Mume Ameritadi Baada Ya Kupata Ugonjwa, Anaishi Naye, Je Ndoa Yake Inasihi? Anaweza Kuolewa Na Mume Mwengine?

SWALI:

 

Mimi ni dada mwenye umri wa miaka 35 ambaye nimeolewa miaka saba iliyopita bahati mbaya mume wangu akapata ugonjwa wa kuupooza, katika kuhangaika akabadili dini na kuwa mkiristo, sasa mimi naishi naye bado je ndoa yetu tuliyofunga kiislamu bado ipo au imekwisha, na kama haipo naweza kuolewa tena, naomba msaada wenu kwangu, nijibu kupitia e mail yangu

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoa yako ya Kiislamu na mume aliyeritadi.

 

Allaah Aliyetukuka Anatufahamisha:

Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mshirikina hata akikupendezeni” (al-Baqarah [2]: 221).

 

 

Kwa hiyo, ikiwa mume ameritadi hapo ndoa imekatika. Kitu ambacho unaweza ni kujaribu kuzungumza naye ili arudi katika Dini ya Uislamu. Lau atakataa kata kata basi mtakuwa si mume na mke na ndoa yenu imekatika. Ikiwa ndoa ishakatika unaweza kishari’ah kuolewa tena na mume ambaye ni Muislamu.

 

Hata hivyo, nasaha yetu kwako ni unapopata posa basi jaribu kutafiti kuhusu mume anayetaka kukuoa. Na unapomuona kweli ameshika Dini basi kubali posa yake na uingie katika Nikaah baada ya kuswali Swalah ya Istikhaarah.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate manufaa zaidi:

 

Kuishi Na Mume Aliyeritadi Kwa Ajili Kumhudumia Ugonjwa

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share