Hikma Ya Kurudia Adhkhaar Na Du’aa Mara 3 Au Mara 7
SWALI:
Assalam Alaykum Warahmatullaahi. Alhamdullahi, tunamshukuru Allah kwa kuwaezesha kututatulia maswali yetu na InshaAllah jaza yenu iko kwa Allah. Swali langu ni hili? Kuna dua nyingine ukisoma unatakiwa uregelee 3 ama 7? Je kuna umuhimu gani kuregelea ama pengine kuna hadithi?
Jazakallah kheir
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kurudia du‘aa mara 3 au zaidi.
Bila shaka mara nyingi huwa tunachanganya baina ya du‘aa na dhikr (utajo au nyiradi).
Adhkaar ndio mara nyingi zinakuwa zaidi ya mara moja na hizo idadi pia huwa zimetokana na Hadiyth. Kwa mfano, Adhkaar baada ya Swalah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuagiza tuseme Subhaana Allaah mara 33, AlhamduliLlaah mara 33, Allaahu Akbar mara 33 na Laa ilaaha Illa Allaah wahdahu Laa Shariykha Lahu, Lahul Mulk wa Lahul Hamd Wa Huwa ‘Alaa Kulli Shay-in Qadiyr mara 1 au mara 100 katika riwaaya nyigine. Pia tumefundishwa kufanya Istighfaar mara 70 au 100 kwa siku kwa kusema Astaghfiru Allaah Wa Atuwbu Ilayhi n.k.
Hayo ndio mafundisho yalivyokuja na hatukutajiwa hekima ya hizo idadi ila tumetajiwa baadhi ya fadhila kwa Adhkaar mbalimbali tunazosoma. Na kuamini na kufuata bila kutaka kujua zaidi yasiyoelezwa kwetu kutoka Qur-aan na Sunnah ndio dalili ya imani.
Kwa faida zaidi utapata kwenye kitabu hiki cha Du’aa na Adhkaar:
Ama Du‘aa ni vizuri kuomba mara tatu kwani ndivyo tulivyofunzwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :
..وَكَانَ إِذَا دَعَا دَعَا ثَلَاثًا وَإِذَا سَأَلَ سَأَلَ ثَلَاثًا ثُمَّ قَالَ: ((اللَّهُمَّ عَلَيْكَ بِقُرَيْشٍ)) ثَلَاثَ مَرَّاتٍ...
...na alikuwa anapoomba anaomba mara tatu, akiuliza anauliza mara tatu kisha akaomba: ((Ee Allaah, juu Yako Maquraysh)) mara tatu ...)) [Muslimu]
Na Allaah Anajua zaidi
- Login or register to post comments
- Email this page
- Chapisha
