Skip navigation.
Home kabah

Ukiukwaji Wa Mafunzo Ya Kiislamu Ndani Ya Nyumba Zetu

 

Ummu Naswrah

 

بِسمِ ٱللهِ ٱلرَّحمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

 

UTANGULIZI

 

Hakika shukrani zote ni zake Allaah, tunaemshukuru, tunaemtegemea, kumtaka msamaha na kutubu kwake.  Tunajikinga Kwake Allaah kutokana na shari za nafsi zetu na makosa ya matendo yake. Mwenye kuongolewa na Allaah hakuna wa kumpotoa, na mwenye kumpotoa hakuna wa kumuongoa.  Rahma na Amani ziwe juu ya kipenzi chetu Muhammad SwallaAllaahu ‘Alayhi wa Aalihu wa Sallam.

‘Amma Ba’ad

 

Nyumba ni neema kubwa ambayo mwanadamu amebarikiwa,

وَٱللَّهُ جَعَلَ لَكُم مِّنۢ بُيُوتِڪُمۡ سَكَنً۬ا

“Na MwenyeziMungu Amekujaalieni majumba yenu yawe maakaazi (yenu)” [An-Nahl 16: 80]

 

Kuweka mazingira sahihi ndani ya majumba ni jukumu la kila Muislam mume na mke, na ni lazima mazingira hayo yaoane sambamba na sheria alizotuwekea Allaah (Subhanahu wa Ta’ala).   Moja kati ya njia ya kuyafikia hayo ni kuepukana na kila aina ya uovu na uharibifu ndani ya majumba.

 

Kuna sababu nyingi kwa mwenye kuamini kuwa makini katika kuijenga na kuilinda nyumba yake katika misingi mema ya Kiislam. Miongoni mwa sababu hizo ni:

 

1.     Kujilinda yeye pamoja na familia yake kutokana na moto wa jahannam, na kujiweka mbali na ghadhabu zake.

 

يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ قُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ وَأَهۡلِيكُمۡ نَارً۬ا وَقُودُهَا ٱلنَّاسُ وَٱلۡحِجَارَةُ

Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu na moto ambao ambao kuni zake ni watu na mawe” [At-Tahriym 66: 6]

 

2.     Kujua wajibu wake juu ya jukumu la kuchunga nyumba, na kujiweka tayari kujibu kwa kila anachokichunga.

 

“Kila mmoja ni mchungaji, na kila mmoja ataulizwa juu ya anachokichunga.” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

3.     Nyumba ni sehemu ya hifadhi kwa binaadamu, kujiweka mbali na kila aina ya ubaya na uovu ukiwa wa mnyama, binaadamu au majini, na kupata utulivu ndani yake.  Amesema Mtume SwallaAllaahu ‘Alayhu wa Ssallam: 

 

“Usalama wa mtu katika wakati wa fitnah ni kubakia nyumbani kwake.”

 

Kilicho muhimu zaidi ni kuzingatia kuwa nyumba ni sehemu nyeti (muhimu) ya kujenga mazingira mazuri ya Kiislam, kwani jamii bora hujengeka kuanzia nyumbani. Kwa masikitiko makubwa majumba yetu mengi yamejiweka mbali na mafundisho sahihi ya Kiislam.

 

InshaAllaah katika makala hii tutaweza kugusia na kutanabahisha baadhi ya vitu ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika mfumo wa Kiislam ndani ya majumba na jamii kwa ujumla, na kujaribu kutafuta njia muafaka kurejesha mazingira mazuri ndani ya mjumba yetu.

 

 

YENYE KUHATARISHA MAJUMBA YA WAISLAM

Kuna mambo mengi ya wazi kabisa ambayo sheria yameyakaza katika uislam na jamii imeghafilika nayo.  Mambo hayo huchangia kuharibika na kuhatarisha mfumo  mzima wa Kiislam ndani ya majumba.  Miongoni mwa yenye kuhatarisha ni haya yafuatayo:

 

1.    TELEVISHENI (TV)

 

Televisheni kama inavyojuilikana (TV) ni chombo ambacho hakikosekani katika kila nyumba. Kama kitatumika vizuri chombo hicho kwa mambo ya kheri yenye kuzidisha imani, kupeleka dini mbele, kukuweka mbali na maasi na kuhifadhi dini ya mja kinaweza kuleta faida.  Na kama kitatumika vibaya kinaweza kuathiri familia kwa asilimia kubwa kabisa.

 

Ukweli ni kuwa kuangalia TV kuna madhara mengi na makubwa kuliko faida. Familia za Kiislam zinaogelea kwa kasi kubwa bila ya kujali au kuona mabaya ya chombo hicho. Hasara moja ya kupoteza muda kuangalia TV inaweza kuzaa makosa mengi ndani yake. Kuona na kusikiliza kunawavutia wengi na kuwafanya watu kutawaliwa na tabia hiyo na kutoweza kuiepuka. Hakuna shaka kuwa jamii hasa watoto imeathirika sana na jambo hili. TV inasababisha kwa kiasi kikubwa watoto wa Kiislam kutumbukia katika tabia zisizo na maadili, ulevi, uzinzi, kukosa heshima, kujinasibisha na uzungu na mengi mengine maovu tunayoyaona katika jamii zetu.  Yote hayo wanayaona na kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye TV.

 

Mtu huhisi kuwa anapoteza wakati tu kujistarehesha na TV, anayakata masaa na dakika kwa ajili ya chombo hicho, ni makosa!!  TV si chombo cha starehe, bali ni chombo kinachotumika kuchochea hisia, kubadilisha muelekeo na utiifu wa mtu.  Yafaa Waislam tuzinduke na kuziona faida chache na hasara nyingi za chombo hiki.  Kama tunaona ni neema hakika tutakuja kuulizwa namna tulivyoitumia. 

ثُمَّ لَتُسۡـَٔلُنَّ يَوۡمَٮِٕذٍ عَنِ ٱلنَّعِيمِ

“Kisha mtaulizwa siku hiyo juu ya neema mlizopewa mlizitumiaje.” [At-Takaathur 102: 8]

 

 

Na kwa hakika hata masikio na macho tunayoyatumia kwa chombo hicho pia tutakuwa ni wenye kuulizwa. Hivyo ni juu yetu kuchagua ni kipi cha kutizama.

إِنَّ ٱلسَّمۡعَ وَٱلۡبَصَرَ وَٱلۡفُؤَادَ كُلُّ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ كَانَ عَنۡهُ مَسۡـُٔولاً

“Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa.” [Al-Israa 17: 36]. 

 

TV ni kama upanga ukiutumia vizuri unaweza kuleta faida na ukiitumia vibaya unaweza kuleta madhara makubwa. Kwa mfano mtu akiweza kuidhibiti na kuangalia kwa nadra kwa vipindi vya kheri vyenye kwenda sambamba na dini yetu inaweza kukubalika, bali ni wachache wenye kufanya hivyo. Wengi wao wameogolea na kuangalia tu bila hata ya kujali faida na hasara zake, na hii ndio iliopelekea madhara kuwa mengi kuliko faida. Miongoni mwa madhara ya TV ni:

 

 

-         Kupoteza wakati bure na kupuuza mengi ya wajibu

-         Inaeneza tamaduni za kikafiri kama ni njia moja ya kuigwa katika maisha

-         Inaeneza upotofu na uhuru kwa kupitia katika michezo, nyimbo matangazo yasiyo ya heshima ambayo hupelekea watizamaji kutumbukia katika tabia hizo za kijinga.

-         Mazoea ya kuangalia TV yanaharibu akili na kuathiri afya ya mtu.

 

Hivyo kama kuna watu wazuri wenye kumuogopa Allaah na kuonyesha mazuri yenye faida bila ya kukiuka mipaka ya Allaah, basi unaweza kuangalia na ni jambo la kupendeza kwa wengi. Ni vyema kuchunga aina gani ya vipindi tunavyoangalia ndani ya majumba yetu.  Ni wajibu wa kila mtu kuelewa wazi madhara na faida ya kifaa hichi ili tuweze kukitumia vyema ama kujiepusha nacho kabisa.

 

 

2.  MUZIKI

 

Miongoni mwa yenye kuzoeleka katika majumba yetu ni muziki. Kwa kweli muziki umeenea kila pembe ya dunia kiasi ambacho unawaumiza Waislamu wengi kimwili na kiakili bila ya kujijua. Kila mtu amekabiliana na hali ambayo humuingiza kusikiliza muziki ama kwa hiari au kwa lazima. Kuongezeka umaarufu wa muziki kunahatarisha sana majumba ya Waislam na hatimae kutumbukia katika balaa hilo usiku mchana.

 

Ukweli ni kuwa muziki unaathiri sana mioyo ya Waislam na kuishughulisha akili kwa mambo ya kipuuzi. Tunatumia muda na pesa nyingi katika kununulia CD za nyimbo zisizo na faida, zana za miziki, na hata kuwatumbukiza watoto wetu kwa vifaa (toys) mbali mbali vilivyojaa miziki; Tunajitia makosani na kuuporomoa itikadi sahihi ya Muislam. Kuna dalili tosha katika Qur-aan na Sunnah zenye kuonyesha uharamu wa muziki. Katika Suurat Luqmaan aya ya 6, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatueleza:

((وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا أُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ))

“Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha” [Luqmaan: 6]

Maulamaa pamoja na wafasiri wengi wa Qur-aan wameeleza kuwa neno ”Lahwal-hadiyth” katika aya hii inakusudiwa nyimbo na zana za miziki. Mfano
Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema kuhusu Aayah hii: "Naapa kwa Allaah hii inamaanisha ni nyimbo"

Pia miongoni mwa Hadiyth zenye kuonyesha uharamu wa ngoma na kila aina ya muziki ni Hadiyth mashuhuri ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki.” [Al-Bukhaariy]

 

Ni vyema tuelewe kuwa hakuna chochote Alichokikataza Allaah isipokuwa kina madhara ndani yake katika ustawi wa jamii. Jua kuwa miziki tunayoichezesha majumbani inaweza kuchochea hisia za mtu, jazba pamoja na muengezeko wa mapigo ya moyo na kushughulisha akili. Ujumbe unaopatikana katika miziki na nyimbo nyingi hasa wakati huu tulionao huenda kinyume kabisa na maadili ya Kiislam, huamsha hisia za mapenzi, uzinzi na uhuru wa kufanya lolote bila ya kuzingatia wajibu wa mja.

 

Umefika wakati kwa Waislam kutanabahi na kujaribu kwa kadiri ya uwezo wetu kuepukana na balaa hili na kurejesha mandhari nzuri ndani ya majumba yetu.  Tusiziuwe nyumba zetu kwa sauti za Shaytwaan (nyimbo na miziki) na kuwawekea makaazi. Ni lazima tuziuhishe nyumba zetu kuwa ni sehemu ya kumkumbuka Allaah (dhikr) kwa kila hali; kwa Swalah, kusoma Qur-aan, na vitabu vyengine vya dini pamoja na masuala mbali mbali yanayowahusu Waislam. Hii itatupelekea kuzungukwa na Malaika, kulindwa na kupata ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

 

 

3. MCHANGANYIKO WA WANAUME NA WANAWAKE (IKHTILAATW)


Moja katika jambo linaloonekana ni la kwawaida hasa katika majumba yetu ni michanganyiko ya wanaume na wanawake (Ikhtilaatw). Ni wajibu wa kila Muislam kuelewa hukumu ya kishari’ah juu ya jambo hili.

 

Ikhtilaatw ni kuchanganyika kwa wanawake na wanaume waliokuwa sio maharim ima kwa wingi au uchache katika sehemu moja. Hali hii imezoeleka sana majumbani mwetu na katika shughuli zetu zikiwa ni za furaha au misiba. Tuelewe kuwa mijumuiko ya aina hii na kudhihirika mapambo ni kitu kilichokatazwa katika shari’ah, huwa ni mzizi wa fitina na ni kichochezi cha maasia mengine kwani Shaytwaan huwa pamoja nao. Katika Hadiyth iliyosimuliwa na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila Shaytwaan huwa ni watatu wao.” [At-Tirmidhiy]

Dini yetu imetuwekea adabu maalum; na kama kuna ulazima wa kuingiliana majumbani, basi ni vyema kuwe na sehemu tofauti kati ya wanaume na wanawake. Tunatakiwa tuwe na hadhari tunapotembelewa na mgeni, hata kama ni ndugu wa mume. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaeleza Maswahaba zake na Waislam wote kuwa:

“Tahadharini kuingilia majumbani mwao wanawake; Wakasema: Ee Mjumbe wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: Shemeji ni mauti.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatueleza:

 

وَإِذَا سَأَلۡتُمُوهُنَّ مَتَـٰعً۬ا فَسۡـَٔلُوهُنَّ مِن وَرَآءِ حِجَابٍ۬ۚ ذَٲلِڪُمۡ أَطۡهَرُ لِقُلُوبِكُمۡ وَقُلُوبِهِنَّۚ

 

“Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia. Kufanya hivyo kunasafisha nyoyo zenu na zao.” [Al-Ahzaab: 53]

 

Ni jukumu letu kama ni wazazi kuzielewa shari’ah hizi na kuzidi kuzipamba nyumba zetu katika mandhari nzuri ya Kiislam. Hii itasaidia hata na vizazi vyetu kuinukia kwa maadili na tabia njema na kujua mipaka yao. Na kama itatokea kwa mwanamume au mwanamke kutembea au kutembelewa na kukutana na mwenyeji wa jinsia tofauti basi na amuogope Allaah na kujihifadhi kwa kadiri ya uwezo wake, wala asirefushe mazungumzo.

 

Allaah Aliyetukuka Anafahamisha katika Qur-aan:

 

ذَٲلِكَ أَزۡكَىٰ لَهُم إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرُۢ بِمَا يَصۡنَعُونَ  قُل لِّلۡمُؤۡمِنِينَ يَغُضُّواْ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِمۡ وَيَحۡفَظُواْ فُرُوجَهُمۡ

 

“Wambie waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa) na wazilinde tupu zao hili ni takaso kwao; bila ya shaka Allaah anazo habari za wanayoyafanya.” [An-Nuur: 30]

 

 

وَقُل لِّلۡمُؤۡمِنَـٰتِ يَغۡضُضۡنَ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِنَّ وَيَحۡفَظۡنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبۡدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنۡهَاۖ

 

“Na wambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokua vinavyodhihirika.” [An-Nuur: 31]

 

 

 

 

4. UVUTAJI SIGARA

 

Uvutaji wa sigara umeenea na kushamiri dunia nzima licha ya kuwa madhara yake yapo wazi. Baadhi ya Waislam wametumbukia katika balaa hili na kuziathiri nyumba zao bila ya kujijua. Kuna sababu tosha zenye kuonyesha uharamu wa jambo hili kwa Muislam. Sigara ina athari sana katika dini, afya, mazingira, familia, rasilimali na mengineyo.

 

i.                   MADHARA KATIKA DINI

 

Sigara inaathiri ‘Ibaadah ya mja na inapunguza malipo ya ‘Ibaadah hiyo. Kwa mfano ‘Ibaadah ya Swalah ambayo ni nguzo muhimu ya Muislam.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

“Mwenye kula Kitunguu maji au thwawm, basi asiukaribie Msikiti wetu na akae nyumbani” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tunaona makatazo yamekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na vitu hivyo ambavyo huwakirihisha watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini). Bila ya shaka mdomo wa mvutaji sigara una harufu mbaya zaidi kuliko vitunguu, ima huwakera watu na Malaika kwa harufu hiyo au kukosa fadhila za Swalah ya jamaa Msikitini kwa mwanamme.

 

 

ii.                 MADHARA KATIKA MWILI

 

Hakuna anayepinga madhara ya sigara katika mwili wa binaadamu. Utafiti wa kiafya umeyaona haya na kuyaeleza kwa kina; hata imekuwa ni sheria kuweka wazi maandishi ya tahadhari kwa kila paketi la sigara angalau watu wazinduke.

Ndani ya sigara hupatikana kemikali zenye sumu kama vile nicotine, arsenic, carbon monoxide na vyenginevyo ambavyo mvutaji huathirika kidogo kidogo hadi kuua sehemu muhimu za mwili wake. Athari zake ni kubwa na ni nyingi; husababisha cancer, TB, mshituko wa moyo, pumu, ubovu wa meno, na huwa ni  chimbuko la  maradhi mengi mengineyo.

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatuonya tusiwe wenyenye kujidhuru.

وَلَا تَقۡتُلُوٓاْ أَنفُسَكُمۡۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِكُمۡ رَحِيمً۬ا

“Wala msijiue, hakika Allaah ni mwenye kukurehemuni.” [An-Nisaa :29]

 Pia katika Suurat Al-Baqarah

وَلَا تُلۡقُواْ بِأَيۡدِيكُمۡ إِلَى ٱلتَّہۡلُكَةِ

“Wala msjiitie kwa mikono yenu katika maangamizo” [Al-Baqarah: 195]

 

 

iii.              ATHARI KWA AKILI NA MATAMANIO

 

Sigara huathiri akili ya mwanaadamu kwa kiasi kikubwa. Mvutaji mzoefu anapoikosa huwa vigumu kwake kufikiri kitu, kutatua tatizo au kuwa makini katika jambo mpaka aipate. Badala kuwa mtumwa wa Mola wake, hugeuka na kuwa mtumwa wa sigara yake na kuifanya dhaifu akili na hisia zake.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatueleza:

وَٱللَّهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيۡڪُمۡ وَيُرِيدُ ٱلَّذِينَ يَتَّبِعُونَ ٱلشَّہَوَٲتِ أَن تَمِيلُواْ مَيۡلاً عَظِيمً۬ا

“Allaah Anataka kukuhafifishieni. Lakini wanaofuata matamanio yao wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa” [An-Nisaa: 27]

 

 

iv.              MADHARA KATIKA MALI

 

Mvutaji sigara hupoteza pesa nyingi karibu kila siku kununulia sigara isiyomletea tija yoyote bali ni kuwafaidisha hao wanaoendesha bishara hii haramu. Kumbuka kuwa mali tunayoipata tutakuja kuulizwa kwa njia gani tumeichuma na vipi tumeitumia.

Allaah Anatueleza:

وَلَا تُؤۡتُواْ ٱلسُّفَهَآءَ أَمۡوَٲلَكُمُ ٱلَّتِى جَعَلَ ٱللَّهُ لَكُمۡ قِيَـٰمً۬ا وَٱرۡزُقُوهُمۡ فِيہَا

“Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allaah Amezijaalia kwa maisha yenu” [An-nisaa: 5] 

Pia katika Suurat Israa

وَلَا تُبَذِّرۡ تَبۡذِيرًا  إِنَّ ٱلۡمُبَذِّرِينَ كَانُوٓاْ إِخۡوَٲنَ ٱلشَّيَـٰطِينِۖ

“Wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu. Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa Mashaytwaan.” [Al-Israa: 26-27]

 

Ni vyema kutanabahi ndugu Muislam na kuachana na mazoea sugu na potofu ya kuvuta sigara. Mvutaji sigara huwa hajali kuvuta mbele ya wale waliomzunguka ndani ya nyumba yake, kama mkewe, watoto na wengineo. Huwasababishia kuvuta moshi wa sumu na wale walio karibu naye. Huleta hali mbaya hasa kwa mazingira ya ndani ya nyumba na ni mfano mbaya kwa kile kinachochungwa (mke na watoto) ndani ya nyumba hiyo.

 

 

5. MAMBO YA KUZINGATIA HASA KWA KINA MAMA

 

Miongoni mwa mambo yenye kuporomoa Uislam katika majumba ya Waislam ni udhaifu wa baadhi ya kinamama kuupuuza au kutoyatambua mafunzo muhimu yanayowahusu ambayo dini yetu yameyaweka wazi. Miongoni mwa hayo ni haya yafuatayo:

 

i.                   Kudhihirisha kwa Mapambo

 

Kawaida, wanawake huwa na mvuto wa kimaumbile, hivyo Uislam umeweka shari’ah maalum juu ya kuhifadhi maumbile hayo, heshima, staha pamoja na hadhi zao. Allaah Anatueleza:

 

يَـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّبِىُّ قُل لِّأَزۡوَٲجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَآءِ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ يُدۡنِينَ عَلَيۡہِنَّ مِن جَلَـٰبِيبِهِنَّۚ ذَٲلِكَ أَدۡنَىٰٓ أَن يُعۡرَفۡنَ فَلَا يُؤۡذَيۡنَۗ

“Ewe Mtume! Wambie wake zako na binti zako na wanawake wa Kiislam wajiteremshie uzuri shungi zao, kufanya hivyo kutapelekea wepesi wajulikane (kuwa ni watu wa heshima) ili wasiudhiwe.” [Al-Ahzaab: 59]

 

Ni mazoea ya wanawake wengi wanapotaka kutoka au kupata wageni majumbani mwao hudhihirisha mapambo yao yakiwemo maumbile yao kwa nguo za wazi au za kubana, manukato pamoja na mapambo mengine. Hali hii inaweza kusababisha vishawishi vingi, fitina na mtafaruku katika familia. Ni lazima tuwe waangalifu ni nani waliotuzunguka hasa wale wasiotakikana kuona mapambo hayo (wasiokuwa Mahrim). Allaah (Ta’ala) Anatuhimiza,

 

وَقُل لِّلۡمُؤۡمِنَـٰتِ يَغۡضُضۡنَ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِنَّ وَيَحۡفَظۡنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبۡدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنۡهَا‌ۖ

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yaona wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika.” [An-Nuur: 31]

Kujistiri kwa Hijaab ya kishari’ah kunapelekea kupata ridhaa ya Allaah (Ta’ala) na kutii amri Yake, kujitakasa pamoja na kuheshimika na wengine.

 

 

ii.                 Kutoka toka bila ya sababu maalum

 

Wanawake wa Kiislam hawajakatazwa kutoka nje ima kwa, kufanya kazi, kutembelea wazee, marafiki au katika shughuli za kijamii, ikiwa hakuna kipingamizi chochote cha shari’ah kitachowazuia. Muhimu ni kuchunga na kuilewa mipaka iliyowekwa katika dini ya Kiislam. Hata hivyo kutulia majumbani ni bora zaidi kwao na kutawaepusha na mambo mengi. 

 

Ulimwengu tulionao, kina mama wengi imekuwa ni adimu kutulia majumbani mwao, hii hupelekea familia kukosa utulivu, kizazi kukosa malezi na maadili mema kutokana na wazazi huwa hawana muda wa kutosha na watoto wao. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anatufahamisha:

 

وقَرۡنَ فِى بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجۡنَ تَبَرُّجَ ٱلۡجَـٰهِلِيَّةِ ٱلۡأُولَىٰۖ

“Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha wanawake wa zama za ujahili (ujinga)” [Al-Ahzaab: 33]

 

Hivyo ni lazima kwa kinamama kuzingatia ni sababu gani zitakazowatoa ndani ya majumba yao, kuwe na mtizamo na upeo wa hali ya juu kabla ya kuamua kutoka. Na ikibidi kutoka basi azingatie mipaka ya Allaah, kusiwe na aina yoyote ya mapambo kama vipodozi, manukato, udi na mengineyo. Awe amejihifadhi vizuri kwa mujibu wa shari’ah.  Kufanya hivyo kutahifadhi utu wao, dini yao pamoja na kizazi chao kwa ujumla.

 

 

HITIMISHO

Ni wajibu wa Waislam kudumisha mafunzo mazuri tuliyoekewa wazi katika dini yetu. Jamii bora huanza majumbani. Ni vyema kwa wasimamizi wa majumba kusaidiana na kushirikiana pamoja katika kulinda na kuhifadhi mazingira mazuri kwa kumuogopa Allaah (Ta’ala). Ni juu yetu kuwa waangalifu wa kile tunachokikuza, kwani wao husoma kutoka kwetu. 

 

Ni jukumu la kila mmoja wetu kusoma na kujifunza kitu gani Allaah Anapendezeshwa nacho na kipi Amekikataza hasa ndani ya majumba yetu ili tuishi hali ya kuwa Allaah Ameturidhia. Tuzipambe nyumba zetu kwa misingi ya Kiislam ili zitofautike na zile zisizo za Kiiislam. Huu ni ukumbusho kwa wenye kukumbuka.

 

Tumuombe Allaah Atuongoze katika haki na kuifuata, tuijue batili na kuicha, Atupe Tawfiyq, Atulinde na Kutuweka katika msimamo ulio sawa, Aamiyn.