Uzushi Wa Mi'raaj, Nisfu Sha'baan Na Swalah Katika Kumi La Mwisho Ramadhwaan

SWALI:

ASSALAAMU ALAYKUM NDUGU ZANGU,

NAOMBA KUWAULIZA NISAIDIENI TAFADHALI KUNA FWDZ ZA SUNNA ZA KASMATI RIZKI,   MERAAJ,   LAILATUL QADRI, NA TAKRIBAN   MIEZI YOTE   12   YA MWAKA WETU--KILA MWEZI NA RAMADHAANI SIKU YA IJUMAA WA MWISHO UNASALI SUNNA   BAADA YA SALATI JUMAA ILI KULIPA SWALAH ULIYOKUWA HUJAZISALI YAANI SALA ZA KUFUTIKA. NAOMBA KUONGOZWA NIONGOZENI. JAZAAKALLAHUKHEIR FIAMAANILLAH.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali lako hilo kuhusu mas-ala hayo uliyoyataja hapo juu. Hakuna du’aa, Swalah wala Ibadah maalumu ya mtu kupata riziki au kugaiwa riziki kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Kila mtu anapozaliwa huwa ashaandikiwa riziki na umri atakaoishi hapa duniani. Kwa hivyo kuomba du’aa wakati wa nusu ya Sha'abaan haipo katika Uislam kabisa.

Kuhusu Mi'iraaj huwa watu wanafunga na kufanya mambo mengine mambo ambayo hayana dalili wala msingi katika Dini yetu tukufu. Tukio hilo ambalo lilitokea katika maisha ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) bila shaka yoyote. Lakini wana-historia wametofautiana kuhusu tarehe na haijulikani kihakika ni gani japokuwa wengine wamechukua ni 27 Rajab. Wakati huo hata Swawm yenyewe ilikuwa haijafaradhishwa kwa Waislam.

Kuhusu Laylatul-Qadr tunapata du’aa ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyomfundisha mkewe, 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) baada ya kumuuliza nikiupata usiku huu nisemeje? Akamjibu: "Sema: Allahumma Innaka 'Afuwwu Tuhibbul 'Afwa Fa'fu 'anniy (Ewe Allah! Hakika Unapenda kusamehe, hivyo nisamehe)" (at-Tirmidhiy).

Katika usiku huo ambao haujulikani hakuna amali nyengine inayotakiwa mbali na kusoma Qur-aan, kuswali Swalah ya usiku, kumdhukuru Allah na amali nyengine ambazo ziko katika sheria. Haifai kuzuru makaburi usiku huo wala kufanya amali nyengine zilizozuliwa.

Katika jambo la ajabu lililozuliwa ambalo halimo ni watu kuhudhuria Swalah ya Ijumaa ya mwisho ya Ramadhaan. Kwa kufanya hilo imezuliwa Hadiyth kuwa hiyo ni Jum’atul-Widaa (Ijumaa ya kuaga) ambayo haimo katika sheria. Watu wameipatia fadhila kubwa sana kuwa mwenye kuswali siku hiyo basi madhambi ya mwaka mzima amesamehewa hata madhambi makubwa ambayo hajafanya toba ya kisawasawa. Sunnah za siku hiyo ni kama za kawaida hakuna kabisa ati unakidhi Swalah za mwaka mzima. Hili ni jambo geni katika Uislamu ambalo halikuwepo wala halitakuwa. Hakuna dalili kabisa ya kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu jambo hilo.

Nasaha zetu za dhati ni kuwa tuache tabia ya kuongeza au kuzua katika Dini, kwani mambo yote hayo hayatakuwa na uzito wowote Siku ya Qiyaama bali yatamuingiza mfanyaji motoni. Tunamuomba Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuepushe na amali isiyokubaliwa mbele Yake na Atupe mwisho mwema. Tujiweke mbali na uzushi katika Dini, kwani madhambi yake ni makubwa.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share