Tenda Mema Usahau
Gufraanah Ibraahiym Siwa
Alifu hapa naanza, kwa kumuomba Manani,
Ni Yeye ndio Muweza, kila kitu duniani,
Hakuna Wakumweza, kwa hilo ninaamini,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Tenda wema wende zako, usingoje shukurani,
Yalo mema ya wenzako, yazingatie moyoni,
Usitaje mema yako, kwa fakhari duniani,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Asojuwa ya wenziwe, yafaa kutafakari,
Ajuwe yake mwenyewe, ya kheri au ya shari,
Duaze zikubaliwe, na Mungu Amsitiri,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Swala tano ni ibada, lazima kuzingatia,
Utapoteza faida, swala kutozingatia,
Uingie kwenye shida, matatizo ya dunia,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Wengi wanaziepuka, kwa mambo ya kidunia,
Kuziqimu ni hakika, wakati ukiwadia,
Usichelewe dakika, adhana ukisikia,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Msikiti twaipita, ndani watu wanaswali,
Nafasi tunazipata, na wengine hawaswali,
Njiani utawakuta, wamo katika shughuli,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
Mtandao umetanda, kwa masomo mbalimbali,
Fungua unapopenda, chemsha yako akili,
Tovuti yenye faida, Alhidaaya asili,
Tenda wema usahau, usingoje shukurani.
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha


