Skip navigation.
Home kabah

Tafsiyr Ya Suratul-'Aswr

 

 


Imekusanywa Na:Ummu Iyyaad

 

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمنِ الرَّحيم

((وَالْعَصْرِ))   

 ((إِنَّ الإِ نسَانَ لَفِي خُسْرٍ))    

 ((إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا)) 

 

KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU

((Naapa kwa Zama!))  

((Hakika binaadamu bila ya shaka yumo katika khasara))  

((Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri)) [All-'Aswr:1-3]

 

UMUHIMU NA MAELEZO YA MWANZO KUHUSU

SURATUL ‘ASRW

1.     Ni katika  Surah za mwanzo kabisa ziloteremka Makkah.  

2.     Ni mojawapo wa Surah ndogo kabisa yenye Aayah tatu tu na nyinginezo ni Suratul-Kawthar na Suratun-Naswr, kwa hiyo jumla zote pia ni tatu.  

3.      Surah hii imeelezea shuruti zote ambazo Muumba wetu   Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Amezitoa kama ni fardhi na wajibu ili aweze mtu kuridhiwa na Muumba wake na kufaulu atakaporudia Kwake (yaani Akhera).

Shuruti zenyewe ni  nne kama ifuatavyo:

·        Kuamini                         

·        Kutenda vitendo vyema

·        Kuusiana kwa haki        

·        Kuusiana kusubiri

Shuruti zote  ni lazima kuzitimiza ili kufaulu Akhera.    

Mfano wake ni kama mfanya kazi na bosi wake kazini.  Ingawa  mfanya kazi huyo anaweza kuwa ni  hodari kabisa kuliko wote,  au mwenye juhudi ya kazi kabisa kuliko wote,  lakini   wakati bosi wake alipomtuma kazi nne akashindwa  kutimiza moja au mbili  basi bila ya shaka hakumfurahisha bosi wake, na pengine apunguziwe mshahara au afukuzwe kazi. 

Ni sawa na Muislamu, japo kuwa anaswali Swalah tano  lakini madamu hafanyi mengine aliyoamrishwa na Mola wake hatokua amemridhisha Mola wake.

4.     Ingawa ni Surah ndogo lakini yaliyomo ndani yake ni muhimu na mazito sana.  Ni Surah nzito  yenye maana ya ndani kabisa na ni msingi unaohusu kupasi au kufaulu Akhera.    

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema katika  Surat Huud

  ((بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ))

((الَر كِتَابٌ أُحْكِمَتْ آيَاتُهُ ثُمَّ فُصِّلَتْ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ خَبِيرٍ))   

((Alif Laam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aayah zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilichotoka kwa Mwenye Hikma na Mwenye Khabari))  [Huud 11:1]

 Kwa hiyo Suratul ‘Aswr ni  Surah   ambayo Aayah zake zimewekwa wazi kwa hikma ya juu kisha zinajichambua au  zinajielezea  zaidi kwa urefu katika Surah  nyingine, kama vile vile Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  katika Suratul-'Imraan:

 ((هُوَ الَّذِيَ أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ...  

((Yeye Ndiye Aliyekuteremshia Kitabu (hiki Quraan) Ndani yake zimo Aayah muhkam (nyepesi kufahamika)  ambazo ndizo msingi  (asili) wa kitabu na ziko nyingine mutashaabihaat ... (zilizofanana) )) [Al-Imraan:7]

Mfano vile vile kama Suratul-Faatiha au Suratul-Ikhlaasw..

Surah Nzito kabisa ambayo ni msingi  katika mafundisho ya imaan ni Suratul-Faatiha. 

Surah nzito kabisa ambayo ni  msingi  katika mafundisho ya  Tawhiyd ni Suratul-Ikhlaasw.

 

كان الرجلان من أصحاب رسول الله صلى الله عليه وآله وسلم إذا التقيا لم يتفرقا حتى يقرأ أحدهما على الآخر سورة والعصر

 ثم يسلم أحدهما على الآخر

 (Walikuwa masahaba wawili kila wanapokutana hawaachani ila baada ya                  kusomeana Suratul 'Al-ِِِAswr ikisha ndio wanaagana ) [At-Twabarani na Bayhaaqiy] 

Ingawa  Surah nyingine kama Suratul-Ikhlaasw   au Suratul-Faatiha ni zenye daraja ya juu  lakini maswahaba walikuwa wakikumbushana  Surah hii. 

Nini faida waliyokuwa wakiipata maswahaba  kukumbushana Surah hii?

Jibu ni kuwa :

 Kwa sababu ya kukumbushana  na kutanabahishana daima  kuwa bila ya kutimiza maamrisho yaliyomo ndani ya Surah hii hawatafaulu au watakuwa waliokuwa katika hasara.   

Imaam Shaafi'iy (Rahimahu-Llah)  kasema mambo mawili mazito  kuhusu Surah hii:

 

 " لو لم ينزل الله سوى هذه السورة لكفت الناس"

Kama isingeliteremshwa Surah nyingine ila hii ingeliwatosheleza watu.

  " لو تدبر الناس هذه السورة لوسعتهم" ) أي لكفتهم (.

Watu wangelizingatia Surah hii maana yake ingeliwatosha  kufaulu Akhera

Tunafahamu kwa usemi huo kuwa ni hidaaya (uongofu) kamili kwa watu wote Waislamu na wasio Waislamu.

5.      Lugha ya Surah hii ni nyepesi kabisa, Bedui yeyote aliweza kuifahamu bila ya tabu. Na hata kwetu pia baadhi ya maneno  ni mepesi kufahamu hata kama mtu hajui lugha ya Kiarabu kwani yamefanana na lugha yetu (kama ya Kiswahili)

6.       Ingawa Surah hii ina Aayah tatu lakini, kwa hakika ni kama Aayah moja tu kwa vile kuzisoma zote ndio kunaleta maana kamili.

  ((وَالْعَصْرِ))  

         ))Naapa kwa zama))

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Anaapa kwa zama.  (maelezo ya maana hii utayapata  chini ya makala hii)  

Neno hilo moja halitoshi kumpa mtu fahamu ya makusudio. Yaani  baada ya kuapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Je!  Anaapa kwa zama gani?  Anaapa kutuelezea nini?  

Kama Anavyoapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Surah nyingine zinazoanzia kwa:

وَالسَّمَاء وَالطَّارِقِ   -  وَالْفَجْرِ   -  وَالشَّمْس    - وَاللَّيْلِ  -   وَالضُّحَى   -   وَالتِّينِ وَالزَّيْتُونِ

((Wassammai Wat-Twaariq – Walfajr – Washamsi – Wallayl – Wadhwuhaa – Wattiyn Wazzaytuun))    

Katika Surah zote hizo Alizoziapia Anatoa maelezo baada ya viapo hivyo na hali kadhalika katika Surah hii Ameelezea kiapo hicho.

 ((إِنَّ الإِ نسَانَ لَفِي خُسْرٍ))   

   ((Hakika binaadamu bila ya shaka  yuko katika hasara)) 

Binaadamu yuko kwenye hasara? Vile vile utaona kuwa haikuleta maana kamili. Yuko kwenye hasara gani?  Kwa kufanya kitendo gani au kwa kutokufanya kitendo gani?  Lazima kuna maelezo zaidi kutujulisha sababu ya kuwa yuko kwenye hasara.  

Ukisoma Aayah ya tatu ndio utajua kuwa kumbe sio wote waliokuwa  katika hasara  kwani Aayah  inasema “ila" au "ispokuwa “ :

 ((إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ))  

 ((Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri))

Hapa sasa ndio tumepata maana   kamili ya Aayah hizi tatu   

TAFSIYR  NA MAELEZO ZAIDI SURAHH HII

  ((وَالْعَصْرِ  ))

((Naapa kwa zama)) 

Zama gani?    

1-Baadhi ya Wafasiri wa Qur-aan  wamesema kuwa ni wakati wa Alasiri

2-Baadhi yao wamesema kuwa ni wakati tokea Nabii Muhammad  (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   mpaka mwisho wa dunia.

3-Na baadhi yao wamesema kuwa ni zama au nyakati  tokea mwanzo wa  kuumbika binaadamu mpaka mwisho wa dunia 

Wakati  au zama kawaida  ni za aina tatu:

Wakati uliopita. 

Wakati tuliokuwepo sasa. 

Wakati utakaokuja baada yetu.   

Kutokana na rai ya  tatu ya Wafasiri wa Qur-aan,  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Anaapa  kama ni ushahidi wa viumbe vyote tokea Adam ('alayhis-salaam)  mpaka mwisho  wa dunia, yaani watashuhudia watu wa nyakati zote hizo tatu; waliotutangulia, tulioko bado duniani na watakaokuja baada  yetu kwamba: 

((إِنَّ الإِ نسَانَ لَفِي خُسْرٍ))    ((إِلاَّ ... ))

((Hakika binaadamu bila ya shaka  yuko katika hasara)) ((Isipokuwa…)  

Kwa hiyo wakati unaendelea tu  na utakwisha tu  kama si mauti basi ni Qiyaamah.  Na kama mfano moyo wetu unavyodunda  mpaka utakaposita kudunda .      

Wale walioondoka duniani  na watakaoondoka  ndio watakokuwa aidha katika hasara  au wamefaulu kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)       

((إِلاَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ))

((Ila wale walioamini, na wakatenda mema, na wakausiana kwa haki, na wakausiana kusubiri))

Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    “ila wale walioamani na wakatenda mema ……..)  

Mfano vile kama darasani Mwalimu akisema “Wanafunzi wote wamefeli mtihani, isipokuwa wale wanafunzi  waliokuwa wakija kusoma zaidi jioni hapa shuleni".  (Yaani wale waliofanya juhudi zaidi ya kuja kusoma)

Kisha Surah imetupa  masharti ya kufaulu akhera.  Watu wengi wanafikiria kuwa kufaulu  ni  kuwa na mali, au elimu ya juu, au cheo kikubwa  na mengi mengineyo.  Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatupa hasa maana au shuruti  za kufaulu duniani na akhera.

Tukiamini  maneno haya ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    basi matamanio ya  dunia  hayatokuwa muhimu kwetu bali tutataka kuwa na imaan, na kufanya vitendo vyema na kuusiana kwa  haki na kuusiana  kwa subira ili tupate kufaulu huko.

Ukiangalia mfano wa Fir'awn  au Qaaruun waliomiliki vyeo na  mali nyingi duniani,  lakini   kama tunavyojua Fir'awn kaangamizwa baharini na Qaaruun kaangamizwa kwa kudidimwiza ardhini. Kwa hiyo wote hawakufaulu bali wamekuwa waliopata hasara kubwa.    

Kinyume chao ni  mfano kama Bilaal (Radhiya Allahu 'anhu)   au  maswahaba  wengine waliokuwa masikini lakini  Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam  aliwabashiria kuwa watu wa kufaulu  Akhera.  

Kukubali kwa kusoma Aayah za Surah hii na kuamini hizi shuruti zilokuwemo ni rahisi lakini  kuzitimiza ni vigumu   kutokana na  fitna  za dunia.    Ndio maana maswahaba walikuwa hawaachi  kukumbushana Surah hii ili wajiepushe  na kujikinga na  fitna.   

Na kwetu sisi ndio tunahitaji zaidi kukumbushana kwa vile fitna za dunia zinazidi na kuzidi. Na kukumbushana huku kila mara na kuzitekeleza shuruti hizo ndio tutaweza kufaulu  hatutakuwa katika hasara duniani wala Akhera. 

Lakini ni lazima kuzitimiza shuruti zote nne kama Alivyoziweka Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani kila neno katika Qur-aan lazima lichukuliwe kwa makini,  yote ni haki,   wala Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Hakuweka hata  herufi moja katika Qur-aan ila ina maana yake. Na hakuna yeyote anayeruhusiwa  kupunguza au kuongeza hata herufi moja.  

Shuruti zote hizo zinaweza  kuwa na daraja mbali mbali, mfano :

·  Imaan, kuna watu ambao imani zao ni kamili za  dhati, kuna wengine imaan zao ni  kiasi tu .

·   Kufanya vitendo vyema, wengine watumie wakati wote kuwa katika vitendo vyema tu, na wengine mara wafanye mara wasifanye.    

·  Kuusiana katika kufanya haki, wengine wafanye kazi hii kwa juhudi kubwa ya kutumia wasila mbali mbali na wengine wafanye kwa watu wachache tu.  

·   Subira, wengine wanaweza kuvumilia mitihani hata mikubwa, na wengine japo wanayo subira lakini katika mitihani mingine huenda wakawa dhaifu kidogo kusubiri. 

Ijapokuwa yote hayo yana daraja zake, lakini kutimiza yote ni lazima ili kupata kufaulu na kutokuwa katika hasara.

Mfano kama mgonjwa  aliyekwenda kwa  daktari  akamuandikia dawa nne kutibu maradhi yake.  Yule mgonjwa  akaona atumie dawa tatu na aache moja labda hiyo moja ilikuwa chungu mno!    Lakini kumbe  ile moja aliyoiacha kutumia  ni ya kumsaidia kuondosha dhara  ya dawa mojawapo ya zile tatu na kwa vile yeye hakuitumia, hakuweza kupata matibabu  sawa sawa.  Kwa hiyo aidha atumie zote nne au aziache abakie na maradhi yake.    Na hivi ndivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Alivyotupa shuruti  hizi nne  zote kuzitimiza  ili kufaulu, yaani ikiwa moja imepunguka basi hajafaulu mtu.

Imaam Ar-Raazi (RahimahuLLah)  alisema maneno mazito kuhusu Aayah hizi za Suratul ‘Aswr :

 إعلم ان هذه الأيات  فيها وعيد شديد لأن الله حكم بالخسارة على جميع الناس إلا من كان آتياً بأشياء أربعة أو متصفاً بصفات أربع وهي : الإيمان ، والعمل الصالح،  والتواصي بالحق والتواصي بالصبر . فدل ذلك على أن النجاة معلقة بمجموع هذه الأمور

"Tambua kwamba Aayah hizi zina maonyo makali kwani  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametoa hukumu kuwa binaadamu  wote wako katika hasara ila atakayetekeleza mambo haya manne  au atakayekuwa na sifa nne nazo ni;  (1) kuamini,  (2) kufanya vitendo vyema (3) kuusiana   na  hakki na (4)  kuusiana   na kusubiri.  Akaonyesha kuwa kufaulu kunaambatana  na mambo yote hayo"

Kwa hiyo ni onyo kali kutoka kwa  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  ni lazima shuruti  zote nne zitekelezwe kama ifuatavyo:  

1.     KUAMINI

Kuamini hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Amekusudia aina mbili.

· Kuamini dini ya mwisho ya kiislamu na Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Yaani kukiri kuwa

أِشْهَدُ أَن لاَ إِلَهَ إلاَّ اللَّه وَ أشْهَدُ أنَّ  مُحَمَّدٌ رَسُولُ اللَّه

“Nakiri kwa moyo na kutamka kwa ulimi kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mjumbe Wake”  

   .     Hii  inawahusu  Waislamu wote.

 Kuwa na imaan baada ya kuwa Muislamu kwa sababu haiwezi kuwa mtu mwenye imaan  ya kweli akawa hamtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama tullivyoamrishwa katika Qur-aan na katika Sunnah. Au   hafanyi vitendo vyema. Kwa hiyo mtu atakuwa katika hali ya Uislamu tu na sie aliyeamini mpaka  imani iingie kwenye moyo wake amtii Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    pamoja na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na atende vitendo vyema hapo ndipo atakapkuwa kaamini khaswa kama alivyotueleza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   katika Suratul Hujuraat .

 قَالَتِ الْأَعْرَابُ آمَنَّا قُل لَّمْ تُؤْمِنُوا وَلَكِن قُولُوا أَسْلَمْنَا وَلَمَّا يَدْخُلِ الْإِيمَانُ فِي قُلُوبِكُمْ وَإِن تُطِيعُوا اللَّهَ وَرَسُولَهُ لَا يَلِتْكُم مِّنْ أَعْمَالِكُمْ شَيْئًا إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ لَمْ يَرْتَابُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّهِ أُوْلَئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

((Mabedui wamesema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu. Na mkimtii  Allah na Mtume Wake, Hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu. Hakika Allah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) 

((Hakika Waumini ni wale waliomuamini Allah na Mtume Wake tena wasitie shaka kabisa, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Allah kwa mali yao na nafsi zao. Hao ndio wakweli)) [Suratul-Hujuraat:14-15]

2.     KUFANYA VITENDO VYEMA

 ((وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ))

Vitendo vyote vyema mbali ya vile vya fardhi,  kama sadaqa, kufunga Swawn za Sunnah, Swalah za Sunna, kutii wazazi,  kusaidia wahitaji kwa njia mbali mbali, kupatanisha watu, kufundisha watu, wema na majirani, na mengi sana mengineyo hata dogo vipi kama mfano kuokota kitu cha dhara njiani  au kumwambia mwenzako tamko zuri. 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   kila mara katika Quraan Analeta Aayah inayosema :

((إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ

(([Wale walioamini na kufanya vitendo vizuri] 

  

3.              KUUSIANA KATIKA HAKI

((وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ))    

Muislamu  anapoona jambo lolote baya lilokuwa sio katika sheria ya Kiislam basi ni wajibu wake  kulisawazisha  na kujaribu kulibadilisha.    

Lakini ni muhimu sana katika kusawazisha huko kutumia hikma  na mawaidha mema kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):         

((ادْعُ إِلِى سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ))

(([Waite  (watu) katika njia ya Mola wako kwa hikma na mauidha mema na ujadiliane nao kwa namna iliyo  bora)) [An-Nahl:125]

Mfano kama rafiki yako haendi mwendo mzuri wa Kiislam   labda haswali au labda  mavazi yake zio mazuri,   anza kwa kumsifia  na kuusifu urafiki wenu na kuomba kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) muendelee urafiki,  na kuwa unaogopa kuwa unalotaka kumnasihi asije kukasirika,  na kwamba unamwambia kwa kumtakia kheri sio shari. Yaani upake mafuta urafiki kwanza.

Hapa tujue kuwa ukweli ni mchungu,  si rahisi kuwa mara moja mtu anakubali kupewa nasiha. Ni jambo gumu sana!   Lakini kwa sababu ni wajibu wetu kupeana nasiha  kama  ilivyo sharti mojawapo ya kufaulu Akhera katika Surah hii basi lazima tuitekeleze.

Vile vile kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Anavyotueleza  kuwa sisi ni Umma bora. Kazi yetu ni kuamrishana mema na kukatazana mabaya,  basi inabidi tu   tuifanye kazi hii na kuwa tayari kusubiri mithinai itakayotusibu kutokana na kazi hizi za daawa.

((كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللّهِ))

((Nyinyi ndio umma bora kuliko umma zilizodhihirishiwa watu, mnaamrisha yaliyo mema na mnakataza yaliyo maovu na mnamuamini Allaah] [Al-'Imraan: 110]

Vile vile  Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katufundisha kuwa tunapoona jambo baya la kuchukiza katika dini basi ni wajibu kulikataza na ndiyo dalili ya Imaan

عَنْ أبيِ سَعِيدٍ الْخُذْرِيٍّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ :   سَمِعْتُ رَسُولُ اللّهِ صلي الله عليه وآله وسلم يَقُولُ :((مَنْ رَأَى مِنْكُمْ مُنْكَراً فَلْيُغَيِّرْهُ  بِيَدِهِ ، فَإنْ  لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِلِسَانِه، فإنْ لَمْ يَسْتَطِعْ فَبِقَلْبِه، وَذَلِكَ أَضْعَفُ الإْيمَان )) 

 رَوَاهُ مُسْلِم

Kutoka   kwa Abi Sa'iydil-Khudhriyyi (Radhiya Allahu 'anhu)  kasema kuwa: "Nimemsikia Mjumbe wa Allaah Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   anasema:  ((Atakayeona katika nyinyi maovu basi aybadilishe kwa mkono wake, kama hakuweza basi kwa ulimi wake na kama hakuweza basi  kwa moyo wake (yaani achukie lile ovu)  na hiyo ni imani ndogo kabisa)) [Muslim]

 

4.     KUUSIANA KUWA NA  SUBIRA

((وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ))

Baada ya kufanya kazi hiyo ya kuamrisha mema na kukataza maovu, ukae tayari kupata mitihani, misukosuko, machungu  ya aina mbali mbali.   Pengine upoteze urafiki  wako na rafiki yako mpenzi  au kama ni kubadilisha maovu  yanayotendekana na  jamaa wengi katika mji au kijiji basi pengine wakukatae na wakufukuze mji. 

Au pengine  mwenye kufanya kazi hiyo ya daawa iwe kwamba hapo zamani hakuwa katika mwendo mzuri, kisha akapata uongofu  na akapenda kuwanasihi wenzake, basi hapo atakumbushwa maovu yake ya  mwanzo ili avunjike moyo na apate uchungu.  

Na machungu ya aina mbali mbali mengineyo yatamfika hata kama alikuwa hana aibu yoyote hapo mwanzo. 

Na mifano bora tunayo kutokana na visa vya Mitume waliofanya daawa kuwaita watu katika dini ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), waliofikwa na tabu na  maudhi  makubwa makubwa.  

Basi subira ni lazima katika daawa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Asije mtu akavunjikwa moyo akaacha kufanya nasaha  kwa watu  au kuendelea kubadilisha mabaya anayoyaona. Aendelee tu kufanya kazi ya Allaah  atalipwa malipo mazuri kabisa Aakhera.  Hakuna kizuri kinachopatikana kwa urahisi.  

Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Alijua ugumu wa jambo hili ndio maana akaunga baada ya  kuusiana  kwa haki na kuusiana kwa subira  

   وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ  وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ    

Luqumaan alipompa nasaha mwanawe kuhusu kuamrisha mema na kukataza mabaya pia alimgusia jambo hilo la subira .

 

(( يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَى مَا أَصَابَكَ إِنَّ ذَلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُور))

 ((Ewe mwanangu!  Simamisha Swalah na uamrishe mema, na ukataze mabaya na usubiri   ju ya yale yatakayokusibu hakika haya ni katika mambo yanayostahili kuazimiwa)) [Luqmaan: 17] 

 

أللهم اجعلنا من الذين آمنوا وعملوا الصلحات وتواصو بالحق وتواصو بالصبر – ِأمين    .

Ya Allaah, Tujaaliye tuwe katika wale waliomini na kutenda vitendo vyema na kuusiana kutenda  haki na kuusiana kuwa na subira.  Aamiyn.  

 

 Naomba radhi kama kutakuwa na makosa yoyote ya kilugha au tahajia