03-Jihaad: Wajibu Wa Kuwa Thabiti

 

Wajibu Wa Kuwa Thabiti

 

Muislamu analazimika kuwa thabiti mbele ya adui na ni haramu kwake kurudi nyumba katika mapambano.

Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُواْ زَحْفاً فَلاَ تُوَلُّوهُمُ الأَدْبَارَ. وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلاَّ مُتَحَرِّفاً لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزاً إِلَى فِئَةٍ فَقَدْ بَاء بِغَضَبٍ مِّنَ اللّهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ

“Enyi Mlioamini! Mkutanapo vitani na wale waliokufuru basi msiwageuzie migongo (mkakimbia).

Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - basi atakuwa amestahiki ghadhabu ya Allaah. Na pahala pake ni Jahannamu, na huo ni mwisho muovu.”

Al-Anfaal: 15-16

 

Aya hizi zinawajibisha kuwa thabiti katika mapambano na zinaharamisha kurudi nyuma isipokuwa katika hali mbili zifuatazo;

 

Ya kwanza – Kwa ajili ya mbinu za kivita kama vile kuondoka mahali penye hatari zaidi na kukimbilia mahali bora, au kuondoka mahali anapoweza kudhurika kwa urahisi na kukimbilia mahali anapoweza kusitirika, au mahali pa chini na kukimbilia penye muinuko atakapoweza kupambana na adui kwa urahisi zaidi.

 

Ya pili – Kurudi kwa nia ya kuungana na wenzake kwa ajili ya kupambana kwa pamoja dhidi ya adui, au kwa ajili ya kuwasaidia wenzake hao, yote sawa ikiwa wenzake hao wako karibu au wako mbali.

 

Kinyume na hivyo, kurudi nyuma kwa ajili ya kukimbia tu ni mojawapo ya madhambi makubwa sana yatakayompelekea mtu kupata adhabu iumizayo.

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Jiepusheni na mambo saba yaangamizayo.”

Wakamuuliza:

“Ni yepi hayo ewe Mtume wa Allaah?”

Akasema:

“Kumshirikisha Allaah, Uchawi, kuiuwa nafsi iliyoharamishwa na Allaah, kula riba, kula mali ya yatima, kukimbia mnapokutana na adui, na kuwasingizia uongo wanawake waliotakasika wasiojua (maovu)."

 

Uongo Na Hadaa Vitani

 

Inajuzu kufanya hadaa na kusema uongo vitani kwa ajili ya kumbabaisha adui, sharti visitumike (uongo na hadaa) katika kuvunja mikataba na ahadi.

 

Mfano wa hadaa ni pale kiongozi anapomhadaa adui akamfanya adhani kuwa ana jeshi kubwa sana na nguvu nyingi.

Katika hadithi iliyotolewa na Al-Bukhaariy kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Vita ni hadaa.”

 

Na imetolewa na Muslim katika hadithi ya Ummu Kulthuum bint ‘Uqbah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa amesema:

“Sijapata kumsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akitoa ruhusa ya kusema uongo juu ya jambo lolote lile katika mazungumzo ya watu isipokuwa katika vita au katika kuleta sulhu baina ya watu na (pia) mtu anapozungumza na mkewe na mwanamke anapozungumza na mumewe.”

 

 

Rehma Vitani

 

Uislamu umeruhusu vita kama ni jambo la dharura na ukaweka vipimo maalumu juu yake, kwa mfano;

 

Asiuliwe isipokuwa anayeshiriki katika vita, ama aliyejitenga asipigane vita, huyo haijuzu kuuliwa au hata kudhuriwa kwa jambo lolote.

 

Imeharamishwa pia kuua wanawake, watoto, wagonjwa, wazee, maulamaa wa dini, wachaji Allaah na waloingia katika sulhu.

 

Imeharamishwa pia kuuharibu mwili wa aliyeuliwa kwa kukatwakatwa, kuuwa wanyama, kufisidi mazao, maji, kuvichafua visima na kubomoa nyumba.

 

Ni haramu pia kuua majeruhi, na kuendeleza chuki, na hii ni kwa sababu vita ni mfano wa opreshen ‘operation’, ambapo anachotakiwa tabibu ni kuyaondoa maradhi tu, na asivuke zaidi ya hapo.

 

Imehadithiwa na Sulaymaan bin Buraydah kutoka kwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anapomchagua kiongozi wa jeshi au wa kikosi, alikuwa akimwita pembeni na kumuusia kumcha Allaah yeye pamoja na maaskari wake, kisha akimwambia:

 

“Piganeni vita kwa jina la Allaah katika njia ya Allaah, piganeni na wanaomkufuru Allaah, piganeni lakini msichupe mipaka, wala msifanye khiyana, wala msiwaharibu maiti kwa kuwakatakata, wala msiuwe watoto.”

 

Amehadithia Nafia kutoka kwa ‘AbduAAllaah bin ‘Umar (Radhiya Allaahu anhu) kuwa katika baadhi ya vita, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimkuta mwanamke ameuliwa, akakataza kuuliwa kwa wanawake na watoto.

Muslim

 

Amehadithia pia Rawaah bin Rabia’ (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuona mwanamke ameuliwa katika mojawapo ya vita alivyoshiriki na huenda akawa ni huyo aliyetajwa katika hadithi iliyotangulia, akasimama mbele ya maiti hiyo kisha akasema:

 

“Hapakuwa na haja ya kumuua mwanamke huyu.” Kisha akawa anaziangilia nyuso za Maswahaba wake kisha akamwambia mmoja wao:

“Kamwahi Khalid bin Walid (umwambie); asiue watoto wala mateka wala mwanamke.”

 

Na katika usia wa Abu Bakr (Radhiya Allaah ‘anhu) alompa ‘Usaamah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipompeleka katika nchi ya Shaam alimwambia:

 

"Msifanye khiyana wala msishambulie bila taarifa (ghadran), wala msikate kate maiti za adui, wala msiuwe mtoto wala mzee wala mwanamke, wala msiunguze mtende wala msikate mti unaotoa mazao wala msichinje mbuzi au n'gome au ngamia ila kwa ajili ya kula. Na mtakutana na watu waliojitenga ndani ya mahekalu yao kwa ajili ya ibada, basi waacheni hivyo hivyo walivyo."

Kisha akasema: "Nendeni kwa jina la Allaah."

 

Na usia kama huu alikuwa akitoa ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na wengine miongoni mwa Makhalifa wa Kiislamu.

 

 

Mwisho

 

 

Share