Skip navigation.
Home kabah

Unapopata Mitihani Subiri

 

             Abdallaah Bin Eifan

           (Jeddah, Saudi Arabia)

 

 

Salaam waheshimiwa, nawaombea baraka,
Tunaomba kujaliwa, kila kheri na fanaka,
Tupate kuondolewa, mitihani na mashaka,
Mtihani Ukifika,
Subira Inatakiwa.

 

Subira inatakiwa, mtihani ukifika,

Utajiri ukinyimwa, halafu ukasumbuka,
Usidhani umetupwa, Kakusahau Rabuka,
Mtihani Ukifika,
Subira Inatakiwa.

 

Na mitihani mikubwa, kama inamiminika,
Tumshukuru MKUBWA, subira hulazimika,
Tuzidi kuomba duwa, hapana kulalamika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Msiba unapokuwa, dhaifu hutetemeka,
Kama mwehu anakuwa, imani inamtoka,
Anasahau ya kuwa, Mungu hivyo Ametaka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Na makelele kupigwa, maafa yakimfika,
Na yote yamekatazwa, Mungu Anaghadhibika,
Apenda  Kushukuriwa, Mola wetu Mtukuka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Kuvumilia ni sawa, na imani kuiweka,
Hadhulumiwi muumbwa, kwa haki kinatendeka,
Hakuna cha kuonewa, imani ya nguvu shika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Yote yamesajiliwa, Mungu Ameshaandika,
Kalamu kuinuliwa, wino umeshakauka,
Mitihani ukikumbwa, hakuna kubadilika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

 

Tangu bado kuzaliwa, vyote vimeandikika,

Riziki imegawiwa, na ajali kadhalika,

Yote hayo majaliwa, hapana kunung’unika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Usikubali kushindwa, shetani akakuteka,
Utageuka mfungwa, wa shetani ni mateka,
Hapo umeshaangushwa, na imani kutoweka,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

Hapa nafunga baruwa, pengine mmeshachoka,
Tunaomba maridhawa, Mola Apate Ridhika,
Tunaomba kuepushwa, na madhambi kufutika,

Mtihani Ukifika, Subira Inatakiwa.

 

 

 

(No subject)

SABURI

Kweli uliyo nena,Saburi kwa kila kitu,QUR'AN 4:45
Mabaya tukiyaona,mithili kukosa kitu,
Hakuna kugombezana,Anapanga Ya~Musitu,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Kusema Inna~Lilihi,Wainna~Ilahi Rajiuni,
Jioni na asubuhi,Tunaipata thamani,
Sawa baro na nikahi,Kheshima kupe Manani,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na Misiba.

Vyema ibada matano,Kwa njia tano nasema,
Riziki yenye mavuno,Kusali dhuha karama,
Hili sifanye achano,Tutakipata kilema,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Riziki tukiitaka,Fumbo lake lipo ndani,
Amenena Mtukuka,Ni MTUME[s.a.w] hadithini,
Dhuha tukiishika,Ni neema maishani,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Lapili nuru kaburi,Kwasala za Tahajudi,
Usingizi ni kiburi,Tukwepe na ukaidi,
Mema kupata saburi,Tukirudi kwa WA~DUDI,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Kaburi kiwanja pepo,Kwa waja tukiwa wema,
Nahili pia lipo,Amenena ALLAAHUMA,
Aliye muumba popo,Na sisimizi ahema,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Kama twatenda maovu,Kaburi zetu motoni,
Tutatamani wokovu,Pindi tukiwa jutoni,
Mithili ya kuni jivu,Au samaki chunguni,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Fikiri Munkari na Nakiri,Ndiyo wetu wasaili,
Majibu yalo mazuri,Qur'an ni wakili,
Tusome bila jeuri,Na hata ya kiswahili,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Maswali ya dini yako,MOLA wako na Mtume[s.a.w],
Kibla tuelekeako,Midomo yetu iseme,
Qur'an ndiyo simbiko,Shime ndugu tuisome,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Na kuivuka Swirati,Kwa wepesi na haraka,
Njia yake madhubuti,Ni Swaumu na Sadaka,
Haya kuyafanya nti,Tunaondoa mashaka,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Tufunge swaumu za suna,Na Mwadhamu Ramadhani,
Ameyafanya Rabana,Mitume ipo kundini,
Sadaka iwe amana,Itatutoa motoni,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Kupata hili sharifu,KIvuli siku hukumu,
Kwa rehema za RAUFU,Kwa siku iliyo ngumu,
Njia yake itikafu,Kutawa kitu muhimu,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Hakutakuwa kivuli,Isipokuwa cha Mungu,
Sote tutakuwa dhili,Joto lajua uchungu,
Tulifanyeni na hili,Kupata radhi za Mungu,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Matano haya magumu,Njia zake ni ibada,
Nawakumbusha kaumu,Kina kaka kina dada,
Nami nipo ndani humu,Ibada ni kama ada,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Tutende yalo amali,Haya tukiyakumbuka,
Atatuafu JALALI,Ibada tukizishika,
Ikitufika ajali,Hesabu kuhesabika,
Saburi kito aghali,Tukifikwa na misiba.

Haya matano tamati,Na njia nimekumbusha,
Hongera ya ithibati,Sauri umefurusha,
Sasa yafaa kunuti,Ibada kutokatisha,
Saburi ndiyo subira,Umenena ya khakika.

Mateno
Nduguyo