Kumpa Mnunuzi Bei Ya Bidhaa Kuliko Anayopelekewa Kawaida

SWALI:

 

Assalam Alaykum Waba'ad je inafaa katika sheria ya kiislamu kumpelekea mnunuzi bidhaa na kumpunguzia bei kuliko ile anayopelekewa kawaida? Mfano una trea zako za mayai ukataka kuzipeleka dukani kwa jumla akakwambia muuza duka kuna mtu ananiletea kwa 5000 wewe ukampa bei ya 4700 ili zitoke zako. Je dini imekataza?

 


 

 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumpa mnunuzi bei ya chini kuliko anavyonunua.

Hakika ni kuwa biashara ni jambo ambalo limekubalika Kiislamu ikiwa bidhaa zinazouzwa ni halali na ikiwa mtu anafuata maadili ya Kiislamu katika kutekeleza shughuli hiyo.

 

Biashara kawaida ni masikilizano baina ya muuza na mnunuzi kwa bidhaa inayouzwa. Hakuna tatizo kwa mtu kupunguza bei ya bidhaa zake kwa ridhaa yake bila kulazimishwa na yeyote. Na kawaida hata ukizungumza kama mfano uliotoa wa mayai, yangu na yako hayatakuwa sawa. Na hata yakiwa sawa kwa kila kitu unaweza kuona kuwa mmoja anatumia gharama za chini katika kuzalisha ilhali mwingine gharama zake ni za juu.

Kwa minajili hiyo unaweza kukuta kuwa mmoja wao anaweza kuuza kwa bei duni kuliko mwengine.

Na hata mashindano ya kuwapata wateja pia yakiwa yapo katika maadili yanayotakiwa ya Kiislamu kutakuwa hakuna matatizo.

 

Hivyo hakuna tatizo katika kupunguza bei ya bidhaa zako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share