambo mabaya kama vile kuomboleza makaburini au kupiga kelele au kutoka pasi na nguo za heshima au kumuita maiti na kumuommba awatatulie shida zao na mengineyo. Ni hakika isiyokanika kuwa mioyo ya wanawake ni dhaifu sana na hata subira zao ni chache. Kwa hiyo, wanapozuru wanafaa wachunge hayo na ikiwa hawawezi basi ni afadhali wakae majumbani mwao.
Na Allaah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


