05-Jihaad: Wajibu Wa Viongozi Wa Jeshi

 

Wajibu Wa Viongozi Wa Jeshi

 

Yafuatayo ni mambo anayowajibika kuwa nayo kiongozi wa jeshi.

 

1.     Kushauriana na wenzake na kutaka rai zao, na asiwe akijiamulia bila kuwashauri, na hii inatokana na kauli ya Allaah Aliposema;

“Na shauriana nao katika mambo.”

Al-‘Imraan: 159

 

Na kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Sijapata kumuona mtu anayependa kutaka ushauri wa Maswahaba wake kupita Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).”

Imam Ahmad na Imam Ash-Shaafi’iy (Radhiya Allaahu ‘anhu).

 

2.     Upole na kuwarahisishia mambo. Anasema Mama ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha):

“Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Yeyote atakayepewa uongozi wa umma wangu basi awe mpole juu yao, awe mpole juu yao.”

 

Na imepokelewa kutoka kwa Mu’aqal bin Yasar kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Hapana amiri yeyote aliyepewa uongozi juu ya Waislamu, kisha asijitahidi juu yao (katika kuwa mpole kwao na katika kuwatafutia manufaa) wala asiwanasihi, (kwa kuwaamrisha mema na kuwakataza mabaya) isipokuwa hatoingia Peponi.”

 

Na amesimulia Abu Daawuud kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akirudi nyuma katika misafara kwa ajili ya kuwasaidia walio dhaifu (kwa kuwashika mikono au kushika hatamu za wanyama wao na kuwatanguliza mbele ili wawe pamoja na wenzao), na kuwapakia juu ya ngamia (wake na wa wengine wendao kwa miguu).”

 

3.     Kuamrisha mema na kukataza maovu ili watu waepukane na kumuasi Allaah.

 

4.     Kulikagua jeshi mara kwa mara apate kuwajuwa vizuri askari wake, na kuwajuwa wale wanaowavunja moyo wenzao wasitake kwenda vitani, na wale wanaosababisha choko choko katika jeshi, kwa kusema kwa mfano; ‘hatuna silaha za kutosha wala nguvu za kutosha.’ Na pia apate kuwajuwa wale wanaotoa siri za jeshi.

 

5.     Kupashana habari na viongozi.

 

6.     Kuchaguwa sehemu zinazofaa kwa ajili ya kupiga kambi.

 

7.     Kutuma wapelelezi kwa ajili ya kujuwa hali za adui.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapotaka kushambulia mahali akiwababaisha adui kwa kuwajulisha kama kwamba anataka kushambulia mahali pengine.

Alikuwa pia akiwatuma wapelelezi wamletee habari za adui, na alikuwa akilipanga vizuri jeshi lake.

 

Amesema Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu):

“Bendera ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ilikuwa nyeusi na ya jeshi ilikuwa nyeupe.”

Abu Daawuud

 

 

 

Usia Kwa Viongozi

 

Kutoka kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa anapompa uongozi yeyote katika Maswahaba wake katika baadhi ya mambo alikuwa akimwambia:

“Wapeni watu bishara njema (juu ya rehma ya Allaah na kusamehe kwake) wala miswape habari za kuwachukiza (kwa kuwatisha na kuwaogopesha), na mambo muyafanye (yawe) mepesi, msiyafanye (yakawa) magumu.”

 

Na pia kutoka kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

“Alinituma Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mimi na Muadh kwenda Yemen akasema:

“Wepesisheni mambo wala msifanye yakawa magumu, wapeni watu bishara njema wala miswape habari za kuwachukiza, wahiyarisheni, na msikhitilafiane.”

Al-Bukhaariy na Muslim

 

Kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Nendeni kwa jina la Allaah, na kwa ajili ya Allaah, na kwa kufuata mwenendo wa Mtume wa Allaah, wala msimuuwe mzee mkongwe, wala mtoto mdogo, wala mwanamke (ila kama ni mwanajeshi), wala msiendeane kinyume katika ngawira, na mchange pamoja ngawira zenu, na mtengeneze na mfanye mema kwa sababu Allaah anawapenda watendao mema.”

Abu Daawuud

 

 

Usia wa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)

 

‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwandikia Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) na askari wake wengine akiwausia yafuatayo;:

“Amma baad - Mimi nakuamrisha wewe pamoja na askari ulio nao kumcha Allaah katika kila jambo, kwa sababu kumcha Mungu ni silaha bora kupita zote mbele ya adui, na ni mbinu yenye nguvu kupita zote kati vita. Na nakuamrisha wewe pamoja na ulio nao mchunge msije kufanya maasi kuliko mnavyomchunga adui yenu, kwa sababu madhambi ya wanajeshi yana hatari zaidi juu yao kupita adui wao. Kwa hakika Allaah huwapa ushindi Waislamu kwa sababu maadui ni watu wenye kumuasi Allaah, ama sivyo sisi hatuna nguvu za kuwashinda, kwa sababu idadi yao ni kubwa kuliko idadi yetu, na silaha zao ni kali kupita silaha zetu. Kwa hivyo tukiwa sawa nao katika kufanya maasi, basi wao watatushinda kwa nguvu zao, kwa sababu tunapewa ushindi kutokana na fadhila zetu na si kwa nguvu zetu.

Na mjuwe kuwa katika msafara wenu mna (Malaika) wenye kuhifadhi wanaojuwa kila mnalotenda, kwa hivyo muwaonee haya, na msiwe wenye kumuasi Allaah mkiwa katika njia ya Allaah, na wala msiseme kuwa; ‘Kwa vile adui wetu wana shari kupita sisi kwa hivyo hawataweza kupewa ushindi juu yetu,’ kwani huenda watu wakasalatishiwa (wakapelekewa) na kushindwa na adui aliye mbaya kupita wao kama pale Bani Israil walipomuasi Allaah akawapelekea Majusi (wanaoabudi moto) wakaingia mijini mwao kila upande, ikawa ahadi iliyoyotimizwa.

Muombeni Allaah akusaidieni katika nafsi zenu kama mnavyomuomba akupeni ushindi juu ya adui yenu, namuomba Allaah anipe mimi na nyinyi yote hayo.

Na kuweni wapole kwa Waislamu katika mwenendo wao wala msiwakalifishe mambo mazito yatakayowataabisha.”

 

 

 

Du’aa Wakati Wa Mapambano

 

Mpigana Jihaad anatakiwa amuombe Allaah ampe ushindi kwa sababu ushindi umo mikononi mwake Subhanahu wa Taala, na huu ndio uliokuwa mwenendo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na mwenendo wa Masahaba baada yake (Radhiya Allaahu ‘‘anhum).

Kutoka kwa Abu Daawuud kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Mawili hayarudi patupu; Dua baada ya muadhini, na (du’aa) katika vita pale wapiganaji wanapovamiana.”

 

Allaah Amesema:

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

“(Kumbukeni) mlipokuwa mkiomba msaada kwa Mola wenu, naye akakujibuni.”

Al-Anfaal: 9

 

Imepokelewa kutoka kwa (Maimamu) watatu (wa elimu ya hadithi) kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi ‘Aufiy kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika siku mojawapo alipokuwa akiwasubiri maadui, alisubiri mpaka wakati wa zawal (kidogo baada ya adhuhuri), kisha akasimama kuwahutubia watu akasema:

“Enyi watu! Msitamani kukutana na adui, na muombeni Allaah usalama, na mtakapokutana naye (adui) basi muwe wenye subira (wavumilivu) na jueni kuwa Pepo ipo chini ya vivuli vya panga.”

 

Kisha akasema:

“Mola wangu uliyekiteremsha kitabu, mwenye kuyasukuma mawingu, uliyewashinda makundi (katika vita vya Ahzaab), washinde na utupe ushindi juu yao.”

 

Na katika du’aa zake wakati wa vita (alikuwa akisema):

“Mola wangu wewe ndiye msaidizi wangu na unipaye ushindi, kwako naelekea na nategemea na kwa ajili yako napigana vita.”

Imepokelewa na Maimaam wa Ahlus-Sunnah

 

 

 

Kupigana Jihaad

 

Dini ya Kiislamu inawaita watu katika uongofu utokao kwa Allaah ili wafaidike na uongofu huo na ili wapate maisha mema ya hapa duniani na ya kesho Akhera.

 

Kwa ajili hiyo Allaah Ameupa Umma wa Kiislamu jukumu la kuinyanyua dini yake, na kuwafikishia watu wahyi wake kwa ajili ya kuuongoza na kuukomboa ulimwengu.

 

Na kwa ajili hii ndiyo umma huu ukawa umma bora kupita umma zote zilizodhihirishiwa watu, na ukawa mbele ya watu wengine ukiongoza mfano wa mwalimu na wanafunzi wake, na kwa ajili hiyo lazima uwe na uwezo wa kujihifadhi na wa kujidumisha, na pia uwezo wa kupambana kwa ajili ya kujipatia haki yake na ili uweze kuchukuwa nafasi yake iliyowekewa na Allaah.

Na kila mwenye kupunguza asitimize wajibu wake katika kujipatia haki yake hiyo, basi anahesabiwa kuwa amefanya makosa makubwa ambayo Allaah humdhalilisha kwayo au kumfutilia mbali.

Uislamu umekataza ulegevu na kutaka amani (kwa makafiri) ikiwa lengo halijafikiwa, kwa sababu kutaka amani katika wakati kama huu haitokuwa na maana yoyote wala tafsiri nyingine isipokuwa ni uoga na kuridhika kuishi kama watu duni.

 

Katika haya Allaah Anasema:

 

فَلا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الاَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَن يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ

“Basi msiregee na kutaka suluhu (piganeni nao maadui zenu) maana nyinyi ndio mtakaoshinda; na Allaah yu pamoja nanyi; wala hatakunyimeni (thawabu za) vitendo vyenu.”

Muhammad: 35

 

Na maana ya neno ‘mtakaoshinda’ maana yake ni kuwashinda na kuwa juu yao katika itikadi, ibada, mwenendo na tabia njema, elimu, na matendo.

Amani ya kweli haipatikani bila ya nguvu na uwezo wa kupigana vita, na hii ndiyo sababu Allaah akaweka sharti kuwa lazima adui aache kuwapiga vita waislamu na kuwafanyia uadui ili dhulma ipate kutoweka juu ya ardhi na ili mtu asiteswe kwa ajili ya dini yake.

Likiwepo mojawapo katika sababu hizo, basi Allaah ametoa idhini ya kupigana vita. (yaani ikiwa waislamu wanapigwa vita au wanadhulimiwa au wanafanyiwa uadui au wanateswa kwa ajili ya itikadi yao basi wanaruhusiwa kupigana vita).

Hapana dini yoyote iliyowapa idhini watu wake kuingia katika mapambano na kupigana vita kwa ajili ya kuisimamisha haki na kwa ajili ya kuwasaidia wanaodhulumiwa na kwa ajli ya kuishi maisha ya kuheshimika isipokuwa dini ya Kiislamu.

Kwa atakayefuatilia aya mbali mbali za Qur-aan tukufu pamoja na maisha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na ya makhalifa wake (Radhiya Allaahu ‘anhu) atayaona yote hayo kwa uwazi kabisa, kwani Allaah Subhanahu wa Taala anautaka umma huu kutumia nguvu zake zote katika kuyatimiza hayo.

 

Allaah Anasema:

 

وَجَاهِدُوا فِي اللَّهِ حَقَّ جِهَادِهِ

“Na ipiganieni dini ya Allaah kama inavyostahiki (kupiganiwa).”

Al-Hajj: 78

 

Kisha Allaah Subhanahu wa Taala ِAkabainisha kuwa Jihaad ni Imani ya matendo, ambayo bila ya hiyo dini haikamiliki, Akasema:

 

أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لا يُفْتَنُونَ. وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ

“Je! Wanadhani watu wataachwa kwa kuwa wanasema: Tumeamini. Nao wasijaribiwe?

Hakika tuliwajaribu walio kuwa kabla yao, na kwa yakini Allaah Atawatambulisha walio wa kweli na atawatambulisha walio waongo.”

Al-‘Ankabuut: 2-3

 

Kisha Akabainisha kuwa hii ndiyo njia aliyowaekea waumini, na kwamba hapana njia nyingine itakayowaletea ushindi na kuwaingiza Peponi, Akasema:

 

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُواْ الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْاْ مِن قَبْلِكُم مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاء وَالضَّرَّاء وَزُلْزِلُواْ حَتَّى يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ مَتَى نَصْرُ اللّهِ أَلا إِنَّ نَصْرَ اللّهِ قَرِيبٌ

“Mnadhani kuwa mtaingia Peponi, bila ya kukujieni kama yaliyo wajia wale walio pita kabla yenu? Iliwapata shida na madhara na wakatikiswa hata Mtume na walio amini pamoja naye wakasema: Lini nusura ya Allaah itakuja? Jueni kuwa nusura ya Allaah ipo karibu.

Al-Baqarah: 214

 

Akawataka Waislamu kujitayarisha vizuri na akawataka pia wawe wenye kutisha mbele ya makafiri, Akasema:

 

وَأَعِدُّواْ لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدْوَّ اللّهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لاَ تَعْلَمُونَهُمُ اللّهُ يَعْلَمُهُمْ وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللّهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لاَ تُظْلَمُونَ

“Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi waliofungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo ambao hamwajui, lakini Allaah Anawajua. Na mkitoa chochote katika Njia ya Allaah mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa”.

Al-Anfaal: 60

 

Na namna ya kujitayarisha inategemea wakati na hali ya mambo, na neno ‘nguvu’, maana yake ni kutumia kila njia inayowezekana kutumika kwa ajili ya kumuondoa adui.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

‘Hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha, hakika nguvu ya kweli ni kurusha.”

Muslim

 

Na katika kujitayarisha ni kuchukua hadhari na kumuandaa kila mwenye uwezo.

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ خُذُواْ حِذْرَكُمْ فَانفِرُواْ ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُواْ جَمِيعًا

“Enyi mlioamini! Chukueni hadhari yenu! Na mtoke kwa vikosi au tokeni nyote pamoja!

An-Nisaa: 71

 

Na kuchukuwa hadhari hakukamiliki ila kwa kujitayarisha na majeshi yanayoweza kupigana ardhini na baharini na angani.

Allaah akatuamrisha kupambana na adui tukiwa katika hali yoyote ile, iwe ya dhiki au katika neema, nzuri au mbaya, Akasema:

 

انْفِرُواْ خِفَافًا وَثِقَالاً وَجَاهِدُواْ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللّهِ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ

“Nendeni mtoke, mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihaad kwa mali yenu na nafsi zenu katika njia ya Allaah. Haya ni kheri kwenu mkiwa mnajua.”

At-Tawbah: 41

 

Uislamu unategemea zaidi nguvu ya imani kuliko nguvu ya silaha na kwa ajili hiyo unatilia nguvu zaidi mambo ya kiroho na kuiamsha hima na azma ya mpiganaji.

 

Allaah Anasema:

 

فَلْيُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللّهِ الَّذِينَ يَشْرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا بِالآخِرَةِ وَمَن يُقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيُقْتَلْ أَو يَغْلِبْ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا. وَمَا لَكُمْ لاَ تُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاء وَالْوِلْدَانِ الَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْ هَـذِهِ الْقَرْيَةِ الظَّالِمِ أَهْلُهَا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا وَاجْعَل لَّنَا مِن لَّدُنكَ نَصِيرًا

“Basi nawapigane katika Njia ya Allaah wale ambao wanaouza uhai wa dunia kwa Akhera. Na anaye pigana katika Njia ya Allaah kisha akauliwa au akashinda basi tutakuja mpa ujira mkubwa.

Na mna nini msipigane katika Njia ya Allaah na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako?”

An-Nisaa: 75-76

 

Na Muislamu anatakiwa awe na subira, kwani kama yeye avyoumia basi adui naye pia anaumia, tena yeye anaumia zaidi kupita wao, na hii ni kwa sababu ya hitilafu kubwa ya malengo yao.

Allaah ِAnasema:

 

وَلاَ تَهِنُواْ فِي ابْتِغَاء الْقَوْمِ إِن تَكُونُواْ تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللّهِ مَا لاَ يَرْجُونَ

“Wala msifanye uvivu kuwafuatia watu (walio maadui). Kama mmepata maumivu basi wao pia wanapata maumivu kama mnavyoumia. Na nyinyi mnatumai kwa Allaah wasiyoyatumai.”

An-Nisaa: 105

 

Na Akasema:

 

الَّذِينَ آمَنُواْ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ كَفَرُواْ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ الطَّاغُوتِ فَقَاتِلُواْ أَوْلِيَاء الشَّيْطَانِ إِنَّ كَيْدَ الشَّيْطَانِ كَانَ ضَعِيفًا

“Walioamini wanapigana katika Njia ya Allaah, na waliokufuru wanapigana katika njia ya upotofu. Basi piganeni na marafiki wa Shetani. Hakika hila za Shetani ni dhaifu.”

An-Nisaa: 76

 

Na maana yake ni kuwa; lengo la Waislamu ni tukufu, na ujumbe wao wanaotaka kuufikisha kwa watu ambao kwa ajili yake wanapigana Jihaad, ambayo ni risala ya haki na ya kheri, nayo ni kulinyanyua juu neno la Allaah ni tukufu pia.

 

Na Muislamu anatakiwa awe mwenye nyoyo thabiti kwenye mapambano.

Allaah Aanasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُواْ زَحْفاً فَلاَ تُوَلُّوهُمُ الأَدْبَارَ 15 وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلاَّ مُتَحَرِّفاً لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزاً إِلَى فِئَةٍ فَقَدْ بَاء بِغَضَبٍ مِّنَ اللّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Enyi Mlioamini! Mkikutana na walio kufuru vitani msiwageuzie mgongo.

Na atakaye wageuzia mgongo wake siku hiyo - isipo kuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi, basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allaah. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.”

Al-Anfaal: 15-16

 

Kisha Akawajulisha juu ya mahali ilipo nguvu zao za imani Aliposema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُواْ وَاذْكُرُواْ اللّهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلَحُونَ. وَأَطِيعُواْ اللّهَ وَرَسُولَهُ وَلاَ تَنَازَعُواْ فَتَفْشَلُواْ وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُواْ إِنَّ اللّهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Enyi mlioamini! Mkikutana na jeshi, basi kueni imara, na mkumbukeni Allaah sana ili mpate kufanikiwa.

Na mt'iini Allaah na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Allaah yu pamoja na wanao subiri”

Al-Anfaal: 45-46

 

Kisha Akatujulisha juu ya nafsi ya Muislamu, na kwamba lazima waipigane kwa juhudi zao zote, kwa sababu hawana isipokuwa hiari mbili tu, ama wauwe au wauliwe, Akasema:

 

إِنَّ اللّهَ اشْتَرَى مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللّهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَى بِعَهْدِهِ مِنَ اللّهِ فَاسْتَبْشِرُواْ بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

 “Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao watapata Pepo. Wanapigana katika Njia ya Allaah - wanauwa na wanauwawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa Haki katika Taurati na Injili na Qur'ani. Na nani atimizae ahadi kuliko Allaah? Basi furahini kwa biashara yenu mliyo fanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.

At-Tawbah: 111

 

Akiuwa atapata ushindi, na akiuliwa atakuwa amekufa shahidi na ataingia Peponi.

 

Allaah Anasema:

 

قُلْ هَلْ تَرَبَّصُونَ بِنَا إِلاَّ إِحْدَى الْحُسْنَيَيْنِ

 “Sema; ‘Nyini hamtutazamii sisi ila (kupata) moja katika mema mawili (ima kushinda au kuuawa mkapata Pepo).”

At-Tawbah: 52

 

Anayeuliwa katika Jihaad kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah hafi akatoweka kama wanavyokufa watu wa kawaida, bali wao wananyanyuliwa na kupelekwa mahali pema zaidi na bora zaidi. Kwa hivyo kufa katika njia ya Allaah maana yake hasa ni kubaki.

Allaah Anasema:

 

وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاء عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ. فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُواْ بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلاَّ خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلاَ هُمْ يَحْزَنُونَ. يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللّهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللّهَ لاَ يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِي

“Wala kabisa usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Allaah kuwa ni maiti. Bali hao ni wahai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.

Wanafurahia aliyo wapa Allaah kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.

Wanashangilia neema na fadhila za Allaah, na ya kwamba Allaah hapotezi ujira wa Waumini."

Al-‘Imraan: 169-171

 

Allaah siku zote huwa pamoja na wanaopigana Jihaad na wala hawaachi mkono.

Allaah Anasema:

 

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلآئِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُواْ الَّذِينَ آمَنُواْ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُواْ الرَّعْبَ فَاضْرِبُواْ فَوْقَ الأَعْنَاقِ وَاضْرِبُواْ مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ

“Mola wako Mlezi alipowafunulia Malaika: Hakika Mimi ni pamoja nanyi, basi watieni nguvu walio amini. Nitatia woga katika nyoyo za walio kufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.”

Al-Anfaal: 12

 

Kisha Allaah Anawatayarishia malipo mema hapa duniani na pia malipo mema huko Akhera.

 

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آَمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَى تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ. تُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّهِ بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ ذَلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ. يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ذَلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ. وَأُخْرَى تُحِبُّونَهَا نَصْرٌ مِّنَ اللَّهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

“Enyi mlioamini! Nikuonyesheni biashara itakayo kuokoeni na adhabu iliyo chungu?

Muaminini Allaah na Mtume wake, na piganeni Jihaad katika Njia ya Allaah kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.

Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.

Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Allaah, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!”

Asw-Swaff: 10 – 13

 

Kwa njia hii dini ya Kiislamu iliwalea waliotangulia na ikaweza kuingiza ndani ya nafsi zao imani iliyowawezesha kupambanua baina ya haki na batili na kuwawezesha kupata ushindi na kuziteka nchi na iliwawezesha kuwamakinisha vizuri juu ya ardhi.

Allaah ِِِAnasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ

“Enyi mlioamini! Mkimnusuru Allaah naye Atakunusuruni na Ataithibitisha miguu yenu.”

Muhammad: 7

 

Na ِAnasema:

 

وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُم فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَى لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ

“Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyo wafanya makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyo wapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.”

An-Nuur: 55

 

 

 

Share