Skip navigation.
Home kabah

Kumlipia Mtu Kwenda Hajj

SWALI

AAWW!

Nauliza:

1. Mume kumtolea nauli ya matumizi mke kwenda HIJJA inasihi? Kama jibu ni ndiyo, kuna pre-requisites e.g. Jee kama yeye mwenyewe an uwezo? Si Hijja inamjuzu mwenye uwezo tu.


2. Hizi Hijja wanzokwenda viongozi kwa gharama za serikali au mialiko ya mfalme wa Saudia zinasihi?
Wabillahi Taufiq,

 

 



JIBU

Kama tunavyoelewa kuwa Hijjah ni nguzo ya tano kwa Waislamu nayo ni Faradhi kwa waume na wake. Hiyo ni kuwa taklifu zote za amali katika Uislamu ni faradhi kwa wote. Allah Anasema:

Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, Tutamhuisha maisha mema; na Tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda(16: 97).

Na Hijjah imefaradhishwa kwa wote pindi yanapopatikana masharti Fulani. Allah Anasema:

Ndani yake zipo Ishara zilizo wazi - masimamio ya Ibrahim, na mwenye kuingia humo anakuwa katika amani. Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea. Na atakaye kanusha basi Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa walimwengu (3: 97).

Na Mtume (s.a.w.) amesema: “…Na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo” (Muslim, Abu Dawud, at-Tirmidhy na an-Nasai kutoka kwa ‘Umar bin al-Khatwaab [r.a]).

Ibara hii ya aya na Hadithi ina maana ya kuwa kila Muislamu ni lazima ahiji mara moja katika maisha yake akiweza kufanya hivyo. Uwezo una tafswili nyingi na yaliyo muhimu ni: -

  1.    Awe na afya nzuri ya kuweza kustahamili mazito ya safari.
  2.   Kuwe na usalama njiani – kwenda na kurudi.
  3.   Awe na uwezo wa kutoa gharama za safari na kuacha masurufu   

          yote ya wale wanaomtegemea. 

Ikiwa sharti moja katika hayo limekosekana basi Hijjah haijamlazimu mtu huyo. 

Hivyo, tukija katika swali la kwanza jibu ni kwamba inafaa kwa mume kumpeleka mkewe Hijjah ikiwa atakuwa ana uwezo huo. Na inapendeza zaidi ikiwa watakwenda pamoja kwani hilo litaongeza mahaba baina yao. Na kwa ajili hiyo alipokuja mtu kwa Mtume (s.a.w.) akamwambia kuwa mkewe anakwenda Hijjah naye amejiandikisha kwenda katika Jihadi, Mtume (s.a.w.) alimwambia aende na mkewe kuhiji.

Na ni msingi wa Uislamu kuwa ((yeyote mwenye kumuelekeza mtu mwengine katika kheri atapata thawabu sawa na mwenye kufanya hiyo amali)) (Muslim, Abu Dawud, at-Tirmidhy na Ibn Maajah kwa kwa Ibn Mas‘uud na Abi Hurayrah [r.a]).

Na hivyo hivyo ikiwa mke ni muweza kuliko mumewe anaweza kumsaidia mumewe kumpeleka Hijjah na pia atapata ujira mkubwa. Ikiwa mke ana uwezo anaweza kujipeleka mwenyewe na wakati huo inakuwa ni lazima kwake kwa sababu masharti yote yametimia. Ikiwa hana uwezo haiwi ni lazima kwake lakini ikiwa atasaidiwa kutekeleza Faradhi hiyo basi hakuna tatizo lolote. Na hii ni ‘Ibadah ambayo ni tofauti na ‘Ibadah nyingine ambazo mtu hata akiwa mgonjwa anatakiwa afanye mwenyewe kama Swalah, lakini Hijjah ikiwa  mgonjwa huwezi kwenda mwenyewe unaweza kumpatia mtu hela zinazohitajika akaenda kukuhijia.

 

(2) Kwa hakika usaidizi unatakiwa upewe Waislamu wanaostahiki ambao ni     hohehahe. Mara nyingi fursa hizi huwa zinatumiwa vibaya kwa kupewa watu ambao ni viongozi wenye uwezo au ambao tayari wamekwenda. Na haitakuwa vyema ikiwa mtu ana uwezo kukubali mwaliko kama huo na vizuri akatae lakini wakati mwengine serikali ya Saudia huwa inataka viongozi wa nchi tofauti kwa ajili ya makongamano na mikutano na ikiwa ni msimu wa Hijjah basi hutaka waalikwa wao wafanye Hijjah kabisa na katika hilo hakuna tatizo. Hijjah aina hizi hazina tatizo lolote na ni thawabu kwa wenye kujitolea kwa hilo. Hata hivyo kujitolea huko kungekuwa natija nzuri zaidi lau wangepatiwa: -

 

1)         Waislamu wasiokuwa na uwezo (masikini na mafakiri).

2)         Wale ambao hawajawahi kwenda kabisa.

3)               Wenye uwezo kukataa kuchukua fursa hizo na badala yake kupendekeza   watu wengine.

4)        Kina mama pia nao wapatiwe fursa hizo.

5)        Kusiwe na ubaguzi katika kuchagua watu.

 

Na Allah Anajua zaidi.