020-Unawezaje Kuupata Moyo Wa Mumeo Na Kumridhisha Mola Wako: Kumtii Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) Kunaingiza Furaha Katika Nyumba

 

KUMTII ALLAAH (SUBHAANAHU WA TA’ALA) KUNAINGIZA FURAHA KATIKA NYUMBA

 

Mara nyingi sisi huwa tunasahau Akhera, lakini haitokezei mtu kusahau kuwanunulia watoto wake nguo mpya za ‘Iyd na hatusahau kamwe kununua aina mbali mbali za vyakula na vinywaji tukitaka kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhaan kila mwaka.

 

Mara nyingi tunashindana ili tuonekane kuwa tuna nyumba nzuri za kisasa zaidi na hili ni jambo zuri halina tatizo lakini Je, tunashindana kwa kiasi hicho hicho kushindania kufanya ‘amali za Akhera nayo ndio amali bora zaidi zinazokusanya maisha mazuri zaidi na ndio maisha halisi.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) anasema,

“…Na katika hayo washindane wenye kushindana.(83:26)

 

Ewe, mke Muumini, Muangalie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimgongea mwanae Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘anha) akiwa na mumewe ‘Aliy usiku akiwaambia wote wawili,

‘Je, Hamswali?!![1] maneno haya yalikuwa ni kulingania katika kushindana katika mambo ya kheri na kujitenga katika kufanya ibada za siri kwa ajili yako ili ikikurubishe kwa Mola wake Mkarimu, kwa hakika Swalah za usiku, hali ya kuwa watu wamelala nyakati hizo ni bora zaidi na zina baraka.

 

Tunasoma katika Hadiyth sahihi kuwa,

“Mwenyezi Mungu Amrehemu mtu aliyesimama usiku akaswali kisha akaamsha familia yake akikataa humwagia maji usoni, kisha Mwenyezi Mungu Amrehemu mwanamke aliyeamka usiku kuswali kisha akamuamsha mume wake akikataa anamwekea maji usoni mwake”[2]

 

Wala sidhani kuwa mke ambae hii ndio hali yake anaweza kuleta matatizo ambayo yakafanya nyumba yao ikawa na migongano na nyufa kubwa, bali jambo la kheri na zaidi ya kheri katika nyumba iliyogubikwa na utiifu, ni kuendelea kuwahimiza katika kufanya mambo ya kheri.

 

 





[1] Al-Bukhaariy na Muslim

[2] Abu Daawuud

Share